Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia tamko alilokuwa akitoa Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye (hayupo pichani) la kufungiwa kwa Redio Five Arusha na Redio Magic FM Dar es Salaam leo Agosti 29,2016 Jijini Dar es Salaam.
“Uamuzi wa kuvifungia vituo hivyo umefikia baada ya kujiridhisha kuwa kipindi cha MATUKIO kilichorushwa tarehe 25 Agosti ,2016 muda wa 02:00 usiku hadi 03:00 usiku na Kituo cha Utangazaji cha Redio Five Arusha na kipindi cha cha Morning Magic katika kipengele cha KUPAKA RANGI kilichorushwa tarehe 17 Agosti, 2016 kati ya saa 01:00 asubuhi na saa 02:00 asubuhi vilikuwa na maudhui ya uchochezi unaoweza kuleta uvunjifu wa amani na hivyo kukiuka masharti ya kanuni ya 5 (a),(b),(c) na (d) pamoja na Kanuni ya Huduma za Utangazaji (Maudhui) za mwaka 2005”, alisema Waziri Nnauye.
Waziri huyo mwenye dhamana na vyombo vya habari nchini alisema vituo hivyo vimefungiwa kwa muda usiojulikana na ameelekeza Kamati ya Maudhui kuviita vyombo hivyo na kuwasikiliza kwa kina zaidi na kumshauri hatua zaidi za kuchukua kwa mujibu wa Kanuni za Utangazaji za mwaka 2005.
Pamoja na hayo Waziri Nape alivitahadharisha vyombo mbalimbali vya habari ,kutoshawishika kuvunja Sheria na Kanuni zinazoongoza tasnia ya Habari ili kulinda heshima ya tasnia ya habari na kuhakikisha nchi inabaki na Amani.
Hata hivyo Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ya mwaka 2003 Kifungu cha 28 (1) kimempa Mamlaka Waziri wa mwenye dhamana na masuala ya Habari kufungia vyombo vya habari vinavyoweza kurusha hewani habari za uchochezi.
|
Post a Comment