Waziri WILLIAM LUKUVI atangaza Mageuzi Makubwa Sekta ya Ardhi Nchini
Na Mwandishi Wetu, DSM
Serikali imetangaza mkakati
mpya wa kupima na kuipanga ardhi yote nchini huku kipaumbele kikiwekwa katika
kuwapatia ardhi wawekezaji hasa katika sekta ya viwanda ndani ya siku saba tu
na kurasimisha makazi ya kaya maskini.
Magaeuzi hayo yametangazwa
jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
William Lukuvi alipokuwa akizungumza katika kipindi cha “TUNATEKELEZA”
kinachoandaliwa kwa pamoja kati ya TBC1 na Idara ya Habari-MAELEZO.
“Tumeanza kutekeleza mpango
wa miaka 10 wa kuhakikisha kila kipande cha ardhi katika nchi hii kinapimwa na
kupangiwa matumizi,” alisema akigusia kuwa mradi huo umeanza kutekelezwa mkoani
Morogoro na utaendelea nchi nzima.
Kutokana na mpango huo na pia
kubadilika kwa utendaji ndani ya wizara yake, Waziri Lukuvi anasema kuwa
kuanzia sasa wawekezaji wote nchini ni marufuku kwenda moja kwa moja vijijini
kununua ardhi.
“Wapite Kituo cha Uwekezaji
na kama pale watakosa ardhi waje wizarani kwangu. Tuna ardhi ya kutosha na
tunajua ilipo. Tutawapatia wawekezaji hasa wanaotaka kuwekeza katika viwanda
ardhi ndani ya siku saba tena bila rushwa wala urasimu,” alisema.
Katika kuhakikisha kuwa
wizara ya Ardhi inakuwa kitovu cha kusaidia utekelezaji wa azma ya Tanzania ya
viwanda, Waziri Lukuvi pia amegusia kuwa Serikali imeshatenga maeneo mbalimbali
nchini kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.
Alitaja kutengwa kwa
takribani viwanja 240 katika Manispaa ya Kigamboni, Dar es Salaam kwa ajili ya
viwanda na kwamba wizara yake inaendelea kubaini maeneo mengine nchini ikiwemo
kwa kuwanyang’anya ardhi hiyo watu waliojilimbikizia bila kuitumia.
“Zile nyakati za mtu
kujilimbikizia ardhi kubwa bila kuitumia zimekwisha. Mheshimiwa Rais ametuagiza
na sisi tunafanyiakazi, tumeamua sasa tutaitwaa ardhi hiyo na kuwa wanaotaka
kuwekeza,” alisisitiza.
Kuhusu tabia ya baadhi ya
watanzania kujilimbikizia viwanja na ardhi, Waziri Lukuvi amesisitiza kuwa
anaandaa mwongozo wa kuweka ukomo wa mtu kumiliki ardhi Tanzania. Mkakati huo
utakamilika ndani ya mwaka huu.
Akigusia makazi ya watu
maskini, alisema Serikali imekwishaanza utekelezaji wa mradi wa kurasimisha
makazi yaliyojengwa kiholela ili kuwapa hati wananchi wa maeneo hayo ili ardhi
yao iwe na thamani.
“Tumeanza zoezi hili kule
Kimara na Chasimba, Dar es Salaam. Wananchi wakiuelewa mradi huu vyema na kutoa
ushirikiano watafaidika nao kwani unalenga kuboresha makazi yao, kuwawekea
miundombinu muhimu na zaidi kuwapimia maeneo yao ili waweze kuwa na hati,’
alisema.
Waziri Lukuvi pia ametumia
muda huo kuwakemea maofisa wa umma wanaosababisha migogoro ya ardhi nchini na
kusisitiza kuwa muda wao wa kufanyakazi kwa mazoea na kiujanjaujanja umekwisha.
“Wananchi wengi wamedhulumiwa
ardhi tena kwa makosa ya watendaji wetu. Kwa Dar es Salaam tumeanza kuwapa
heshima ya kuwafidia wananchi wa aina hiyo kwa kuwapa viwanja vingine zaidi ya
600. Ole wao watendaji watakaoendelea kusababisha migogoro hiyo,” alionya.
Mpango wa Pili wa Miaka
Mitano unaazimia kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Maono na nia ya Waziri
Lukuvi katika kuleta mageuzi katika wizara yake ni chachu ya mafanikio ya azma
ya viwanda.
Post a Comment