Wafanyakazi wa TEMESA watakiwa Kujituma Ili Kutekeleza Majukumu yao Ipasavyo
Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Dkt.Musa Mgwatu (Kulia) akisalimiana na watendaji wa Wakala
huo, mara baada ya kufungua kikao kazi kwa watendaji hao, Jijini Dar es salaam.
|
Na Theresia Mwami TEMESA.
Wafanyakazi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA)
wameshauriwa kujituma kwa bidii katika kutekeleza majukumu yao ya kazi.
Ushauri huo umetolewa leo na Mtendaji Mkuu wa
TEMESA Dkt Musa Mgwatu alipokutana na watumishi hao kutoka katika Mikoa/vituo
vya TEMESA vilivyopo nchi nzima katika kikao kazi kilichofanyika Uwanja wa
Taifa Jijini Dar es Salaam.
Dkt Musa Mgwatu amesema kuwa ana muda mchache
tangu aanze kutekeleza majukumu yake na ameanza kujifunza mambo mbalimbali
kuhusu Wakala huu na kuahidi kupita katika vituo vilivyopo mikoani ili aweze
kujifunza zaidi.
“Naahidi kushirikiana nanyi katika kuijenga TEMESA
Mpya na naomba ushirikiano wenu na muwe wafatiliaji wa mambo kwani kazi zetu
zinahitaji sana ufatiliaji wa kina” Alisema Dkt Mgwatu.
Ameongeza
kuwa amepanga mikakati ya kuiimarisha TEMESA katika maeneo ya Matengenezo ya
magari kwenye karakana za TEMESA, namna ya kuyatambua madeni ya TEMESA pamoja
na utunzaji wa taarifa zake, utendaji kazi chini ya kiwango wa baadhi ya
karakana, mawasiliano kati ya TEMESA makao makuu na mikoa au vituo vyake na utendaji
kazi na watu au kampuni zilizosajiliwa.
Amesisitiza
kuwa watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili kuondoa dhana potofu
iliyojengwa juu ya TEMESA kwa wateja wake, wajiimarishe katika utendaji kazi
kwa kasi, ubora, weledi uadilifu, ufuatiliaji, na uwajibikaji.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za uendeshaji TEMESA Bw. Senzo Gwanchele
amesema kuwa kikao kazi hicho kimelenga kuondoa baadhi ya matatizo
yanayojitokeza katika utendaji wa kila siku ikiwemo hoja mbali mbali za ukaguzi,
ulipaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) pamoja na uzingatiaji wa sheria ya
Ununuzi wa Umma.
Wakala
wa Ufundi na Umeme (TEMESA) hivi karibuni imepata Mtendaji Mkuu mpya ambaye
amekuja na mikakati ya kujenga na kuimarisha TEMESA kwa kupambana na changamoto
zinazoikabili Wakala kwa sasa.
Post a Comment