Mkurugenzi
wa Barabara, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Ven Ndyamukama, akitoa hotuba ya utangulizi katika
uzinduzi wa Mwongozo wa ujenzi wa Barabara zinazotumiwa na magari machache, uliozinduliwa leo jijini
Dar es Salaam.
................................
Serikali imezindua
mwongozo wa mpango na usanifu wa ujenzi wa barabara zinazopitisha magari
machache kwa lengo la kutoa maelekezo na kuwawezesha wahandisi wanaofanya
usanifu wa barabara hizo kutumia gharama nafuu za ujenzi.
Akizungumza katika
uzinduzi huo leo jijini Dar es salaam Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga amesema kuwa mwongozo
huu utakuwa tiba na kuwezesha Serikali kujenga barabara nyingi na gharama nafuu.
“Ujenzi na ukarabati ya
barabara zinazopitisha magari chini ya 300 kwa siku utakuwa wa gharama nafuu,
kama tutatumia mwongozo huu kwani utasaidia kutatua changamoto mbalimbali
zinazokabili barabara nyingi hususan za vijijini”, amesema Katibu Mkuu.
Amewataka wahandisi na
Mafundi ujenzi kutumia mwongozo huo katika utekelezaji wa majukumu yao ili
kuweza kusaidia kazi na miradi mbalimbali ya barabara kuweza kufanyika kwa
viwango vilivyo bora na gharama nafuu.
“Hakikisheni wahandisi
na Mafundi ujenzi mnafuata mwongozo huu ipasavyo na kuanzia sasa uwe dira kwenu
katika kazi zenu za kila siku”,
amesisitiza Eng. Nyamhanga.
Ameongeza kuwa
kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa Serikali imegundua uhitaji mkubwa katika
mtandao wa barabara nchini ili kusaidia maendeleo ya kila mwananchi mijini na
vijijini.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa Barabara katika Wizara hiyo Eng. Ven Ndyamukama amesema kuwa
mwongozo huo unafananua namna ujenzi wa
barabara hizo unavyokuwa ikiwemo kujenga kulingana na idadi ya magari yanayopita.
Ameongeza kuwa
Mwongozo huo unaelekeza kutumia rasilimali chache zilizopo na kuhakikisha masuala
ya mazingira katika maeneo yanayojengwa
barabara hizo yatazingatiwa.
|
Post a Comment