MAKAMU WA KWANZA RAIS WA ZANZIBAR, MAALIM SEIF SHARIFF AFANYA ZIARA SOKONI MJINI UNGUJA
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Seif Shariff Hamad, akiulizia bei samaki aina ya vibua katika soko la mombasa ambapo fungu moja huuzwa kati ya shilingi elfu tano. |
Na: Hassan Hamad, OMKR.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema upungufu wa bidhaa katika masoko mbali mbali ya Zanzibar, umechangia kupanda kwa bei za bidhaa hizo.
Amesema tofauti na Ramadhani iliyopita, Ramadhani hii kumejitokeza upungufu wa bidhaa zinazotumika zaidi kwa futari zikiwemo ndizi, viazi vikuu na majimbi, hali iliyochangia bei ya bidhaa hizo kuwa juu ikilinganishwa na kipato cha wananchi.
Maalim Seif ameeleza hayo leo katika ziara yake ya kutembelea masoko mbali mbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi, kuangalia hali ya upatikanaji wa bidhaa za matunda na nafaka ambazo hutumika zaidi katika mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa ajili ya futari.
Masoko aliyoyatembelea ni pamoja na soko la matunda Mombasa, Mwanakwerekwe, eneo la biashara Saateni, Soko la samaki Malindi na Darajani.
Amesema upungufu huo wa bidhaa unaweza kuchangiwa na sababu mbali mbali zikiwemo kiangazi cha muda mrefu, pamoja na mafuriko yaliyotokea Tanzania Bara ambapo bidhaa kutoka mikoani zinachelewa kufika katika masoko ya Dar es Salaam na Zanzibar.
Hata hivyo ameelezea matumaini yake kuwa bei ya bidhaa hizo zinaweza kushuka na kuwanufaisha wananchi, iwapo zitapatikana kwa wingi katika masoko.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa samaki amesema pia bei ziko juu ikilinganishwa na kipato cha wananchi, na kutoa wito kwa wafanyabiashara wa samaki kuzingatia hali hiyo.
Katika eneo la biashara Saateni, Maalim Seif amesema bado eneo hilo linakabiliwa na upungufu wa wateja licha ya baadhi ya wafanyabiashara kuitikia wito wa kuendelea kufanya biashara katika eneo hilo.
Baadhi ya wafabiashara wa eneo hilo la Saateni wamesema miundombinu ya eneo hilo hairidhishi, na hivyo wateja wengi kushindwa kufika kununua bidhaa zao.
Wamezitaja kasoro kubwa zinazochangia hali hiyo kuwa ni kutokuwepo kituo cha daladala katika eneo hilo, na kwamba wateja wao hupata usumbufu wanapotaka kwenda eneo hilo.
Hivyo, wameliomba baraza la manispaa kuimarisha miundombinu hiyo ili kuliweka eneo hilo katika mazingira mazuri ya kibiashara.
Mapema Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Zanzibar Abeid Juma Ali, amekiri kuwepo kwa kasoro hizo lakini amesema tatizo la kufika kwa gari za abiria linatokana na madereva, kwani baraza hilo tayari limeshaweka utaratibu wa kuwepo kwa kituo hicho.
Post a Comment