Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. George B.Simbachawene (MB) akikagua maendeleo ya Mradi wa kituo cha Afya katika kijiji cha Winza (Makao makuu ya kata ya Massa) ambapo asilimia kubwa ya mradi huo ipo katika hatua za mwisho, kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mpwapwa Bw. Donald Ng’wenzi. ..................................................................
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi),George Simbachawene ameziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuhakikisha zinatunga sheria ndogo ndogo kwa ajili ya uhifadhi vyanzo vya maji, barabara za mamlaka hizo na njia mbaya za kilimo zinazo athiri mazingira.
Simbachawene ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Kibakwe aliyasema hayo alipotembelea baadhi ya maeneo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa wilayani Mpwapwa ambapo alitembelea kata ya Massa na Ruhundwa katika vijiji vya Mkoleko, Makose, Chogola, Winza, Njia Panda na Ikuyu na alijionea hali halisi ya maendeleo ya wananchi katika vijiji hivyo.
Aidha alibaini kuwapo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na njia mbaya za kilimo katika kijiji cha Mkoleko na kumtaka Mkuu wa wilaya hiyo Bw. Jabir Shekimweri na timu ya wataalam wa wilaya kuchukua hatua za makusudi kunusuru hali ya mmomonyoko wa udongo unayotishia kutoweka kabisa kwa kijiji hicho.
“kamati ya huduma za Jamii ifanye kazi yake, mweke kontua na kuacha kulima na kukata miti katika kingo za makorongo ili kulinda mazingira” alisisitiza Simbachawene.
Amewaasa wananchi kutumia fursa za ujio wa makao makuu ya nchi mkoani Dodoma kwa kulima mazao ya chakula na biashara kwani miundo mbinu ya lami kutoka Mbande kuja Kongwa, Mpwapwa, Gulwe hadi Kibakwe ujenzi wake unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2017/2018.
“barabara yetu inayotoka Mbande, Kongwa, Mpwapwa, Gulwe, Kibakwe, Rudi hadi Chipogoro itajengwa kwa kiwango cha lami lakini awamu hii Serikali imetangazwa barabara ya lami kutoka Mbande kuja Kongwa, Mpwapwa, Gulwe hadi Kibakwe” alisema Mhe. Simbachawene.
Mhe. Simbachawene Akiwa katika kijiji cha Chogola ameziagiza Mamlaka za Serikali nchini kufuata Sera na Sheria lakini pia kutunga sheria ndogo ndogo zinazozingatia utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira kwani kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira vijijini.
Kuhusu ombi la wananchi wa kijiji cha Ikuyu kuanzisha kata mpya Mhe. Simbachawene amesema Serikali inapenda kubana matumizi kwa kuepuka uanzishaji wa maeneo mapya ya utawala yasiyo na tija kwa wananchi, hivyo ameshauri kata ya Ikuyu yenye vijiji vya Ikuyu, Kidenge, Mpwanila, Chang’ombe, Muungano na Ruhundwa ibaki kama ilivyo kwa kuwa eneo la kata mpya wanayoomba yenye vijiji vya Ikuyu, Chang’ombe na Muungano litakuwa dogo.
“Sisi kama Serikali ya awamu ya tano hatutaki kufanya vitu visivyo na tija kwa sababu ugawaji wa maeneo ya utawala ya vijiji, kata, halmashauri, wilaya na mikoa, hatudhani kama kufanya hivyo kunaondoa kero au shida ya wananchi, wananchi hawa wanashida za maji, barabara na kupata madawa hospitalini. Mimi nadhani tija ya wananchi sio kuigawa nchi hii katika vipande vidogo vidogo”, Alisema Mhe.Simbachawene.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mpwapwa Bw. Jabir Shekimweri aliwaagiza wananchi kata za Ruhundwa na Massa kupanda mazao yanayovumilia ukame kwa kuwa mwaka huu kunatarajiwa kuwa na mvua chini ya wastani pia alimwagiza Mtendaji wa Kata ya Massa kufuatilia masuala ya mazingira kwa ukaribu zaidi.
|
Post a Comment