Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Eng. Patrick Mfugale akifafanua jambo
wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa ujenzi wa barabara za juu eneo la ubungo
(Interchange) utakaotekelezwa na kampuni M/S China Civil Engeneering
Construction Cooperation kutoka China (CCECC).
................................
Wakala wa Barabara
nchini (TANROADS), leo umetiliana saini na kampuni ya M/S China Civil
Engeneering Construction Cooperation kutoka China (CCECC) mkataba wa ujenzi wa barabara za Juu ‘Interchange’ katika
makutano ya barabara ya Sam Najoma na Mandela Ubungo jijini Dar es salaam.
Mkataba huo unamtaka
Mkandarasi kampuni ya CCECC kutoka China kuanza ujenzi huo mara moja na ujenzi
huo unatarajiwa kutumia takriban miezi 30 hadi kukamilika kwake.
Akizungumza mara baada
ya kusaini mkataba huo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS Eng.
Patrick Mfugale amesema zaidi ya shilingi Bilioni 177.4 zinatarajiwa kutumika
katika ujenzi huo utakaowekewa jiwe la msingi mwezi machi mwaka huu.
“Hakikisheni mnaanza ujenzi
mara moja kwani Serikali imeshakamilisha taratibu zote na tayari kiasi cha
shilingi bilioni 2.1 kimelipwa kwa ajili ya fidia kwa wananchi walioguswa na
mradi huo”. Amesema Eng. Mfugale.
Ujenzi wa Ubungo
interchange unajengwa kwa fedha ya mkopo kutoka Benki ya Dunia ambapo Serikali
kwa upande wake imeshalipa fidia ya zaidi ya shilingi bilioni 2.1.
“Zaidi ya magari
65,000 yanapita kila siku katika katika makutano ya barabara za
morogoro,Mandela na Sam Nujoma eneo la Ubungo hali inayosababisha msongamano
katika barabara ya Morogoro ambayo ndio lango kuu la kuingia jijini Dar es
salaam hivyo ufanisi wa mradi huo
utahuisha hali ya usafirishaji katika jiji la Dar es salaam na kuchochea ukuaji
wa uchumi” amesisitiza Eng. Mfugale.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa kampuni ya CCECC Bw, Jiang Yigao amemhakikishia Eng. Mfugale kuwa wataanza
maandalizi ya ujenzi huo mara moja na watafanya kazi hiyo kwa wakati.
|
Post a Comment