Mabwawa ya Maji Taka eneo la VINGUNGUTI, Kuanza Uzalishaji wa Gesi ?
Mratibu wa Mradi wa kuzalisha
gesi ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa 4 katika fani ya Uhandisi wa
Mazingira, Chuo Kikuu cha Ardhi John Rutahirwa Akitoa ufafanuzi kwa
waandishi wa habari kuhusu moja ya mtambo wa kukusanyia maji taka kutoka
majumbani eneo la mradi wa kuzalisha gesi Vingunguti.Gesi hiyo itaanza
kutumika mwezi Desemba mwaka huu.
Mtaalam anayehusika na ujenzi,
mafunzo na usimamizi wa mfumo wa mradi wa kuzalisha Gesi
Vingunguti ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa nne wa shahada ya
Uhandisi wa Mazingira, Chuo Kikuu cha Ardhi Rukia Yange akitoa maelezo
kwa waandishi wa habari kuhusu maji taka yanayokusanywa eneo la
Vingunguti ambayo yatazalisha nishati ya Gesi na kuwahudumia wanaoishi
kuzunguka mabwawa ya Maji Taka Vingunguti.
Meneja Uhusiano wa DAWASCO Bi.Neli
Msuya (kulia) akiwa na Mtaalam anayehusika na ujenzi, mafunzo na
usimamizi wa mfumo wa mradi wa kuzalisha Gesi Vingunguti ambaye pia ni
mwanafunzi wa mwaka wa nne wa shahada ya Uhandisi wa Mazingira, Chuo
Kikuu cha Ardhi Rukia Yange wakionyesha moja ya kifungashio cha Gesi
itakayotumika majumbani Kutokana na maji taka yanayokusanywa eneo la
Vingunguti.Mradi huo unalenga kuwapunguzia wananchi gharama za uhifadhi
wa maji taka na kuwapatia nishati ya gesi kwa gharama nafuu
itakayowasaidia kuondokana na matumizi ya mkaa.
umanne Saidi Fundi ujenzi wa vyoo
na msimamizi wa mradi wa majaribio wa Biogasi Vingunguti akitoa
ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu kazi ya ufungaji wa miundombinu
ya kuzalisha gesi katika eneo la Vingunguti.
Mtambo wa kuzalisha Gesi katika
katika eneo la Mradi wa Majaribio eneo la Vingunguti unaokusanya maji
taka moja kwa moja kutoka katika makazi ya wananchi.Mtambo huo kwa
mujibu wa maelezo ya watalaam wa mradi huo una uwezo wa kukaa ardhini
kwa kipindi cha miaka 50.
Moja ya choo cha kisasa kilichojengwa katika moja ya familia kwa ajili ya mradi wa kuzalisha Gesi katika eneo la Vingunguti.
Eneo la Mtaa wa mji mpya
Vingunguti ambako mabomba ya kupitishia maji taka kutoka kwenye vyoo vya
wananchi ambayo huenda moja kwa moja kwenye mtambo wa kuzalishia Gesi.
……………………………………………
Na.Aron Msigwa – MAELEZO
Wakazi wa mtaa wa mji mpya, kata
ya Vingunguti, Manispaa ya Ilala jijini Dar es salaam wako mbioni
kuanza kunufaika na mradi wa uzalishaji wa Gesi inayotokana na maji taka
ya vyoo vyao na yale ya yaliyo katika mabwawa makubwa ya kuhifadhia
maji taka yaliyo katika eneo hilo.
Akizungumza na waandishi wa
habari katika eneo unapojengwa mradi wa majaribio wa kuzalisha Gesi,
Mratibu wa Mradi huo ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa 4 katika fani
ya Uhandisi wa Mazingira, Chuo Kikuu cha Ardhi John Rutahirwa amesema
kuwa wananchi wataanza kutumia gesi itakayozalishwa kuanzia mwezi
Desemba mwaka huu.
Amesema kazi ya kufanikisha
ujenzi wa miundombinu ya mradi huo inaendelea chini ya usimamizi wa
Mamlaka ya Maji Taka (DAWASA) kwa kushirikiana na Wanafunzi wa fani ya
Uhandisi wa Chuo Chuo Kikuu cha Ardhi na Taasisi isiyo ya kiserikali ya
wanafunzi wanaosomea fani ya uhandisi wa Mazingira (CDI) ya Chuo kikuu
cha Cambridge, Uingereza.
Amesema wanafunzi wanaosomea
fani ya Uhandisi wa Mazingira wa Chuo Kikuu cha Cambridge,Uingereza kwa
kushirikiana na baadhi ya wanafunzi wanaosomea Uhandisi wa Mazingira wa
Chuo Kikuu cha Ardhi nchini Tanzania walikuja na wazo na kubuni mradi
huo wenye lengo la kuboresha maisha kupitia maji taka.
Amesema chini ya uratibu wa
DAWASA yenye jukumu la kusimamia miundombinu ya maji taka na Taasisi ya
mikopo la Bridge for change ya Tanzania inayotoa mikopo midogo midogo
kwa wananchi walianza kufanya mapitio kwa kila nyumba ili kuona namna
wanavyoweza kutumia changamoto ya maji taka katika eneo hilo kwa
kuigeuza kuwa fursa.
Amefafanua kuwa wakihusisha
wataalm wa mradi na viongozi wa mtaa wa vingnguti mji mpya, walianza
kuzungumza na kujadiliana na wakazi wa eneo hilo ili kuwezesha kazi ya
kuunganisha vyoo vyao katika mtandao wa mabomba ya kusafirisha maji
taka kuelekea kwenye mtambo wa kuzalisha gesi.
Amefafanua kuwa chini ya mradi
huo maji taka yote kutoka kutoka katika nyumba zilizounganishwa kupitia
mabomba yanakusanywa na kusafirishwa moja kwa moja kwenye mtambo wa
kuzalisha gesi.
Kwa upande wake Mtaalam
anayehusika na ujenzi, mafunzo na usimamizi wa mfumo wa mradi huo ambaye
pia ni mwanafunzi wa mwaka wa nne wa shahada ya Uhandisi wa Mazingira
Chuo Kikuu cha Ardhi Rukia Yange amesema mradi huo ambao uko kwenye
majaribio unalenga kuwapunguzia wananchi gharama za uhifadhi wa maji
taka kwa kuwapatia nishati ya gesi kwa gharama nafuu itakayowasaidia
kuondokana na matumizi ya mkaa.
Amesema kwa kuanzia
utawanufaisha watu 150 wa eneo hilo na kuongeza kuwa kuanzia Desemba
mwaka huu wataanza kuiweka gesi hiyo katika vifungashio maalum
vitakavyoanza kusambazwa majumbani mwao tayari kwa matumizi.
Amesema gesi hiyo itamwezesha
mwananchi kuitumia kwa kipindi cha mwezi mmoja na kupunguza matumizi
makubwa ya mkaa na uharibifu wa mazingira.
Aidha, amesema gharama za
mwananchi kuunganishwa katika mfumo huo inaanzia shilingi 150,000/ kwa
wale walio na vyoo vinavyoruhusu mfumo huo na shilingi 700,000/= kwa
mwananchi anayetaka kujengewa choo kipya katika eneo lake la makazi
gharama ambazo hulipwa kidogo kidogo kupitia utaratibu wa mikopo nafuu
ulioanzishwa.
Naye Meneja Uhusiano wa DAWASA
Bi. Neli Msuya akifafanua kuhusu mradi huo amesema suala la ujenzi wa
miundombinu ya kuchukualia maji taka na matumizi ya gesi itakayozalishwa
litakwenda sambamba na utoaji wa elimu kwa wananchi hao juu ya matumizi
na uhifadhi wa gesi hiyo.
Amefafanua kuwa DAWASA
inaendelea kuendesha mafunzo ya uzingatiaji wa usalama katika matumizi
ya gesi hiyo pamoja na suala la usafi, utunzaji na ulinzi wa
miundombinu ya kusafirishia maji taka iliyojengwa katika eneo hilo ili
iweze kudumu kwa kipindi kirefu.
Ameeleza kuwa mbali na mradi wa
kuzalisha gesi DAWASCO kwa kushirikiana na wadau wa matumizi ya Nishati
endelevu na uhifadhi wa mazingira inatarajia kuanzisha mradi wa
kuzalisha mbolea itakayotokana na maji taka yaliyohifadhiwa katika eneo
hilo.
“DAWASA tukishirikiana na wadau
mbalimbali tuna mpango wa kuyatumia maji taka haya yaliyohifadhiwa
kuzalisha mbolea itakayotumiwa na wakulima katika shughuli za
kilimo,tunalenga kuibadilisha changamoto hii ya maji taka kuwa fursa
itakayowanufaisha wananchi badala ya kuwa kero kwao” Amesisitiza.
Wakiuzungumzia mradi huo baadhi
ya wakazi wa mtaa wa mji mpya ambao vyoo vyao vimeunganishwa kwenye
mfumo wa kusafirishia maji Taka wamesema mradi huo ni ukombozi katika
maisha yao kwa kuwa umewapatia vyoo bora na kuwaondolea adha na gharama
ya uhifadhi wa maji taka waliyokuwa wakiipata hapo awali kutokana na
ujenzi holela wa makazi yao.
Wameongeza kuwa mradi huo
umewasaidia katika uhifadhi wa mazingira na kuondoa tatizo la
utiririshaji wa muda mrefu wa maji taka uliosababishwa na uwepo wa
mifumo mibovu ya vyoo vyao.
Wamesema kuwa kutokana na
uimarishaji wa mifumo ya kusafirisha maji uliofanywa na DAWASA kwa
kushirikiana na Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Wanafunzi wa Chuo
Kikuu cha Cambrige (CDI) na Taasisi ya utoaji wa mikopo ya Bridge for
Change wameondoa hofu waliyokuwa nayo ya kupata magonjwa ya mlipuko
ikiwemo kipindupindu na kutoas wito kwa wananchi katika maeneo mengine
kujiunga na mradi huo.
Post a Comment