Header Ads

Serikali yapiga Marufuku Usafirishaji Wanyama nje ya Nchi

Na Hassan Silayo, MAELEZO

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe amesema kuwa serikali imepiga marufuku biashara ya kusafirisha wanyama hai nje ya nchi mpaka pale itakapowekwa misingi mizuri ili nchi iweze kunufaika na biashara hiyo.

Prof. Maghembe ameyasmea hayo wakati wa kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoandaliwa na Idara ya Habari-MAELEZO na TBC 1 ambapo alisema Serikali iliamua kuangalia upya utaratibu huo wa kuuza wanyama hai na kuamua kusitisha biashara hiyo hadi pale taratibu na misingi mizuri ya biashara hiyo itakapowekwa.

“Ni kweli kulikuwa na utaratibu wa kuuza wanyama hai nje ya nchi bila kuiwezesha nchi kupata faida yoyote ile, hivyo kwa sasa kama nchi tumeamua kupiga marufuku biashara kwa maslahi ya taifa”.

“Haiwezekani uuze wanyama hai nje halafu anayenufaika ni yule anayenunua na kuiacha nchi bila faida yoyote ya uwepo wa maliasili hiyo, hivyo kama nchi tumeamua kupiga marufuku biashara hiyo hadi pale misingi mizuri ya kibiashara itakapowekwa na kuiwezesha Tanzania kunufaika na rasilimali zake, na nisisitize kwa sasa hata Chawa wa Tanzania hataweza kusafirishwa nje ya nchi”. Alisema Prof. Maghembe.

Aidha, Prof. Maghembe alisema kuwa kwa sasa Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kupambana na ujangili wa wanyama pori kama Tembo na Faru ikiwemo kukamata watu wote wanaohusika katika biashara hiyo na mpaka sasa wameshakamata  baadhi ya watu akiwamo mwanamama anayejiita malikia wa pembe za ndovu ambaye alikuwa kinara katika biashara hiyo.

Prof. Maghembe aliongeza kuwa hatua hiyo imeonesha mafanikio kwani kwa kipindi cha hivi karibuni soko la mauzo ya pembe za ndovu nje nchi hasa bara la Asia ambao ndio walikuwa wanunuzi wakubwa wa bidhaa hizo yameshuka na hatua hiyo inatokana na mikakati iliyowekwa na Serikali.

Akizungumzia wizi katika mazao ya misitu Prof. Maghembe alisema kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua za kupambana na wizi wa mazao ya misitu na imekubaliwa kuwa iwapo gari litakamatwa likiwa na mazao hayo bila kuwa na kibali, Serikali itataifisha gari hilo na wahusika watashtakiwa kama wahujumu uchumi.

Pia Prof. Maghembe alisema kuwa kwa sasa utawekwa utaratibu wa magari yote yanayobeba mazao ya misitu kusafiri mchana kwenye gari lililo wazi ili kurahisisha ufuatiliaji na udhibiti wa wizi huo.


Serikali imeahidi kuanzisha miradi ya ufugaji nyuki kwenye vijiji vilivyo pembezoni mwa misitu ili kuweza kudhibiti uchomaji moto kwenye kwenye maeneo hayo hali itakayowezesha pia utunzaji wa mazingira.

No comments

Powered by Blogger.