STARTIMES KUANZA KUONESHA MICHUANO YA KOMBE LA DUNIA U20
WAPENZI wa soka nchini sasa watafaidi kwa kutazama michuano ya kombe la dunia chini ya miaka 20 mwaka 2015 moja wa moja kwenye luninga zao kupitia ving’amuzi vya StarTimes pekee.
Michuano hiyo ambayo itaanza kutimua vumbi tarehe 30 mwezi Mei na kumalizikatarehe 20 mwezi Juni mwaka huu moja kwa moja kutoka nchini New Zealand ambapo timu 24 za vijana kutoka mataifa mbalimbali duniani yatachuana kuwania ubingwa.
Akizungumza baada ya kupata haki miliki kutoka kwa FIFA za kutangaza michuano hiyo maarufu duniani ambayo hubeba mastaa wa baadae kwa timu zao za taifa, Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif amesema kuwa wanafuraha kubwa kuonyesha michuano hiyo kwani soka ni mchezo unaopendwa zaidi duniani.
“Tunayofuraha kubwa kuwatangazia wateja wetu kuwa tumepata haki miliki kutoka FIFA za kuonyesha michuano ya kombe la dunia kwa vijana wa umri chini ya miaka 20 mwaka 2015 itakayofanyika nchini New Zealand. Soka ni mchezo unaopendwa zaidi nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla na tunaamini tutawapatia wateja wetu burudani ya matangazo yenye ubora wa hali ya juu kupitia ving’amuzi vya StarTimes.” Alisema Bi. Hanif
“Itakuwa ni mara ya kwanza kwa nchi ya New Zealand kuwa wenyeji wa michuano hii ambayo inalenga kuyakusanya mataifa pamoja na kukuza umoja na amani. Wapenzi wa soka wataweza kujionea mechi 52 kutoka kwa timu 24 tofauti. Mchezo wa kwanza utapigwa tarehe 30 Mei ambapo utamkutanisha mwenyeji New Zealand na Ukraine, mechi itakayoonyeshwa moja kwa moja katika chaneli ya StarTimes Sports 2 inayopatikana katika ving’amuzi vyote vya dishi na antenna.” Aliongezea
“Ninachoweza kusema mwaka huu kwetu StarTimes ni wa bahati kubwa sana kwani tumeweza kufanya maboresho makubwa katika vipindi vyetu hususani vya michezo. Mbali na michuano hii pia kuna mingine mingi inakuja kwenye king’amuzi hiki hivyo wapendwa wateja wetu wakae mkao wa kula,” alisema Bi. Hanif na kumalizia, “Hivyo nawaomba wateja wetu walipie na wale wasiojiunga wafanye hivyo sasa ili wasipitwe na uhondo huu.”
Katika michuano hiyo bara la Afrika linawakilishwa na timu za vijana wa chini ya miaka ishirini kutoka nchi za Senegali, Mali, Ghana na Nigeria. Huku barani ulaya ni Ureno, Ujerumani, Austria, Ukraine, Hungary na Serbia; kwa bara la Amerika ni Marekani, Mexico, Honduras, Panama, Colombia, Brazil, Ajentina na Urugwai; bara la Asia ni Qatar, Myanmar, Uzibekistani na Korea ya Kaskazini; na pia visiwa vya Fiji na New Zealand ambao ni wenyeji wa michuano hiyo kwa mara ya kwanza.
Post a Comment