Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii yaipongeza TASUBA
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Wafanyakazi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) wakijadiliana wakati wa kikao 17 Machi, 2017. |
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakitoa maoni yao wakati wa kikao cha kujadili na kukagua mradi wa ukarabati wa taasisi hiyo, 17 Machi, 2017. |
Na Benedict Liwenga-WHUSM
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
imeipongeza Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) kwa juhudi zake
inazozifanya katika kuibua na kukuza vipaji vya Vijana nchini.
Pongeza hizo zimetolewa leo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani na
Wajumbe wa Kamati hiyo wakati walipoitembelea taasisi hiyo kwa ajili ya kukagua
mradi wa ukarabati wa taasisi hiyo.
Akiongea wakati wa kikao na Watendaji wa Taasisi hiyo,
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Peter Serukamba amesema kwamba, suala la
muziki, filamu na utamaduni ni suala la kipaji, hivyo halihitaji elimu kubwa kwa
vijana, bali kuwepo na mazingira mazuri yatakayowezesha wenye vipaji na wasio
na vipaji waweze kupata fursa ya kujifunza na kuonyesha vipaji vyao.
Mhe. Serukamba amelishauri Baraza la Mitihani Tanzania
(NECTA) kuweka mazuri ambayo hayatawabana vijana ambao hawakupata fursa ya
elimu lakini wana vipaji, hivyo ameshauri vijana nchini wapewe fursa ya
kujifunza na vipaji vyao viendelee kuibuliwa.
Sambamba na hilo, Mhe. Serukamba ameishauri taasisi hiyo kutoa
elimu ya lugha mbalimbali kama vile lugha za Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa,
Kijerumani, Kichina na nyinginezo ili ziweze kuwasaidia vijana hao wawapo nje
ya nchi na pindi wanapokuwa wameiva katika masomo yao ndani ya chuo hicho.
“Chuo hiki naomba kione namna ya kufundisha lugha pamoja
kwamba mnafundisha muziki, basi vema mkawafundisha vijana wetu lugha mbalimbali
ili waweze kwenda Duniani, kwasababu kama watakuwa na tatizo la lugha itawapa
shida”, alisema Serukamba.
Kuhusu suala la bajeti katika taasisi hiyo, ameshauri kwamba,
Uongozi wa taasisi hiyo haunabudi kujitangaza ili waweze kupata fedha za
kutosha badala ya kulalamika kwamba hawana fedha.
“Lazima Mkuu wa Chuo uende mbali zaidi kwasababu vitu
mnavyofundisha hapa katika taasisi yenu ni vya kipekee, havifundishwi kwingine,
hivyo una fursa kubwa ya kujitangaza na kuweza kupata fedha za kukisaidia chuo
hiki, kwa mfano unaweza kuwatafuta watu toka sekta binafsi ambao hawa wataweza
kukusaidia kama vile makampuni mbalimbali hapa nchini”, aliongeza Serukamba.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo,
Mhe. Nape Nnauye amesema kwamba, moja ya changamoto kubwa ambayo imekuwa
ikiikabili taasisi hiyo ni mmomonyoko wa kingo za mpaka wa taasisi hiyo ambao
umesababishwa na bahari kusogelea eneo la taasisi hiyo hali ambayo inahatarisha
majengo yake, hivyo amefafanua kuwa tayari Wizara iliwasiliana na Ofisi ya
Makamu wa Rais upande wa Mazingira ambao wao tayari walifika na kupima athari
za mmonyoko huo.
Ameongeza kuwa, kwa hivi sasa kinachosubiriwa ni fedha ambazo
zitatumika kuanza ujenzi wa kingo ambayo itasaidia kuepusha mmomonyoko huo unaofanywa
na maji ya bahari.
“Hili eneo la taasisi ya TaSUBA watu wa NEMC walishafika na
kupima na tunategemea katika mwaka ujao wa fedha, fedha itapatikana ili kuanza
ujenzi wa kingo katika eneo hili ili tuweze kuzuia maji ya bahari kuendelea
kuharibu eneo la taasisi hii”, alisema Mhe. Nnauye.
Kuhusu suala la elimu itolewayo katika taasisi hiyo, amesema
kwamba anakubaliana na mapendekezo ya Kamati kwamba, vijana wapewe fursa ya kufundishwa
kwa kuangalia vipaji vyao na isiwe lazima sana kuangalia elimu waliyonayo kwani
wako vijana wengi ambao wana vipaji lakini hawakupata fursa ya kuelimika, lakini
pia na wale walioelimika wanayo nafasi ya kujifunza ndani ya chuo hiko.
Awali akitoa taarifa ya taasisi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi hiyo, Dkt. Helbert Makoye amesema kwamba, taasisi anayoiongoza ni
taasisi iliyotukuka na inafundisha masuala mbalimbali ya Sanaa, inakuza viwango
vya Sanaa, inakuza matumizi ya Sanaa kama vile maonyesho mbalimbali yenye kutoa
elimu kwa jamii.
“Hapa chuoni pia tunafundisha watendaji kwenye masuala ya Sanaa
lakini pia Wasimamizi, tunawandaa Watafiti na Washauri wa Sanaa na utamaduni
kwa ngazi ya Taifa na Kimataifa”, alisema Dkt. Makoye.
Post a Comment