Header Ads

Benki ya EXIM ya China yaahidi Kuendeleza Ushirikiano na TANZANIA

Rais wa Benki ya Exim ya Nchini China Bw. Liu Liang amesema Benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufadhili miradi ya maendeleo ikiwa ni hatua ya kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya China na Tanzania unaolenga kuboresha, kujenga na kuinua uchumi imara kwa wananchi wa Nchi hizo.

Bw. Liang amesema hayo mbele ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano  Profesa Makame Mbarawa Jijini Dar es Salaam mara baada ya kukagua kituo mahiri cha Kuhifadhia Kumbukumbu (Internet Data Centre), kilichopo eneo la Kijitonyama ambacho ujenzi wake umefadhiliwa na benki hiyo.

Aidha amesifia kazi nzuri inayofanywa na Viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika jitihada zake za kusimamia vizuri miradi ya maendeleo ambayo itawaletea wananchi wake maendeleo ya haraka kwa kipindi kifupi.

“Naipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri inayofanya kwa kusimamia vizuri fedha zinazotolewa na wahisani kwa ajili ya utekelezaji wa  miradi ya maendeleo, na hivyo kutushawishi sisi kama benki ya Exim kuendelea kutoa fedha kwa miradi mbalimbali ya maendeleo", amesema Bw. Liang. 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza kulia)   akizungumza kumshukuru Rais wa Benki ya Exim ya nchini China Bw, Liu Lian’ge (hayupo pichani) mara baada ya kukagua kituo mahiri cha kutunza kumbukumbu (Internet Data centre) kilichopo eneo la kijitonyama Dsm.

Kwa upande wake Waziri Profesa Makame Mbarawa (Mb) ameipongeza Serikali ya China kupitia Benki hiyo kwa kuwa wadau wakubwa wanaochangia fedha kwa ajili ya maendeleo ya nchi na kuomba ushirikiano huo uwe endelevu kwa manufaa ya nchi hizo mbili.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayesimamia sekta ya Mawasiliano) Prof. Faustine Kamuzora amesema maendeleo makubwa kwenye ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yamesababisha uzalishwaji  mwingi wa data hivyo Serikali na Sekta mbalimbali wanahimizwa kutumia kituo hicho mahiri cha kuhifadhia kumbukumbu zao kwani zitakuwa salama.

Amesema huduma ya mtandao katika kituo hicho imeimarishwa kutokana na kuunganishwa na mkongo wa taifa na hivyo itawarahisishia wateja wake kuweka na kuchukua taarifa kwa haraka.

Kituo cha kutunza Kumbukumbu (Internet Data Centre)  ambacho ni cha kwanza kujengwa katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ni fursa mpya kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali wenye taarifa nyingi kuzihifadhi na kuzitumia wanapozihitaji,  kinalimikiwa na Serikali. 
Rais wa Benki ya Exim ya nchini China Bw, Liu Lian’ge (wa kwanza kushoto) akizungumza mara baada ya kukagua kituo mahiri cha kuhifadhia kumbukumbu ambacho kilijengwa kwa ufadhili wa Benki ya Exim ya nchini china.  
Rais wa   Benki ya Exim ya nchini China Bw, Liu Lian’ge  (wa pili kutoka kulia) akizungumza na  Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza kulia) wakati wakikagua kituo mahiri cha kuhifadhi kumbukumbu (Internet Data centre) kilichopo eneo la kijitonyama Dsm. 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto)  akishuka ngazi wakati wa kukagua kituo mahiri cha kutunzia kumbukumbu (Internet Data centre) kilichopo eneo la kijitonyama,  (wa kwanza kulia) ni Rais wa Benki ya Exim ya nchini China Bw. Liu Lian’ge.

No comments

Powered by Blogger.