SHIRIKA LA BIASHARA LA TAIFA ZANZIBAR (ZSTC) LAFANYA MKUTANO NA WAKULIMA WA KARAFUU MKOA WA KUSINI
Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Dkt.
Idrissa Muslih Hijja akifungua Mkutano wa Wakulima wa zao la Karafuu wa
Mkoa Huo uliofanyika Skuli ya Dunga.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika
la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) Mwanahija Almas Ali akizungumza na
wakulima wa zao la Karafuu katika mkutano uliofanyika Skuli ya Dunga.
Afisa kutoka Wizara ya Kilimo na
Maliasili Badru Mwemvura akitoa tathmini ya ugawaji wa miche ya
mikarafuu inayotolewa na Wizara ya Kilimo na Maliasili katika mkutano wa
wazalishaji wa zao la karafu wa Mkoa Kusini Unguja.
Baadhi ya wakulima wa zao la karafuu wakifuatilia mkutano huo uliofanyika Skuli ya Dunga.
Habari Picha- na Makame Mshenga- Maelezo Zanzibar.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika
la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) Mwanahija Almas Ali amewataka
wakulima wa zao la Karafuu kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na
Serikali katika kuhakikisha ubora wa zao la Karafuu za Zanzibar
unabakia ili kukidhi vigezo vya sifa vya Kimataifa.
Akizungumza katika mkukutano wa
Wakulima wa Karafuu wa Mkoa Kusini Unguja uliofanyika Skuli ya Dunga
amesema lengo la Serikali katika kilimo cha zao la Karafuu ni kuona
linaendelea kuwa tegemeo katika kuingiza fedha za kigeni na kusaidia
kukuza Uchumi hivyo linahitaji kulindwa na kila Mwananchi kwa kuongeza
uzalishaji na kulinda ubora.
Mwanahija ameeleza kuwa Karafuu ni
zao la Kilimo lenye faida kubwa katika kuimarisha uchumi na ametaka
kila mmoja ashiriki katika kulikuza na kuliendeleza ili kuhuisha ustawi
wa wakulima na wananchi kwa jumla.
“Kukuza Kilimo cha Karafuu ni sawa
na kukuza maendeleo ya Zanzibar, jitihada za makusudi zinahitajika ili
lengo la Serikali liweze kufikiwa,” alisisitiza Mkurugenzi Mwendeshaji
ZSTC.
Amewataka wakulima wa zao hilo
kuchukua jitihada za makusudi kuhakikisha usafi wa Karafuu unaimarika
kwa vile hadaa na uchafuzi wa zao hilo ni hasara kwa wakulima, wananchi
na Taifa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
ya ZSTC Kassim Maalim Suleiman amewataka Wakulima wa zao la Karafuu
kutumia utaalamu wa kisasa na kuachana kuendeleza Kilimo hicho kwa
mazoea.
Aidha amewashauri Wakulima hao
kufungua akaunti benki ili waweze kuingiziwa fedha moja kwa moja baada
ya kuuza Karafuu zao na kuachana na tabia iliyozoeleka ya kutembea na
fedha nyingi mifukoni.
Akifungua mkutano huo Mkuu wa Mkoa
Kusini Unguja Dkt. Idrissa Muslih Hijja amelipongeza Shirika la
Biashara la Taifa Zanzibar kwa kuwa karibu na Wakulima wa zao hilo.
Amevitaka vyombo vya ulinzi na
usalama kuendeleza juhudi za kupambana na baadhi ya watu wanaoendelea
kusafirisha zao hilo kwa njia ya magendo licha ya kuwa vitendo hivyo
vimepungua kwa sasa.
Afisa kutoka Wizara ya Kilimo na
Maliasili Badru Mwemvura amesema Wizara inaendelea kuchukua jitihada za
kuimarisha zao la Karafuu kwa kuatika miche na kutoa bure kwa Wakulima.
Alisema lengo lilikuwa ni kuotesha
miche 500, 000 kwa mwaka Unguja na Pemba ili kufufua zao la Karafuu
kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 2000 kutokana na kushuka uzalishaji wa
zao hilo.
Hata hivyo amesema kuanzia mwaka
2012 hadi mwaka uliopita lengo hilo liliongezeka na kufikia 1,000,000
baada ya Wizara kushajiisha jamii kuotesha miche ya mikarafuu kupitia
skuli za wakulima.
Ameongeza kuwa miche ya mikarafuu
inagawiwa bure kwa Wakulima kupitia kwa masheha, maafisa Kilimo na
misitu wa Wilaya na kila mkulima hupatiwa miche 35 hadi 40 na Wizara
imekuwa ikifuatilia kwa karibu maendeleo ya uotaji wake.
Mwemvura amesema pamoja na juhudi
hizo bado zipo changamoto nyingi ikiwemo mahitaji ya miche kuwa kubwa
kuliko uwezo wa kuotesha, huduma dhaifu kwa mikarafuu michanga na baadhi
ya wakulima kutaka miche mingi kuliko uwezo wa kuipanda na kuihudumia.
Wakitoa michango yao baadhi ya
Wakulima wamelalamikia ugawaji mbaya wa miche ya mikarafuu unaofanywa na
Maafisa wa Kilimo kwa kutoa miche yenye ubora kwa wakubwa na wengine
kupewa miche dhaifu ambayo mingi ya miche hiyo inakufa.
Aidha Wakulima hao wamesisiza juu
ya usimamizi wa Sheria ili ziweze kusaidi kulinda ubora wa zao hilo la
Karafuu na kutomuonea muhali mtu yoyote.
Post a Comment