Wanasayansi Wagundua Sayari Inayofanana na Dunia
Wanasayansi wamegundua sayari ambayo inakaribia sana Dunia kwa mazingira na ukubwa wake na ambayo inazunguka nyota ijulikanayo kama Proxima Centauri, iliyo na mfumo unaokaribia zaidi mfumo wetu wa jua.
Sayari hiyo, ambayo kwa sasa imepewa jina 'Proxima b' inazunguka nyota hiyo katika eneo ambalo kuna uwezekano mkubwa sana wa kupatikana kwa maji.
Proxima inapatikana umbali wa kilomita trilioni 40 na inaweza kumchukua mtu, akitumia teknolojia ya sasa ya vyombo vya usafiri wa anga za juu, maelfu ya miaka kufika huko.
Licha ya kwamba ni mbali sana, kugunduliwa kwa sayari hiyo huenda kukasisimua hisia na mawazo ya binadamu na wanasayansi kuhusu kuwepo kwa viumbe katika sayari nyingine au uwezekano wa wakati mmoja watu kuishi kwenye sayari nyingine.
"Kusema kweli, kufika huko kwa sasa hiyo ni kama hadithi ya kubuni kisayansi, lakini watu sasa wanalifikiria hilo na si jambo lisiloweza kufikirika kwamba wakati mmoja huenda watu wakatuma chombo huko," Guillem Anglada-Escudé, ambaye kundi lake la Pale Red Dot limechapisha matokeo ya ugunduzi wa sayari hiyo katika jarida la Nature amesema.
Mapema mwaka huu, bilionea Yuri Milner alisema atawekeza $100m katika utafiti wa kuunda chombo au kifaa kidogo kinachoweza kusafiri anga za juu kwa kutumia teknolojia ya laser.
Chombo kama hicho kinaweza kusafiri kwa pengine asilimia 20 ya kasi ya mwanga na hivyo kufupisha safari ya kufika kwenye nyota kama vile Proxima Centauri kutoka maelfu ya miaka hadi miongo kadha.
Ugunduzi wa sayari hiyo ulifanikishwa kupitia darubini ya kisasa yenye kifaa kujulikanacho kama HARPS.
Darubini hiyo imewekwa nchini Chile.
Takwimu kutoka kwa darubini hiyo zinaonyesha uzito wa Proxima b huenda ukawa mara 1.3 zaidi ya uzito wa dunia na kwamba inazunguka nyota ya Proxima katika umbali wa kilomita milioni 7.5. Huchukua siku 11.2 kumaliza mzunguko mmoja.
Umbali kutoka kwa nyota hiyo na sayari hiyo ni mfupi ukilinganisha na umbali kutoka kwa Dunia hadi kwa Jua (kilomita 149 milioni). Lakini Proxima Centauri ni 'nyota nyekundu mbilikimo'. Si kubwa sana na nguvu zake si nyingi kama za Jua hivyo safari inaweza kuwa karibu na nyota hiyo lakini iwe na mazingira sawa na ya dunia.
- Proxima Centauri ni 'nyota nyekundu mbilikimo'; ni ndogo na pia haina joto sana kama Jua
- Inakaribia zaidi lakini kuna uwezekano ikawa imeunganishwa kwa mvuto na Alpha Centauri A & B
- Kwa mtu anayetumia jicho lake kutazama juu angani Alpha Centauri A & B huonekana kama nyota moja
- Sirius A ndiyo nyota inayong'aa zaidi na inayotambulika kwa urahisi zaidi angani usiku
- Jupiter ndiyo sayari kubwa zaidi mfumo wetu wa Jua. Iwapo ingelikuwa na uzito mara 80 zaidi ya sasa, basi ingegeuka na kuwa jua
Post a Comment