Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
(katikati), akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi wa Usambazaji Umeme
vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III) katika mkoa wa Pwani. Wengine katika picha
ni Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo (wa kwanza kushoto), Mbunge
wa Chalinze, Mhe. Ridhiwani Kikwete (wa pili kushoto), Mbunge wa Kibaha
Vijijini, Mhe.Hamoud Jumaa (wa nne kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-hanga.
...............................................
Na Teresia Mhagama
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo, amezindua mradi wa Usambazaji Umeme
vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III) katika mkoa wa Pwani ambao utawezesha
vijiji mbalimbali katika mkoa huo kupata huduma ya Umeme.
Hafla ya Uzinduzi huo ilifanyika katika kijiji cha
Msufini mkoani humo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa mkoa
wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, Mbunge wa Chalinze, Mhe. Ridhiwani Kikwete
na Mbunge wa Kibaha Vijijini, Mhe.Hamoud Jumaa.
Uzinduzi wa mradi huo ulienda sambamba na utambulishaji wa
Mkandarasi atakayetekeleza sehemu ya kwanza ya Mradi huo ambaye ni kampuni ya Steg International Services.
Kabla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-hanga alieleza kuwa Mradi wa
Usambazaji Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu unahusisha vipengele Mradi vitatu
vya utekelezaji.
Alisema kuwa kipengele cha kwanza cha utekelezaji kitahusisha kufikisha umeme kwenye vijiji
ambavyo havijafikiwa kabisa na miundombinu ya umeme wa gridi na kipengele cha
Pili kitahusika na kuongeza wigo wa usambazaji umeme kwenye vijiji ambavyo
vimefikiwa na miundombinu ya umeme.
“Kipengele cha Tatu katika Mradi huu kitahusika na
usambazaji wa nishati jadidifu kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi, ambayo ni
vigumu kufikiwa na umeme wa gridi yakiwemo maeneo ya Visiwa”, aliongeza Mhandisi
Nyamo-hanga.
Alisema kuwa Utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini
Awamu ya Tatu katika Mkoa wa Pwani utahusisha vipengele vyote vitatu na
utatekelezwa kwa vipindi viwili tofauti ambapo sehemu ya kwanza itahusisha
upelekaji umeme katika vijiji 204 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 30.2 ambapo
utekelezaji wa sehemu ya kwanza umeanza Mwezi Februari 2017 na unatarajiwa
kukamilika Machi 2019.
Mhandisi Nyamo-hanga alitoa wito kwa wananchi
watakaounganishiwa umeme kukamilisha utandazaji wa nyaya katika nyumba zao
mapema ili wakati mkandarasi atakapofika katika maeneo yao, wawe tayari kulipia
na kuunganishiwa umeme.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Muhongo, alisema kuwa utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini imefanyika kwa
ufanisi kwani katika mwaka 2007 ni asilimia 2.5 tu ya watanzania waishio vijijini
walikuwa na umeme lakini mpaka mwisho wa mwaka 2016, upatikanji wa umeme
vijijini ulifikia asilimia 49.5.
Alisema kuwa, Watanzania wana haki ya kujivunia miradi
hiyo inayofadhiliwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kutekelezwa na
TANESCO, kwani ni ya kipekee duniani kutokana faida zake kwa wananchi wa
vijijini ambapo gharama mbalimbali
zinabebwa na Serikali huku mwananchi akitakiwa kulipia shilingi elfu 27,000 ili
aunganishiwe umeme.
Alisema kuwa, kwa kutambua umuhimu wa miradi hiyo, bajeti
iliyotengwa kwa mwaka wa Fedha 2016/17 ili
kusambaza umeme vijijini ni zaidi ya shilingi Trilioni moja.
Kuhusu hali ya Umeme katika mkoa wa Pwani, aliwaagiza watendaji wa TANESCO na wataalam
kutoka Ofisi ya Mkuu wa mkoa huo, kujadiliana ili kufahamu mahitaji halisi ya
umeme, hasa ikizingatiwa kuwa kuna viwanda vinavyoendelea kujengwa na vilivyopo
ambavyo vinahitaji si chini ya megawati 60.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kutodai fidia katika
miradi ya Umeme, kutokana na umuhimu
wake katika huduma za kijamii kama vituo vya Afya, Shule, majumbani na shughuli
za kiuchumi ili kuleta mapinduzi katika maisha ya wananchi hao.
Wabunge pamoja na Mkuu wa mkoa wa Pwani, walipongeza
juhudi za usambazaji umeme nchini zinazofanywa na Wizara ya Nishati na Madini,
chini ya Profesa Muhongo na kutumia fursa hiyo kueleza changamoto mbalimbali
zinazopaswa kushughulikiwa na Serikali ili wananchi pamoja na viwanda viweze
kupata umeme wa uhakika.
|
Post a Comment