Header Ads

Mgogoro wa Pori la Akiba la MKUNGUNERO Kondoa Vijijini waanza Kupatiwa Ufumbuzi

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia) akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Keikei Wilayani Kondoa jana kwa ajili ya kusikiliza kero zao mbalimbali kuhusu Pori la Akiba Mkungunero. Wananchi hao wameiomba Serikali iwape maeneo kwa ajili ya Kilimo, Ufugaji na Makazi kutokana na uhaba wa ardhi katika maeneo hayo. 

Naibu Waziri Makani aliwaomba wananchi hao kuwa na subira wakati huu Serikali inapoenda kushuulikia maombi yao ambapo tayari imeshaundwa tume ambayo ipo chini ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kukusanya takwimu mbali mbali ikiwemo mahitaji halisi ya ardhi na idadi ya watu ambapo zitatumika katika kutatua changamoto zilizopo. 


Alieleza kuwa Serikali ya awamu ya tano imepanga kutatua kero mbalimbali za  wananchi ambapo tayari migogoro yote ya ardhi nchini imeshaorodheshwa kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu, ambapo kitaundwa kikosi kazi cha kitaifa kitakachohusisha Wizara ya Ardhi, Kilimo, Maliasili, Tamisemi, Sheria na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira.


Eng. Makani alisema kuwa Tanzania bado ina maeneo mengi ambayo yanaweza kutumika kwa ajili ya kilimo na ufugaji, hivyo kumega hifadhi ili kukabiliana na tatizo uhaba wa ardhi itakuwa jambo la mwisho kufanyika baada ya maeneo mengine kuzingatiwa. Aliitaka tume iliyoundwa kukamilisha kazi yake haraka ili changamoto hiyo iweze kupatiwa ufumbuzi na mamlaka husika.


Pori la Akiba Mkungunero lilitangazwa rasmi na Tangazo la Serikali la mwaka 1996 na zoezi la kutafsiri mipaka husika likafanyika mwaka 2006. Tangu hapo ukaanza mgogoro kati ya wananchi na hifadhi kwa madai kuwa baadhi ya vitongoji vya vijiji vyao halali vipo ndani ya hifadhi hiyo. 


Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini, Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (kulia) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango akizungumza na wananchi wa Jimbo lake wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika kijiji cha keikei Wilayani Kondoa.

 Dkt. Kijaji aliwasilisha kero na changamoto mbalimbali za wananchi wake, moja ikiwa ni uhaba wa maeneo kwa ajili ya kilimo na ufugaji,  maeneo ya vijiji halali vilivyopimwa kudaiwa kuwemo ndani ya hifadhi na mahusiano mabaya kati ya wananchi wake na watumishi wa Pori la Akiba Mkungunero. 


Akijibu changamoto hizo, Naibu Waziri Makani aliahidi kuzifanyia kazi kwa mujibu wa sheria za nchi na taratibu zilizowekwa mara baada ya tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa kukamilisha kazi yake na kukabidhi taarifa na mapendekezo yake Wizarani.  Aliongeza kuwa kumega maeneo ya hifadhi haiwezi kuwa jibu pekee la changamoto zinazowakabili wananchi bali wanaweza kutumia maeneo madogo waliyonayo kwa kuweka mipango mizuri ikawa na tija zaidi kwa taifa na watu wake.


Mwananchi wa Kijiji cha Kisondoko, Khalifa Othman akiwasilisha kero zake wakati wa mkutano huo. Kilio chake kikubwa kilikuwa kupatiwa maeneo kwa ajili ya ufugaji na kilimo. Kulia aliyesimama ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Vijijini ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kwadelo, Omari Kariati. Kushoto ni Naibu Waziri, Eng. Ramo Makani.

  Mkazi wa Kijiji cha Kisondoko Wilayani Kondoa akitoa kero zake kwenye Mkutano huo. Aliiomba Serikali kuzisaidia jamii za Wabarbaij na Wamang'ati kupata maeneo ya kulima na kufuga kwakuwa kwa sasa jamii hizo zimetengwa na hazina kabisa maeneo kwa ajili ya shughuli hizo, "Sisi Wamang'ati hatuna hata kipande cha ardhi na tukifa hatujui tutazikwa wapi" alieleza. 

 Naibu Waziri Makani akiendelea kuongoza mkutano huo. Alifikisha salam za Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa wananchi hao ambapo aliwataka, Kudumisha amani ya nchi yetu, kutumia amani hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha zaidi kukuza uchumi wa taifa letu. 

Baadhi ya wajumbe walioshiriki mkutano huo. 

(Picha na Hamza Temba - WMU)

No comments

Powered by Blogger.