Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kushoto) akipata maelezo kutoka
kwa Mkandarasi wa kampuni ya Sumitomo Mitsui Eng. K Tsuji, anayejenga barabara
ya juu (TAZARA fly over) wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi huo jijini Dar
es salaam.
.............................
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi wa kampuni
ya ujenzi ya Sumitomo Mitsui anayejenga barabara ya juu (Fly over) ya Tazara
kuongeza kasi ya ujenzi huo ili kupunguza
muda wa ujenzi wa mradi huo.
Akizungumza katika
eneo la ujenzi huo leo jijini Dar es salaam, Profesa Mbarawa amepongeza hatua
iliyofikiwa sasa lakini pia amesisitiza kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo
ili wananchi waweze kunufaika.
“Hakikisheni badala ya
kutumia miezi 35 kujenga mradi huu, mnatumia miezi pungufu zaidi ili
kuwawezesha wananchi na wadau wengine kunufaika na fursa za mradi huu”,
amesisitiza Waziri Mbarawa.
Aidha, Amewataka
wafanyakazi wote katika mradi huo kufanya kazi kwa bidii na uaminifu mkubwa kwa
kuwa Serikali ina mpango mwengine wa kujenga Fly over kama hiyo itakayowawezesha
kupata tena fursa ya ajira.
Hatua hiyo itapelekea
kuwezesha wananchi kunufaika na mradi huo mapema, hivyo kupunguza gharama
wanazozipata kutokana na msongamano wa magari uliopo sasa jijini Dar es salaam.
Naye, Balozi wa Japan
nchini Bw. Masaharu Yoshida, amemhakikishia Waziri huyo kuwa ujenzi wa mradi
huo utamalizika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa, hivyo kuondoa
changamoto ya msongamano katika barabara ya Nyerere na Mandela.
|
Post a Comment