WANANCHI WAMETAKIWA KUUCHUKIA UHALIFU KWA VITENDO
Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi.
……………………………………………..
Wananchi wametakiwa kuuchukia
uhalifu kwa vitendo pamoja na kuwa na kauli moja katika kupambana nao
kwa kushirikiana na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na
wahalifu ili kukomesha vitendo hivyo hapa nchini.
Hayo yalisemwa jana na Naibu
Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki wakati alipokuwa
akifungua semina ya siku moja katika ukumbi wa Nkurumah iliyokuwa na
kauli mbiu ya Kataa uhalifu iliyoandaliwa kwa pamoja kati ya Jeshi la
Polisi na Shule kuu ya Sheria ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam kwa lengo
la kupambana na uhalifu hapa nchini, semina ambayo iliwashirikisha
wahadhiri, maofisa wa Polisi na wanafunzi wa chuo hicho.
Kaniki alisema wananchi
wakiukataa uhalifu watawezesha jamii ya watanzania kuwa salama na
kuondoa vikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuwa uhalifu ndio
kikwazo katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali.
Aidha aliwaomba wasomi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam
hususani wanaosomea shahada ya sanaa katika utekelezaji wa sheria
kufanya tafiti ambazo zitaweza kulisaidia Jeshi la Polisi katika kutatua
kero za uhalifu hapa nchini.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa
Chuo kikuu cha Dar es Salaam Prof.Rwekaza Mukandala alisema jukumu la
kupambana na uhalifu sio la jeshi la polisi pekee bali ni jukumu la watu
wote.
Aliongeza kuwa kwakutambua hilo
mwaka 2009 walianzisha shahada ya utekelezaji wa sheria ambayo asilimia
kubwa ya wanafunzi wanatoka katika vyombo vya ulinzi na usalama na
wakufunzi wa shahada hiyo ni maofisa kutoka katika Jeshi la Polisi.
Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai nchini (DCI) Diwani Athuman alisema kauli mbiu hiyo ya
kataa uhalifu ilibuniwa na Shirikisho la Polisi wa Kimataifa (INTERPOL)
ili kutimiza malengo yake ya kuwa na dunia iliyo salama kwa binadamu
ambapo kwa hapa nchini ilizinduliwa mwaka jana kwa kushirikisha wadau
mbalimbali.
Alisema katika semina
hiyo wajumbe watapata fursa ya kujadili kwa pamoja makosa yaliyopo hapa
nchini yakiwemo ya madawa ya kulevya, ujangili, mauaji ya albino,
mauaji ya vikongwe, kujichukulia sheria mkononi , waham,iaji haramu
pamoja na usafirishaji haramu wa binadamu.
Post a Comment