Header Ads

Vijana Wahimizwa Kujishughulisha ili Kuleta Tija


Tabia ya vijana kutojishughulisha katika miradi mbalimbali yenye tija kumeeelezwa kuwa moja ya vyanzo vya kudorora kwa uchumi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mh. Jenista Mhagama katika ufunguzi wa kongamano la kitaifa la vijana lililofanyika katika ukumbi wa shule ya msingi Allience Mjini Bariadi.

Alisema kumeanza kujitokeza hali ambapo vijana nchini kutokupenda kujishughulisha katika miradi mbalimbali ya kiuchumi na hivyo kushindwa kuondokana na umaskini na pia kuchangia katika pato la taifa.

Alisema kuwa vijana wanaongoza kwa idadi kubwa lakini wanashindwa kujishughulisha kuhakikisha wanapata maendeleo ambayo yanaweza kulisaidia taifa.



Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dk.Tausi Kida (kushoto) akisalimiana na mgeni rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mh. Jenista Mhagama (kulia) alipowasili katika ukumbi wa shule ya msingi Allience mjini Bariadi kufungua kongamano la vijana.

Mhagama alisema katika Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na Mkoa wa Simiyu, kuratibiwa na Taasisi ya utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), kwamba kuna fursa nyingi lakini vijana wanakuwa wagumu kuzichangamkia na matokeo yake kubaki wakiilalamika serikali kuwa haiwajali.

Alibainisha kuwa serikali itaendelea kusaidia makundi ya vijana yanaoonesha nia ya kujiendeleza

Aidha alifafanua kuwa itawaongezea mtaji wa shilingi milioni 30 kwa kikundi cha vijana cwalioanzisha kiwanda Maziwa cha Meatu pamoja na kile cha Chaki kutokana na jitihada zao walizofanya na matunda kuonekana.

Awali kabla ya kumkaribisha mgeni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema lengo la serikali mkoani hapa ni kuhakikisha linainua pato la mkoa na kuchangia katika pato la taifa kwa kuwawezesha vijana wake kutengeneza bidhaa zinazotokana na malighafi zinazozalishwa mkoani hapa.



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mh. Jenista Mhagama na Naibu wake Mh. Anthony Mavunde wakisalimiana na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Simiyu na ESRF mara baada ya kuwasili kwenye kongamano la kitaifa la vijana lililofanyika jana katika ukumbi wa shule ya msingi Allience mjini Bariadi.

Alisema zaidi kwamba wanalengo la kuhakikisha mkoa unaingia katika tano bora ya uchangiaji wa pato la taifa.

Amehimiza viongozi kuwasaidia vijana kuwaongoza, kuwaelekeza na amewataka vijana kuwa na uthubutu na kuungana kwa pamoja.

Pamoja na harakati za kiuchumi vijana wametakiwa kuwa na mwendo wenye maadili mema ili kuendelea kuwa na afya bora na kukwepa magonjwa yanatokanayo na ukosefu wa maadili.

Amesistiza kuwa kauli mbiu waliyoanzisha ya “Bidhaa moja,wilaya moja” itumike ipasavyo ili kufanikisha maendeleo yao na ya wilaya.



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mh. Jenista Mhagama akitoa hotuba ya ufunguzi wa kongamano la vijana Simiyu lililofanyika jana katika ukumbi wa shule ya msingi Allience mjini Bariadi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dk.Tausi Kida alisema ushiriki wa vijana katika viwanda vidogovidogo kunaweza kukuza uchumi kutokana na viwanda hivyo kutoa ajira na pia kutengeneza mnyororo wa thamani katika mazao ya wakulima ambako vijana ndiko wanakotarajiwa kuonesha ushujaa wao.

Hata hivyo alisema ukuaji wa uchumi kwa sasa bado ni changamoto kwa wananchi wanaoishi vijijini kutokana na baadhi ya huduma kutowafikia kwani asilimia 7 inayopanda kiuchumi huwa haitafsiriki kufikia makundi yote ya kijamii .

“Tumekuwa tukiendesha tafiti nyingi lakini tunaona kipato chetu kinaendelea kushuka hasa katika wananchi wanaoishi vijijini hivyo kuwepo kwa viwanda kutaweza kuwainua kiuchumi wananchi kutokana na bidhaa zao ghafi kuuzwa katika viwanda”Alisema Dk. Kida.

Nao wafadhili wa Kongamano hilo UNDP wamesema wametenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia vijana katika programu zao za maendeleo.



Sehemu ya wageni waalikwa wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi Waziri Mhagama.



Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka akizungumza machache awali kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mh. Jenista Mhagama kufungua kongamano la kitaifa la vijana lililofanyika jana katika ukumbi wa shule ya msingi Allience mjini Bariadi.



Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Moudline Castico akitoa salamu kwa vijana kutoka visiwani Zanzibari kwenye kongamano la vijana Simiyu, lililofanyika jana katika ukumbi wa shule ya msingi Allience mjini Bariadi.

No comments

Powered by Blogger.