Mamia Wapigwa Picha wakiwa Utupu nchini Uingereza
Watu zaidi ya 3,000 walipigwa picha wakiwa utupu nchini Uingereza chini ya mradi wa kuadhimisha na kusherehekea utamaduni.
Mradi huo uliopewa jina Bahari ya Hull unatumiwa kusherehekea mji wa Hull kama Mji wa Utamaduni kwenye sherehe kuu mwaka ujao.
Baraza la Jiji la Hull lilisema mradi huo wa sanaa, ndio mkubwa zaidi wa aina yake kufanyika Uingereza.
Uliendeshwa na mpigapicha mashuhuri duniani Spencer Tunick na kushirikisha watu 3,200 kutoka nchi 20, ambao walipigwa picha katika maeneo mbalimbali maarufu mjini humo Jumamosi iliyopita.
Picha hizo, ambazo zinasimamiwa na shirika la maonesho ya Sanaa la Ferens Art Gallery, zitawekwa kwenye maonesho wakati wa shughuli za Jiji la Utamaduni Uingereza mwaka 2017.
Maelfu ya watu walifika kabla ya jua kuchomoza na wakapakwa rangi ya samawati iliyokozwa kwa viwango vinne, kuashiria maji.
Walipigiwa picha maeneo mbalimbali yakiwemo Bustani ya Malkia, Guildhall na daraja la Scale Lane.
Shughuli yote ilidumu saa nne.
Mmoja wa walioshiriki alikuwa Stephane Janssen, mwenye umri wa miaka 80 anayetoka Brussels.
Ameshiriki miradi ya upigaji picha wa watu wengi wakiwa utupu ya Tunick mara 20 awali.
“Ni maridadi sana, ni kupakwa rangi kidogo tu. Kila mtu ni sawa – hakuna tofauti ya rangi au jinsia – kila mtu ni sawa na yule mwingine akiwa utupu, na hilo ndilo napenda,” alisema.
Sarah Hossack, kutoka Hull, alisema alifurahia sana.
Post a Comment