Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (kulia) akipokea zawadi ya bango la picha zilizopigwa na baadhi ya Waandishi wa Habari waliowahi kujengewa uwezo na Tanzania Media Foundation 12 Julai, 2016 jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation, Bw. Ernest Sungura ameyataja baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa na Taasisi hiyo katika kuwajengea uwezo wanahabari nchini ambapo amesema kuwa, mpaka sasa wameweza kuwajengea uwezo jumla ya Waandishi wa habari wapatao 700 pamoja na Vyombo vya Habari 135.
Mbali na kuanza na miradi ya mwandishi mmoja mmoja, kwa sasa wanatarajia kuanza na miradi mingine inayoanza mwishoni mwa mwezi huu na itakuwa ni ya Awamu ya Pili ambapo itahusisha jumla ya Waandishi wa habari wapatao 30 kwenda vijijini kufanya kazi za kihabari na kupewa mafunzo ya namna ya kuandika habari za vijijini.
‘’Kwa sasa tumeanza mradi wa watu kubobea katika eneo maalum na safari hii tutajikita katika masuala ya Viwanda yaani kuwaandaa waandishi wa habari watakaobobea katika masuala ya viwanda na tayari tumeshamdokeza Waziri wa Viwanda kuhusu taarifa hizo kwa ajili ya kuizindua miradi hiyo’’, alisema Sungura.
Ameongeza kuwa katika kuandika masuala ya viwanda, tayari kuna waandishi wa habari wapatao 10 ambao hivi sasa wanajengewa uwezo ili waweze kuendana na kasi ya Serikali na katika suala la kuwandaa waandishi hao wanatumia Waandishi wa habari wazoefu pamoja na wadau wengine.
Amefafanua kuwa, lengo kubwa la kazi hizo zote ni kuwawezesha waandishi nchini kuweza kuyafikia maeneo ambayo yamekuwa hayafikiki, hivyo wanatoa rasimali fedha kwa waandshi hao ili kuweza kutembelea maeneo hayo na kuhabarisha umma.
‘’Ziko takwimu nyingi kila mahali kama vile za maji, afya, alimu lakini baadhi ya waandishi wetu hawafanyi ule uandishi wa kuzifanya takwimu hizo zieleweke na ziwe na manufaa kwa walaji, hivyo sisi tumeamua kuwajengea waandishi katika maeneo hayo’’, alisema Sungura.
|
Post a Comment