Waziri wa Habari NAPE NNAUYE azipa Kongole Kurugenzi za Ikulu na Habari Maelezo
Na Mwandishi Wetu-Dodoma
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Nnauye amezipongeza Kurugenzi za Mawasiliano Ikulu na Idara ya Habari MAELEZO kwa ubunifu wanaouonesha katika kuelezezea mafanikio ya Serikali kwa kutumia teknolojia mbalimbali za habari na mawasiliano.
Waziri Nape alisema licha ya changamoto ya vifaa vinavyowakabili Maafisa Mawasiliano wa Serikali wamekuwa wanafanya kazi nzuri za kuisaidia Sarikali ,amewataka kuwa wabunifu kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano hasa mitandao ya kijamii katika kutekeleza majukumu yao kwani ni nafuu na rahisi.
“Nawapongeza wakurugenzi vijana Dkt. Hassan Abbasi wa MAELEZO na Grayson Msigwa wa Ikulu, hawa ni mfano wa ubunifu wa namna Serikali inavyoweza kutumia teknolojia mbalimbali za mawasiliano katika kuhakikisha mazuri yanayofanywa na Serikali yanatangazwa, yanaenezwa na kutetewa”alisema Waziri Nape.
Waziri Nape aliongeza kuwa pamoja na ubunifu wao katika mitandao ya kijamii, utayarishaji wa makala za Serikali na kujibu hoja kwa haraka kupitia taarifa kwa umma, wameweza pia kubuni vipindi vya TUNATEKELEZA na SAFARI YA DODOMA ikiwa ni mkakati wa kusukuma mbele ajenda za Serikali.
Aidha, Waziri Nape amewataka Maafisa Mawasiliano kutumia fursa zinazotolewa na baadhi ya vyombo vya habari binafsi kupitia vipindi vya bure kwenye Televisheni, redio na magazeti kuhakikisha mambo mazuri yanayotekelezwa na Serikali yanatangazwa na kuweza kusikika kwa Wananchi.
“Nimezungumzia hoja na haja ya mabadiliko kiutendaji, lakini nikiwa kiongozi ambaye pia katika maisha yangu nimefanya kazi ya kuongoza kitengo cha habari na uenezi nafahamu changamoto zinazoikabili kada hii,lakini unaweza ukageuza changamoto kuwa fursa,kwahiyo tujiongeze ndugu zangu ” alisema Waziri Nape.
Waziri Nape alitoa wito kwa Makatibu Wakuu, Wakurugenzi,Wakuu wa Taasisi pamoja na watendaji wakuu katika ofisi za umma kuhakikisha wanatenga fedha katika bajeti kwaajili ya kununua vifaa vya kutendea kazi ili kuviwezesha vitengo vya Mawasiliano Serikalini kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha na ufanisi katika kuisemea Serikali.
Post a Comment