Dawasa yachangia Kuongezeka kwa Maji; yajipanga Kujenga Mitambo ya Majitaka
Na Benedict Liwenga-WHUSM
Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka
Dar es Salaam (DAWASA) imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha kuwa
upatikanaji wa maji safi na salama nchini unaongezeka.
Akiongea leo na Baadhi ya Viongozi
na Watendaji wa Mashirika ya DAWASA na DAWASCO pamoja Waandishi wa Habari Jijini
Dar es Salaam katika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani
ambayo huadhimisha kila mwaka kuanzia siku ya tarehe 16 hadi 22 Machi, Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda amesema kwamba, katika kuadhimisha
Wiki hiyo ya Maji, Mkoa wa Dar es Salaam umelenga kuwahamasisha na kuwaelimisha
Wananchi, Viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na Kamati za Maji kuhusu namna
bora ya usimamizi wa shughuli za maji katika maeneo yao ikiwemo na tarataibu za
umiliki wa visima.
Amesema kwamba, lengo la maadhimisho
hayo ni kuongeza upatikanaji wa maji, uzalishaji na usambazaji wa maji safi na
salama ambayo yatatumika kwa uangalifu ili kupunguza kiwango cha matumizi yake.
Ameongeza kuwa, hali ilivyo sasa,
kiwango kikubwa cha Majitaka kutoka viwandani na majumbani kinaachwa kutiririka
bila kutibiwa na kurudishwa kutumika tena ambapo jambo hilo husababisha
virutubisho vingi vilivyomo katika maji hayo kupotea.
“Katika kuhakikisha maendeleo
endelevu na mzunguko wa uchumi, Majitaka ni rasilimali muhimu na hivyo
kuyasindika, kuyasafisha kwa kuyatibu na kuyatumia tena ni jambo la lazima”,
Alisema Makonda.
Aidha, ameongeza kuwa, katika
maadhimisho ya Wiki ya Maji, shughuli za usafi na upandaji miti katika maeneo
ya vyanzo vya maji zitafanyika, miradi mitatu ya maji katika maeneo ya Mbagala
pamoja na Pugu itazinduliwa na pia miradi 20 ya Jamii itakabidhiwa rasmi
DAWASCO.
Amefafanua kuwa, huduma ya maji kwa
wakazi wa Dar es Salaam hutolewa na DAWASA ambayo imekodisha shughuli za
uendeshaji huduma kwa Shirika la Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO)
ambapo vyanzo vikuu vya maji ni Mto Ruvu, Mto Kizinga pamoja na maji chini ya
ardhi.
Mhe. Makondaa ameongeza
kuwa, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa Wakazi wa Dar es Salaam ni
asilimia 75 ambapo uzalishaji wa maji hayo kwa sasa ni lita Milioni 390 kwa
siku wakati mahitaji ya maji hayo kwa sasa ni ni lita Milioni 510 kwa siku.
Kuhusu Huduma ya
Majitaka, Mhe. Makonda amesema kwamba, mfumo uliopo sasa unahudumia asilimia 10
tu ya wakazi wote wa Jiji, lakini kuna mitambo mitatu ambayo inatarajiwa
kujengwa katika maeneo ya Jangwani, Kurasini pamoja na Kunduchi na mifumo
mingine 50 midogo itajengwa katika maeneo ambayo yanakumbwa na kipindupindu
mara kwa mara.
Makonda ameeleza pia
kuhusu miradi ya visima vya dharura katika maeneo yasiyo na maji ya bomba
ambapo amesema kwamba, DAWASA ina idadi ya visima 147, Manispaa 789 na Taasisi
na Watu binafsi visima 600.
Kuhusu mafanikio
katika sekta hiyo, amesema kwamba, moja ya mafanikio yaliyopatikana katika
utoaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira kwa Mkoa wa Dar es Salaam
toka mwaka jana hadi mwezi Machi mwaka huu ni pamoja na kukamilika kwa Mradi
Mkubwa wa Ruvu Chini ambao umeongeza upatikanaji wa maji toka lita Milioni 182
kwa siku hadi kufikia lita Milioni 270 kwa siku, pia Mradi Mkubwa wa Ruvu Juu
ambao utaongeza upatikanaji wa maji kutoka lita Milioni 82 kwa siku hadi
kufikia lta Milioni 196 kwa siku ambapo mradi huu unatarajiwa kukamilika
mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu baada ya kukamilika kwa kazi ya kuunganisha
umeme mkubwa kutoka Chalinze.
“Elimu juu ya maji
zitolewazo na Serikali kupitia DAWASA na DAWASCO itatolewa, hivyo DAWASCO
wameandaa Madawati maalum kwa wananchi wote katika maeneo yote ya huduma na
yatakuwa wazi wiki nzima kuanzia leo tarehe 16 hadi 22 Machi, 2017 kuanzia saa
2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni kila siku”, alisema Makonda.
Kwa upande wake Kaimu
Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika
la Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) Bw. Kiula Kingu amesema
kwamba, DAWASCO pamoja na DAWASA wamefanikiwa kuzuia upotevu wa maji kwa kiasi
kikubwa ambapo kwa mwaka jana ulikuwa ni
asilimia 47 na mwaka huu umepungua na kufikia asilimia 38.6.
Ameongeza kuwa, wao kama taasisi wamekuwa wakijitahidi
kuhakikisha kuwa wanaendelea kupunguza upotevu wa maji kwa kubadilisha
miundombinu chakavu ya maji na kuweka miundombinu mipya, pia ubadilishaji wa
mita zilizozidi umri wa miaka mitano umeendelea kufanyika hali ambayo imesaidia
watu wengi kupata maji.
Naye Meneja Mahusiano ya Jamii Mamlaka ya Maji Safi na Maji
Taka Dar es Salaam (DAWASA) Bi. Neli Msuya ameeleza kwamba, maeneo yote ya Dar
es Salaam yasiyo na mtandao wa maji yamekuwa yakitengenezewa ramani (design)
ili yawekewe mitandao hiyo ya maji ili maji yaweze kupatikana kwa wakazi wa
maeneo hayo.
Wiki ya Maji huadhimishwa Duniani kote kuanzia tarehe 16-22
ya mwezi Machi ambapo Kaulimbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni “Majisafi na Majitaka-Punguza Uchafuzi
yatumike kwa Ufanisi (Water and Waste Water-Reduce and Reuse).
Post a Comment