OSHA kuendesha Zoezi la Upimaji Afya za Waliokuwa Wafanyakazi wa Mgodi wa BULYANHULU
Na Mwandishi Wetu
Wakala
wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) utaendesha zoezi maalum la upimaji
afya za waliokuwa wafanyakazi wa mgodi wa Bulyanhulu ambao waliachishwa kazi na
mgodi huo mnamo mwaka 2007 bila kupimwa afya zao kinyume na Sheria ya Usalama
na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.
Baada
ya ukikwaji huo wa sheria kuripotiwa kwa Wakala, hatua stahiki zilichukuliwa
ikiwemo kufanya kaguzi maalum za usalama na afya katika eneo la mgodi na kutoa
onyo kali kwa mwajiri wa walalamikaji pamoja na kugharimia upimaji afya za
waathirika wote.
Katika
kushughulikia tatizo hilo, vikao vya mashauriano vilivyojumuisha serikali,
mwajiri (Mgodi wa Bulyanhulu) na waathirika kupitia chama chao, TAMICO,
vilifanyika na utaratibu wa kushughulikia suala hilo ukawekwa. Katika utaratibu
huo, TAMICO ilipewa jukumu la kuwatafuta waathirika wote popote walipo na
kuwasilisha majina yao kwa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi. Wakala
ulikuwa na jukumu la kuyapeleka majina hayo kwa mwajiri kwaajili ya uhakiki na
kuratibu upimaji afya wa waathirika hao baada ya majina yao kuhakikiwa.
Hadi
kufikia sasa tayari waathirika 315 kati ya 371 ambao mwajiri alithibitisha
kwamba walikuwa wafanyakazi wake wameshapimwa afya zao. Waathirika 56 waliobaki
hawakujitokeza wakati wa upimaji afya licha ya kupewa taarifa juu ya zoezi
hilo.
Waathirika
watakaopimwa kwasasa ni wale ambao vipimo vyao vya awali vilionesha kwamba
wanahitaji vipimo zaidi kutoka kwa madaktari bingwa.
Maandalizi
ya upimaji huu yamekamilika na zoezi hili litafanyika katika hospitali ya Taifa
ya Muhimbili siku ya Jumamosi tarehe 20/08/2016 na katika hospitali ya rufaa ya
Bugando mnamo tarehe 22/08-15/09/2016. Katika zoezi hili waathirika ambao
orodha ya majina yao imeambatanishwa katika taarifa hii wataonana na madaktari
bingwa wa magonjwa ambayo wana dalili nayo ili kubaini kama wana matatizo
kiafya na hatimaye kuweza kutazama kama matatizo waliyo nayo yametokana na kazi
walizokuwa wakifanya mgodini.
Kwa
waathirika ambao madaktari watathibitisha kwamba matatizo yao ya kiafya yamesababishwa
na kazi walizokuwa wanafanya, Wakala utashauri namna ambavyo
wanapaswa kufidiwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Waathirika ambao watakutwa na
matatizo ya kiafya ambayo hayatokani na kazi, watashauriwa kuendelea na
matibabu katika hospitali zilizopo karibu nao.
Aidha
kwa waathirika ambao hawatakutwa na matatizo yoyote ya kiafya watapatiwa vyeti
vyao (certificate
of fitness) ambavyo hutolewa kwa wafanyakazi wanaopimwa afya zao baada
ya kukoma kwa ajira zao kwa mujibu wa kifungu Na.24 (2) cha Sheria ya Usalama
na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.
Ikumbukwe
kwamba, upimaji huu ni mwendelezo wa hatua mbali mbali zinazochukuliwa na
serikali katika kushughulikia tatizo hili ambalo lilitokea mwaka 2007 ambapo waliokuwa
wafanyakazi wa mgodi wa Bulyanhulu waliachishwa kazi na mwajiri wao baada ya
kugoma kufanya kazi. Hata hivyo mwajiri wao (Mgodi wa Bulyanhulu) haukuweza
kuwapima afya zao kama Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003
inavyomtaka.
Mwisho,
kwakuwa suala hili ni la kisheria na serikali ina nia ya dhati ya kulishughulikia,
tunaomba ushirikiano kutoka pande zote (waathirika na mwajiri) ili kuhakikisha
kwamba zoezi hili linatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
Imetolewa na;
Dkt. Akwilina
Kayumba
Mtendaji Mkuu
Post a Comment