( MAKALA ) Jeshi la Polisi Lijipime Upya kwa Mauaji ya Wenzao Yaliyotokea MBANDE
Na Baraka Ngofira
Awali ya yote nianze kwa
kutoa pole kwa Jeshi la polisi, waziri wa mambo ya ndani ya Nchi ndugu Mwigulu
Nchemba, ndugu na jamaa wa Askari polisi 4 waliouawa kwa kupigwa risasi maeneo
ya mbande usiku Wa kuamkia jumatano ya Agosti 24.
Ni siku ya jumanne Usiku
majira ya saa tatu kasoro hivi naona picha ya polisi akiwa chini akiwa amepigwa
risasi huku damu nyingi zikiwa zimejaa chini na matumaini ya askari huyu kuamka
tena yakiwa hayapo.
Na baadaye kidogo napokea
ujumbe unaliandikwa Askari wanne wapigwa risasi maeneo ya Mbande wakiwa
wanalinda benki ya CRDB. Taarifa hii inanishtua na kuamua kuuliza watu wangu wa
karibu na kwenye makundi niliyanayo ya whatsApp ili nipewe namba ya Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Dar es salaam, Kamanda Sirro ili anipe uhakika wa tukio hilo. Lakini
pamoja na juhudi zangu zote naambiwa kamanda Sirro yupo eneo la Tukio japo simu
yake haikupokelewa tena baada ya kuambiwa kauli hiyo.
Huku nikiendelea kuwaza juu
ya tukio hilo, taarifa ya awali inakuja ikiwataja kwa majina askari wanne waliofariki
katika tukio hilo na cha kushangaza zaidi taarifa zinasema bunduki moja
waliyokuwa nayo polisi imechukuliwa na watu hao wanaosadikika kuwa ni majambazi
mara baada ya kutekeleza unyama huo.
Naingia kwenye mitandao ya
kijamii husasani Facebook huku nakuta mjadala mkali huku wengi wakifurahia kile
kilichowatokea askari hao. Kwa madai ya kuwa Askari polisi wamesahau jukumu lao
kuu la kumlinda raia na mali zake na kugeuka kuwa vipaza sauti vya watawala na
wanasiasa kutekeleza maagizo yao na kusahau kuwa sheria ni msumeno hukata mbele
na nyuma.
Mjadala huo unaendelea huku
zikiwa zimesalia siku chache kufika siku ya tarehe moja septemba iliyotangazwa
siku za hivi karibuni na viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini cha
Chadema. Kuwa itakuwa siku maalum ambayo
viongozi na wafuasi wake waandamana nchi nzima kupinga kile wanachokidai ni
Udikteta unaofanya na serikali ya awamu ya tano na kutaka kuwaziba midomo
wapinzani, huku wakiibatiza jina la Operasheni Ukuta yaani Umoja wa Kupinga
Udikteta Tanzania.
Siku za hivi karibuni
yameshuhudiwa makundi ya Askari polisi wakifanya mazoezi kikamilifu. Huku
wakiwa na silaha za moto, magari na vifaa vingine vya hatari ikiwemo magari ya
maji ya kuwasha, mabomu ya machozi, mbwa na mengineyo mengi. Ambapo taarifa ya
Jeshi la polisi iliyotolewa kwa Umma kuwa ni mazoezi ya kawaida kabisa na
kuwataka wananchi kuondoa woga kabisa.
Maonyesho haya ya polisi
ambayo ni ya aina yake tangu nipate ufahamu na kujitambua kuyaona yakifanyika mchana kweupe na katikati ya mji. Maana hata
rais wa nchi hii Dr. John Magufuli anasema haiwezekani nchi ambayo tumejitawala
kwa miaka zaidi ya 50 raia wake wakitaka kusafiri wanasindikizwa na askari
polisi.
Lakini cha ajabu ni kuwaona
askari hawa wakifanya mazoezi mjini na hadharani na kuonyesha mbinu mbalimbali
za kijeshi walizofundishwa na ambazo kimsingi zinapaswa kufanyika katika kambi
zao ambazo ninaamini kuwa zina maeneo makubwa na ya kutosha kabisa kufanya
mazoezi hayo.
Maana hali hii haijazoeleka
kabisa nchini hapa na hii imesababisha hofu kubwa kwa raia ambao wengi wao
wanajiuliza kuhusu amani gani tunayoitaja huku polisi wanazurura mitaani na
silaha za moto. Huku wakiwa wamejitayarisha tayari kupambana na adui au yeyote
atakayejitokeza mbele yao.
Hali hii imezua maswali mengi
sana miongoni mwa raia kujiuliza kweli wapo Tanzania nchi ambayo tunatamba na
kujivunia amani au ndo ni maeneo ya Somalia, Sudan au Kongo ambayo vyombo
habari kila siku vinaonyesha majeshi yakilandalanda mitaani na silaha za kivita
wakilinda amani na kuwasaka mahalamia na magaidi.
Tukio hili la mauaji ambalo
kwangu ni la kinyama na lisio na chembe ya ubinadamu hata kidogo linaumiza na
limeacha simanzi kubwa kwa wazalendo Wa nchi hii, na jamii kwa ujumla. Japo kwa
baadhi ya watu wamelipokea kwa furaha kutokana na hali halisi na tabaka ambalo
lilianza kujitokeza na sasa. Ambapo polisi wanalalamikiwa kutumiwa na watawala
na baadhi ya viongozi wa serikali kwa kile wanachokiita nguvu ya dola.
Jambo hili ambalo kwa sasa
limeifanya jamii kuwaona askari polisi kuwa adui machoni pao, na kuchangia
jamii kuwa na ushirikiano mdogo kwani kwa maeneo mengi sasa polisi na raia
wamekuwa kama paka na panya.
Na hivyo kuchangia jamii
kuwatunza waalifu au kushindwa kutoa ushirikiano kwa jeshi hili lengo jukumu la
kulinda raia na mali zao. Na ndiyo maana matukio mengi ya kuvamiwa na kuchomwa
moto kwa vituo mbalimbali vya polisi, na kuuliwa kwa Askari polisi yaliyotokea
mwaka jana na baadhi ya bunduki kuchukuliwa na watu waliotekeleza matukio hayo
yalichukua muda mrefu kwa watuhumiwa kukamatwa.
Hivyo basi ni muda mwafaka
sasa kwa viongozi wa jeshi la polisi kuona umuhimu wa kujenga ushirikiano na
jamii ili jamii iweze kutoa ushirikiano wa kutosha kuwafichua waalifu hasa wale
wanaotekeleza mashambulizi dhidi yao, na kuua askari polisi na baadhi ya
wanaovamia au kufanya uhalifu katika vituo vya polisi.
Hivyo basi kwa mauaji ya
askari wanne waliouliwa huko Mbande ambapo katika mitandao ya kijamii wahalifu
wameugwa mkono na watumiaji wengi ya mitandao hii. Ni kipimo tosha kwa jeshi la
polisi kujitafakari upya uhusiano wake na raia wanao walinda na kuwahudumia.
Itakumbukwa kuwa Askari
polisi ni ndugu zetu, ni mama, baba,Shangazi na wajomba zetu, lakini pia
wengine ni watoto, wadogo, kaka na Dada zetu.
Kwa nini
tupigane, kwa nini tusishirikiane ili tuweze kujenga taifa Bora na thabiti,
kuliko kuendeleza chuki na kinyongo mioyoni mwa raia, na jamii kwa ujumla na
kufanya majanga mbalimbali ikiwemo mauaji ya polisi ambayo yanathibitisha msemo
wa Kiswahili usemao Adui muombee njaa, ambayo kwa sasa mauaji hayo ya askari
yanapongezwa na raia huku polisi hawa tukiishi nao majumbani kwetu.
Na niimani
yangu kuwa vyombo vya usalama kwa kushirikiana na interejensia vinafanya msako
wa usiku na mchana ili kuwabaini waliohusika na tukio hilo hili waweze
kueachukulia hatua stahiki. Mungu ibariki Tanzania, ibariki na watu wake pia
waishi kwa upendo.
Makala haya yameandaliwa na Baraka Ngofira mwanafunzi wa
Shahada ya kwanza ya Mawasiliano ya Umma katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam,
anapatikana kwa mawasiliano ya 0763580901 au barua pepe ya
barakangofira@gmail.com.
Post a Comment