Wawakilishi wa TANZANIA kupeperusha Bendera Olimpiki 2016, BRAZIL
Na Raymond Mushumbusi WHUSM
Zikiwa zimebaki siku chache kabla kuanza rasmi michezo ya 31 ya Olimpiki mjini Rio de Janeiro nchini Brazilinayotarajiwa kuanza Ijumaa ya Agosti 4, 2016 katika mji wa Sao Paulo na Rio De Jeneiro nchini Brazil,
wawakilishi wa Tanzania katika michuano hiyo wamepata baraka zote kutoka kwa Serikali na kukabidhiwa bendera ya Taifa kabla ya kwenda kuipeperusha nchini Brazil.
Akikabidhi bendera kwa timu hiyo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia Wambura aliwataka washiriki wanaokwenda kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya Olimpiki mwaka huu huko Rio De Jeneiro nchini Brazil kujituma na kuhakikisha wanafanya vizuri ili warudi na medali.
Mhe. Annastazia Wambura alisema kuwa wanapokwenda kuiwakilisha waamini kuwa macho na masikio ya watanzania wote yapo kwao kwahiyo wajitahidi kadri ya uwezo wao kuweza kuhakikisha watakapokuwa wanarejea basi waje wakiwa wamevaa medali zao.
" Mnakwenda katika mashindano ya Olimpiki macho yote ya watanzania yapo kwenu tunategemea mkiwa mnarudi basi tutakuja kuwapokea mkiwa na medali zenu kifuani na hilo linawezekana kama mtajituma mkiwa na ari ya ushindi".
Aidha Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania , Filbert Bayi alisema kuwa kwa mwaka huu washiriki wamekaa kambi katika sehemu tofauti nchini na wengine wakiwa nje ya nchi na hilo limefanikisha kuweza kujifua vyema na kujiandaa ili kuweza kurejesha ushindi nyumbani.
Akizungumzia mara baada ya kukabidhiwa bendera Kocha wa timu ya kuogelea Bw. Alexandra Mwaipasi alisema kuwa wachezaji wake wameiva kwani mwanzoni walikuwa na changamoto ya kupata mabwawa yenye viwango vinavyoendana na mashindano hayo ili kwa matayarisho aliyowapatia wachezaji wake anahakika watarudi na medali.
Moja ya washiriki wa mchezo wa kuogelea katika mashindano ya Olimpiki kwa mwaka 2016 Magdalena Mosha alisema kuwa amejiandaa vizuri na anaamini kwa miaka aliyoshiriki kwenye mashindano ya Olimpiki ya Beijing na London yamempa uelewa zaidi wa nini anatakiwa kufanya na kuyafanyia kazi mazoezi aliyoyapata nchini Australia ili kurudi na ushindi.
Naye mmoja wa wawakilishi katika mchezo wa Judo, Adrew Thomas alisema amejiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano hayo na yuko tayari kuiwakilisha Tanzania na kuleta ushindi na pia kuitangaza Tanzania katika michezo na utalii uliopo kwa kuvitangaza vivutio vilivyopo nchini.
Kwa upande wake Sara Ramadhani ambaye ni mwakilishi mwanamke pekee katika mshindano hayo kwa wakimbiaji wa Marathon alisema yuko vizuri kuipeperusha bendera ya taifa na kuitangaza Tanzania kimataifa kwa kushindana na kushinda medali hivyo kuiletea sifa nchini.
Mmoja wa wadhamini wa safari hiyo kampuni ya Multichoice Africa, imewataka washiriki hao kujituma zaidi kwani watanzania wote watakuwa wanawaangalia kupitia chaneli zao zinazopatikana kwenye kisimbuzi cha DSTV.
Katika mchango wao kwa wawakilishi hao Kampuni ya visimbuzi ya Dstv imetoa mchango wa kuwakutanisha pamoja kwa kuandaa hafla ya kuwaaga wawakilishi hao ikiwa ni moja ya kuwatia moyo waende kupambana na kushinda katika michezo mbalimbali na kuliletea sifa taifa.
Akizungumza kwa niaba ya kampuni hiyo Mkurugenzi wa Multichoice Tanzania Maharage Chande alisema mwaka huu mashindano yote yatakuwa yakioneshwa moja kwa moja kupitia channeli za Super Sport na itawapa fursa watanzania kuwashuhudia wawakilishi wao kwenye mashindano hayo makubwa duniani.
Bodi ya Utalii nayo haikuwa nyuma kuwapa nguvu na morali wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Olimpiki kwenda kufanya vizuri katika mashindano hayo na pia kutangaza vivutio vilivyopo nchini kwa mataifa mbalimbali yanayoshiriki mashindano hayo kwa kuwapatia vifurushi kwa ajili ya kusambaza ujumbe kuhusu utalii wa Tanzania.
Akitoa nasaha zake kwa wawakilishi hao Mkurugenzi wa Utalii Bw. Godfrey Tengeneza aliwaasa wawakilishi hao kujituma kwa bidii na kutangaza nchi kupitia michezo na pia watumie fursa hiyo kutangaza vivutio vilivyopo Tanzania kwa kueneza habari kuhusu utalii Tanzania.
“Mtakapokuwa huko mbali na kushiriki katika michezo muitangaze nchi yetu kwa vivutio vilivyopo nchini ili tuzidi kupata watalii wengi kutoka duniani kote”.
Timu ya Tanzania inayoenda kushiriki mashindano ya 31 ya Olimpiki nchini Brazil inawakilishwa na wachezaji saba ambao ni waogeleaji wawili Magdalena Mosha anayeenda kwa mara ya tatu kwa upande wa wanawake huku Hilal Hilal akienda kwa mara ya kwanza kwa upande wa wanaume na wote watakuwa ni waogeleaji kwa umbali wa mita 50.
Wengine ni Fabian Joseph, Said Juma Makula na Alphonce Felix Simbu watakaokimbia marathon kwa wanaume na Sara Ramadhani ambaye ni mwanamke pekee anayeiwakilisha Tanzania katika mbio za marathon.
Na kwa upande wa mchezo wa Judo Tanzania itawakilishwa na Adrew Thomas Mulugu katika uzito wa kilogramu 73.
Katika mashindano ya Olimpiki mwaka huu takribani M yanatarajiwa kushindana katika michezo mbalimbali huku Marekani ikiongoza kuwa na wachezaji wengi zaidi katika mashindano hayo ikiwa na wachezaji 550 ikifuatiwa na Brazil iliyo na wachezaji 450 na China inayowakilishwa na wachezaji 380.
Post a Comment