Kasi ya Utendaji Kazi wa Rais Dkt JOHN MAGUFULI yaongeza Idadi ya Watalii Tanzania
Na Mwandishi Wetu
Kasi ya Rais Magufuli katika kuhakikisha Tanzania inajitegemea kwa kila mhusika kulipa kodi imeanza kulipa kufuatia takwimu kuonesha kwamba watalii wameongezeka nchini na hivyo kuongeza mapato zaidi Serikalini.
Ukweli huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof Jumanne Mghembe alipokuwa akizungumza kuhusu mikakati mbalimbali iliyotekelezwa na Wizara yake.
“Pamoja na kelele za sekta ya utalii baada ya Serikali kuanza kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika sekta ya utalii, lakini nakuhakikishia hivi sasa watalii wameongezeka nchini na mapato yamekua kwa asilimia 22 zaidi,” alisema Waziri Maghembe.
Waziri Maghembe ametanabaisha kuwa tofauti na mtazamo wa wadau wa sekta ya utalii ongezeko la kodi hiyo halijaathiri watalii wengi hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania inabaki kuwa na vivutio vya kipekee duniani.
“Nchi yetu ina vivutio vingi ambavyo havipo nchi nyingine yoyote. Hii ikijumlishwa na hali ya amani na utulivu iliyopo nchini, hakuna mtalii atakayeshindwa kugharamia ongezeko la dola nane tu,” alisema Waziri Maghembe.
Alitumia muda huo pia kueleza kuwa utafiti wake katika nchi za nje unaonesha kwamba Balozi za Tanzania zinaongoza kutoa viza kwa watalii mbalimbali ikilinganishwa na nchi nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki hasa katika miji mikubwa kama Berlin.
Akizungumzia vita dhidi ya ujangili, Waziri Maghembe amesema juhudi za Serikali kuwekeza katika mafunzo na vifaa vya kisasa zimezaa matunda pia baada ya ujangili kupungua nchini kwa kiasi kikubwa.
Alisema tayari watuhumiwa wakubwa wa mtandao wa ujangili wameshakamatwa na baadhi wamehukumiwa vifungo jela. Alimtaja mmoja wa watuhumiwa wakubwa wa mtandao huo raia wa kigeni ajulikanaye kwa jina la “Malkia wa Pembe za Ndovu” naye yuko mahabusu kwa sasa.
“Katika vita hii tumeamua kuuchukulia ujangili kama ugaidi au uhujumu uchumi. Tumekamata majangili wakubwa na wafadhili wao na bado vigogo zaidi tunaendelea kuwafuatilia na muda wowote tutawakamata,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali pia imepiga marufuku uvunaji wa mazao ya misitu hasa magogoro bila leseni na kwamba atakayefanya hivyo atakamatwa, mali na gari husika vitataifishwa na wahusika kufikishwa mahakamani.
Takwimu za kuongezeka watalii nchini zinaipa nguvu Serikali ya Rais Magufuli kwa sababu tangu alipoingia amekuwa akisisitiza sana katika umuhimu wa kukusanya kodi ili nchi ijitegemee. Tofauti na mtazamo huo, baadhi ya watu wamekuwa hawaamini kama hilo linawezekana.
Post a Comment