Vijiji 73 Wilayani Ruangwa Kuunganishiwa Nishati ya Umeme
Na Rhoda James, Lindi
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt Medard Kalemani amesema kuwa Vijiji Vipatavyo 73 vya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi vitaunganishiwa umeme kupitia mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu ( REA Phase III).
Dkt. Kalemani aliyasema hayo hivi karibuni wakati alipofanya ziara ya siku mbili mkoani Lindi ikiwemo Wilaya ya Ruangwa lengo likiwa ni kutathimini utekelezaji wa miradi ya REA Awamu ya Pili.
Alisema kuwa tathmini hiyo ya REA II, inasaidia kubaini changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa miradi hiyo ya umeme vijijini Awamu ya Pili na hivyo kuboresha utekelezaji wa REA Awamu ya III ulioanza mwezi Agosti mwaka huu.
Kuhusu wilaya ya Ruangwa, Dkt. Kalemani alisema kuwa wilaya hiyo ina jumla ya vijiji 90 ambapo kati ya hivyo ni vijiji 13 tu ndiyo vimeunganishiwa umeme.
Aidha, Dkt. Kalemani alisema kuwa vijiji vyote katika Mikoa ya Lindi na Mtwara ambavyo havikupata umeme kupitia REA Awamu ya Pili vitaunganishiwa umeme kupitia REA Awamu ya Tatu ili kuweza kuharakisha maendeleo katika Mikoa hiyo.
“Nachukua fursa hii kukumbusha tena kuwa, wale wakandarasi ambao hawakufanya kazi nzuri ya usambazaji umeme vijijini katika Awamu ya Pili wasitegemee kufanya kazi tena na Serikali hasa katika kusambaza umeme vijijini,” alisema Dkt. Kalemani.
Alisema kuwa gharama ya kuunganishiwa umeme huo vijijini bado ni shilingi 27,000 na pia hakuna kulipia fomu ya maombi ya kuunganishiwa umeme ambayo hapo awali ilikuwa ikinunuliwa kwa shilingi 5000.
Dkt. Kalemani aliongeza kuwa kwa wananchi wasiokuwa na uwezo watafungiwa kifaa cha umeme kiitwacho ‘UMETA’ yaani ‘Umeme Tayari’ ambacho hakimhitaji mwananchi kuingia gharama ya kusuka nyanya za umeme ndani ya nyumba (wiring) hivyo mwananchi ataepusha gharama hizo za wiring.
Vilevile aliwaagiza watendaji wa TANESCO kuhakikisha kuwa wanawafuata wateja sehemu walipo badala ya kuwasubiri ofisini na kueleza kuwa wananchi walio wengi hawana uwezo wa kifedha wa kuwafuata TANESCO maofisini.
“TANESCO ni wajibu wenu sasa kuwafuata wananchi pale walipo, wengi wao hawana uwezo wa kifedha wa kuwafuata ninyi maofisini, na wengi ni wazee hivyo basi wafuateni na sio wao kuwafuata,” alisema Dkt. Kalemani.
Katika ziara hiyo Dkt. Kalemani alitembelea vijiji vya Narung’ombe, Chunyu, Mbekenyera, Namichiga, Nambilanje, Chienjele, Namahema, Nandagala na Luchelegwa vyote vya wilayani Ruangwa.
Post a Comment