Kilele cha Siku ya Kifua Kikuu Chafanyika Mererani, MANYARA
Picha ya pamoja katika maadhimisho ya kifua kikuu - Mererani.
.............................
Shirika lisilo la kiserikali la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojishughulisha na mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI limeungana na wadau wote duniani katika maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani, 24 March 2017.
Maadhimisho hayo yalifanyika katika mji mdogo wa Mererani, wilaya ya Simanjiro katika Mkoa wa Manyara, eneo ambalo Shirika la AGPAHI linatekeleza mradi wa kutoa huduma shirikishi za kifua kikuu na UKIMWI sehemu za migodini kwa hisani ya shirika la ADPP la Msumbiji.
Katika maadhimisho hayo, shirika la AGPAHI kwa kushirikiana na timu ya afya ya wilaya walifanya zoezi la kutoa huduma mbalimbali kwa jamiii inayozonguka mji mdogo wa Marerani kuanzia tarehe 23 – 25 Machi, 2017.
Huduma zilizotolewa ni uchunguzi wa kifua kikuu, kupima Virusi vya Ukimwi na kutoa elimu kwa umma kuhusu kifua kikuu na VVU/UKIMWI.
Zoezi hilo lilisimamiwa na afisa mradi wa kifua kikuu na UKIMWI, kutoka AGPAHI, mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Simanjiro, wataalamu wa maabara, watoa huduma wa Afya kutoka kituo cha Afya Mererani na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani ni; “TUUNGANE PAMOJA KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU”.
Shirika la AGPAHI linafanya kazi katika mikoa sita ambayo ni Mwanza, Geita, Mara, Tanga Shinyanga na Simiyu. Huduma zitolewazo na shirika la AGPAHI ni kusaidia serikali kupitia vituo vya kutolea huduma za afya katika:
1.Kutoa huduma za tiba na matunzo kwa watu
wanaoishi na virusi vya UKIMWI;
2.Kutoa huduma za kuzuia maambukizi ya virusi vya
UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto;
3.Kutoa huduma ya uchunguzi wa dalili za awali na
huduma za awali za saratani ya mlango wa kizazi
na
4.Kutoa huduma shirikishi za kifua kikuu na UKIMWI
sehemu za migodini.
Vilevile, shirika linafanya kazi katika mji mdogo wa mererani katika kutekeleza mradi wa kifua kikuu sehemu za migodini.
Matukio katika picha.
Afisa mradi wa Kifua kikuu na UKIMWI kutoka AGPAHI, Bi Alio Hussein akiwaelimisha na kugawa vipeperushi kwa wakazi wa Mererani kuhusu Kifua kikuu na VVU/UKIMWI.
Mhudumu wa afya ngazi ya jamii akiwaelezea wakazi wa Mererani dalili za Kifua Kikuu na namna ya kuweza kujikinga na maambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii wakichukua maelezo ya baadhi wakazi wa Mererani waliokua tayari kuchunguzwa kama wana maambukizi ya vijidudu vya Kifua Kikuu.
Elimu kwa wachimbaji wa madini ya Tanzanite kuhusu Kifua kikuu na VVU/UKIMWI ikiendelea.
Wachimbaji wa madini ya Tanzanite katika Kitalu D, wakiwa wamekusanyika kwa wingi wakielimishwa kuhusu Kifua kikuu na VVU/UKIMWI.
Na Joshua Fanuel , Kilimanjaro
Post a Comment