Kamishna wa Bima, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima
Tanzania Bw. Baghayo Abdallah Saqware akiongea na waandishi wa habari kuhusu
mwelekeo wa sekta ya Bima nchini na mikakati ya kuendeleza na kupanua shughuli
za bima nchini, leo Jijini Dar es salaam, Kushoto ni Meneja Mawasiliano wa
mamlaka hiyo Bw. Eliezer Rweikiza.
......................................................
Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imejizatiti kurudisha thamani ya huduma za bima kwa kubadilisha baadhi ya sheria na kanuni za bima pamoja na kutengeneza mfumo wenye kutoa tija kwa Wananchi, Serikali pamoja na Kampuni za Bima nchini.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Bima, Baghayo Saqware alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya namna mamlaka hiyo ilivyojipanga kurudisha thamani ya bima kwa wananchi na makampuni ya bima hapa nchini, leo Jijini Dar es Salaam.
Baghayo Saqware amesema kwamba moja ya kanuni na sheria zitakazoboreshwa ni pamoja na kupeleka biashara ya bima (Insurance business – risks) nje ya nchi badala ya kutumia makampuni ya ndani.
“Tutaweka kanuni itakayolazimisha Kampuni za bima hapa nchini kuongeza mitaji au kutengeneza mfuko wa pamoja au mfumo wa makampuni kushirikina kimtaji ili kuweza kuandikisha na kubakisha sehemu kubwa au biashara yote ya bima nchini,” alifafanua Saqware.
Aliendelea kwa kusema kuwa utawekwa utaratibu wa kisheria utakaohakikisha waingizaji wa mizigo kutoka nje ya nchi wanakatia bima za mizigo yao kupitia kampuni za bima nchini.
Aidha amesema kwamba ikibidi mamlaka hiyo itabadilisha sheria ya bima nchini ili wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nje ya nchi (import goods) iwe ni lazima kukatia bima nchini ili kuongeza mapato ya kodi (VAT) pamoja na bima (Premium Levy).
Katika kurudisha thamani ya huduma ya bima kwa wananchi mamlaka hiyo itahakikisha makampuni yanayotoa huduma ya bima yanatoa huduma stahiki kwa wateja wa bima pamoja na kuhakikish malalamiko ya wateja yanayofikishwa katika mamlaka husika yanashughulikiwa kwa wakati.
Aidha, katika kupanua shughuli za bima mamlaka hiyo iko katika hatua za mwisho za kukamilisha bima ya kilimo, mifugo pamoja na bima za watu wenye kipato cha chini (Micro-insurance) pamoja na kukamilisha utekelezaji wa sera ya Taifa ya Bima.
Vile vile inapanua matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) kwa kutumia utaratibu wa kusajili na kutoa leseni za biashara ndani ya siku saba hadi thelathini, aidha mfumo huo utaondoa tatizo la bima bandia za vyombo vya moto pamoja na kuhakiki uhalali wa stika za bima kwa walionazo.
Nae, Meneja Tehama TIRA, Aron Mlaki amesema kwamba mfumo huo wa Tehama utamuwezesha mwananchi kupata maelezo ya bima yake kupitia intanenti na meseji za kawaida ambapo kwa upande wa message za kawaida ataandika neno ‘STIKA’ likifuatiwa na namba ya Stika na kuituma kwenye namba 15200 baada ya hapo atapokea taarifa za bima yake.
|
Post a Comment