Mwanadiplomasia Dkt BERNARD ACHIULA amesema Hakuna Sababu ya Maandamano
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Tofauti za kisiasa zilizopo nchini zisivuruge nuru ya amani
iliyojengwa tangu enzi za Serikali ya Awamu ya Kwanza ambapo siasa za nchi
zililenga katika umoja, amani na ujenzi wa Taifa imara, anaonyesha mmoja
wa walimu wa diplomasia nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia nchini
(CFR), Dkt. Bernard Achiula wakati wa mahojiano na Mwandishi wa habari hii
kuhusu hali ya siasa nchini kwa sasa na ushiriki wa watanzania kwa ujumla
katika kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano katika utatuzi wa changamoto za
kimaendeleo badala ya kuanzisha tabia za vurugu na maandamano.
Dkt. Achiula amesema kuwa uwepo wa amani nchini unachangia katika
kuvutia wawekezaji nchini, kukuza utalii wa ndani, kuvutia wahisani kutoa
misaada kwa kuchangia katika uanzishaji na uendelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo hivyo kila raia nchini bila kujali itikadi yake ya dini wala chama
ana budi kuilinda amani iliyopo.
“Tofauti za kisiasa zipo katika kila nchi kulingana na mitazamo tofauti iliyopo
ila kinachotakiwa ni kuweka taifa mbele kwa manufaa ya nchi, watanzania
tunatakiwa kuwa wazalendo ili kuimarisha umoja na amani iliyopo kwani vitu
hivi vinategemeana na hatimaye kuiwezesha Serikali ya awamu ya tano kuwatumikia
wananchi kwa kuwaletea maendeleo.
“Tofauti hizo zisiwe chachu ya kuvuruga amani tuliyonayo bali
watanzania kwa ujumla tunatakiwa kuitunza amani hii iliyojengwa tangu enzi za
Mwalimu Julius Nyerere ili kuweza kuvutia wawekezaji na utalii katika
nchi yetu” alifafanua Dkt Achiula.
Alisema kuwa haoni sababu kwa vyama vya siasa nchini kuandaa
maandamano yanayolenga kuvuruga amani iliyopo kwani kikubwa kinachotakiwa kwa
wananchi ni misingi mikuu ya maendeleo ikiwemo elimu, afya na huduma bora
mbalimbali ambapo Rais Magufuli ameanza kuvifanyiakazi.
Akizungumza kuhusu Balozi zetu nje ya nchi Dkt Achiula aliwashauri
mabalozi hao kuzidi kuitanganza nchi yetu ya Tanzania ili kuweza kuvutia
wawekezaji, utalii na biashara ili kusaidia katika ukuuaji wa sekta ya viwanda
ambapo Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuipeleka nchi katika uchumi wa
viwanda.
Akizungumzia utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano Dkt Achiula
amesema kuwa Rais Dkt. Magufuli amejikita katika kutatua changamoto
zinazolikabili taifa kwa muda mrefu ikiwemo kupiga vita rushwa, kuongeza
ukusanyaji mapato kwa kuwabana wakwepa kodi, kubana matumizi ikiwa nia
ni kuimarisha uchumi wa nchi na kuipeleka nchi kwenye uchumi wa Kati.
Post a Comment