Vitendo vya Ukatili wa Kijinsia Soko la Mchikichini na Kisutu Jijini Dar es Salaam Vyapungua
Mwenyekiti wa Soko la Ilala Mchikichini, Jumanne Kongogo, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu kupungua vitendo vya ukatili wa kijinsia katika soko hilo baada ya kufanyika kampeni mbalimbali za kupinga ukatili huo zilizofanywa na Shirika la Equality for Growth (EfG) kwa kipindi cha miaka mitatu.
............................................
............................................
Na Dotto Mwaibale
Shirika la Equality for Growth (EfG) limetajwa kusaidia kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika masoko ya Ilala Mchikichini na Kisutu jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyabiashara, viongozi wa masoko hayo pamoja na wasaidizi wa kisheria Dar es Salaam jana wamesema baada ya shirika hilo kutoa mafunzo na kufanya kampeni mbalimbali za kupinga ukatili huo hali imekuwa tofauti na awali.
"Soko letu la Mchikichini lilikuwa na kesi nyingi za vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kutokana na muingiliano wa watu hasa vijana kutoka katika maeneo yasiyo rasmi waliyokuwa wakifanyia biashara na kuhamia hapa kwetu" alisema Mwenyekiti wa soko hilo Jumanne Kongogo.
Alisema vijana wengi walihamia katika soko hilo wakitokea Manzese, Kariakoo, Mnazi Mmoja, Buguruni na maeneo mengine ya jiji na hata nje ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema baada ya EfG kufanya kampeni za kupinga ukatili huo na watuhumiwa kupigwa faini ya sh. 50,000 vitendo hivyo vimepungua kwa kiasi kikubwa.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wafanyabiashara katika soko hilo, Betty Mtewele alisema mafunzo waliyopata kupitia shirika hilo yamewafanya wanawake kujiamini na kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
Mwezeshaji wa kisheria katika soko hilo Charles Beatus alisema matokeo ya kazi wanayoifanya ni makubwa mno baada ya kupata mafunzo kwa kuwezeshwa na shirika hilo.
Alisema kupitia kamati walioiunda wamefanikiwa kupunguza vitendo hivyo kwa asilimia kubwa kwani kupitia kamati hizo mtu akibainika kufanya udhalilishaji wowote amekuwa akiitwa mbele ya kamati.
Mwenyekiti wa Soko la Kisutu Tamimu Chande alisema katika soko hilo vitendo hivyo havipo na kama vitakuwepo basi vitakuwa vinafanyika kwa usiri bila wao kujua.
Katibu wa Soko hilo, Suitbert Nyawalle alisema mafunzo na kampeni zilizofanya na EfG katika soko hilo zimeonesha mafanikio makubwa.
"Niseme kuwa kampeni zilizofanywa na EfG zimewafanya wafanyabiashara katika soko hilo kujielewa na kujua kumfanyia mtu kitendo cha udhalilishaji pamoja na kumtukana ni kosa kisheria" alisema Nyawella.
Nyawella aliongeza kuwa mwaka juzi baada ya EfG kufanya tamasha la kupinga ukati wa kijinsia katika soko hilo kunamfanyabiashara mmoja alitenda kosa la udhalilishaji na alipopelekewa wito wa kuitwa alitoroka na mpaka leo hii hajarudi katika soko hilo kwa kuogopa asidakwe na mkono wa sheria.
Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa shirika hilo Shabani alisema shirika lao limekuwa likifanya kampeni ya kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mwanza na Tanga na kwa Dar es Salaam wameendesha kampeni katika masoko ya Ilala Mchikichini, Temeke Sterio, Gezaulole, Ferry, Kisutu na Tabata Muslim.
Alisema kampeni yao ya kwanza ilikuwa ni Mpe Riziki na Si matusi na imesaidia sana wafanyabiashara kujielewa na kutambua suala zima la unyanyasaji wa kijinsia.
Mwenyekiti wa Soko la Kisutu, Taminu Chande, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu kupungua vitendo vya ukatili katika soko hilo. Kushoto ni Katibu wa soko hilo, Suitbert Nyawalla.
Mfanyabiashara wa soko la Ilala Mchikichini, Denis Ngaiza (kulia), akizungumza katika mkutano huo. Wengine ni wafanyabiashara wa soko hilo. Kutoka kushoto ni Yasin Kiluwa, Tatu Shehe na Samilla Kirundwa.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wafanyabiashara katika Soko la Ilala Mchikichini, Betty Mtewele (kulia), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu kupungua kwa vitendo vya ukati wa kijinsia katika soko hilo baada ya Shirika la Equality for Growth (EfG) kutoa elimu ya kupinga ukatili huo. Wengine ni wafanyabiashara wa soko hilo.
Mwezeshaji wa kisheria katika soko la Ilala Mchikichini, Charles Beatus (katikati), akizungumza. Kulia ni Mwezeshaji wa kisheria, Eva Kakobe na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wafanyabiashara katika Soko la Ilala Mchikichini, Betty Mtewele.
Mwezeshaji wa kisheria, Domitila Ngwada (kulia), akichangia jambo.
Mfanyabiashara wa Soko la Kisutu, Abdallah Mkumba (kulia), akichangia jambo. Kutoka kushoto ni Juma Khalid na Jumanne Ally.
Mfanyabiashara wa Soko la Kisutu, Rose Bruno, akizungumzia kupungua kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika soko hilo.
Post a Comment