NAPE NNAUYE: Hata kwa Goli la Mkono lazima Tuibuke Washindi Gabon
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema hata kwa goili la mkono ni lazima Serengeti Boys warejee nyumbani wakiwa ama na kombe au wakiwa wamefuzu kushiriki kombe la dunia kwa kuwa moja ya timu mbili zinazohitajika.
Kauli ya Waziri Nape ameitoa leo asubuhi wakati akifungua mashindano ya Kombe la Standard Chartered 2017 safari kuelekea Anfield ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 100 tangu benki hiyo kuanzishwa mwaka 1917 yaliyoanza kutimua vumbi katika viwanja vya JK Park Kidongo Chekundu, Gerezani.
Alisema haiwezekani taifa hili kuwa na Waziri mjanja kama Nape halafu Serengeti Boys inakosa kombe huko Gabon na nafasi ya ushiriki Kombe la dunia.
Pamoja na kauli yake hiyo Waziri Nape aliiomba Benki ya Standard Chartered kushiriki katika jukumu la kuhakikisha kwamba Serengeti Boys ama inarejea na kombe au inafuzu miongoni mwa timu mbili zitakashiriki Kombe la Dunia.
Picha juu na chini ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye (katikati), Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Tanzania Sanjay Rughani (mwenye kofia) na Mwenyekiti wa Kamati ya uamuzi TFF, Salum Chama (wa tatu kulia) wakijumuika kwa pamoja na washiriki wa mashindano ya Kombe la Standard Chartered 2017 (Road to Anfield) kutoka makampuni mbalimbali kupasha misuli moto yaliyoanza kutimua vumbi leo kwenye viwanja vya JK Park Kidongo Chekundu, Gerezani jijini Dar es Salaam.
Alisema kwa sasa serikali inawaomba wadau kushiriki katika kuhakikisha kwamba Kambi ya Serengeti Boys inaimarika na kuwezesha kuwa na kikosi cha ushindi.
Aliishukuru Benki hiyo kwa kuhakikisha kwamba inainua michezo nchini kwa kusaidia kunyanyua na timu ya wanawake na kusema kitendo cha wao kuileta Dunia nchini Tanzania (Liverpool na mashabiki wake na michuano ya kuelekea Anfield) ni cha kushukuriwa sana.
Aliishukuru pia kwa kumleta nguli John Barnes na kulitaka Shirikisho la kabumbu nchini (TFF) kuhakikisha kwamba wanatumia nafasi hiyo kuwaweka sawa pia kisaikolojia vijana wa Serengeti Boys.
Alisema ujio wa Barnes unaneema kubwa hasa ratiba yake ya kukutana na vijana wa Serengeti.
Pamoja na kuzungumzia Serengeti Boys, Waziri Nape aliitaka jamii kuthamini michezo na kushiriki kwa kuwa huleta afya na kujenga umoja.
Alitaka timu zote 32 zinazowania kufuzu kucheza ngwe ya Afrika mashariki kucheza kwa bidii na furaha na kuhakikisha wanapata ushindi halali ili waweze kuiwakilisha vyema Tanzania katika michuano ya Afrika Mashariki jumamosi ijayo.
Washindi wa mwaka jana timu ya Mwananchi ilitolewa mapema katika mashindano hayo ambayo yanaendelea hadi jioni ya leo wakati mshindi atakapopatikana.
Mshindi wa mashindano hayo atapambana na washindi kutoka Kenya na Uganda ambao nao leo wanawasaka washindi wao katika nchi hizo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye (katikati), Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Tanzania Sanjay Rughani (mwenye kofia) na Mwenyekiti wa Kamati ya uamuzi TFF, Salum Chama (kushoto kwa Waziri Nape) katika picha ya pamoja baada ya kukabidhi bendera kwa washiriki kutoka makampuni mbalimbali wa mashindano ya Kombe la Standard Chartered 2017 (Road to Anfield) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 100 tangu benki hiyo kuanzishwa mwaka 1917 yaliyoanza kutimua vumbi leo kwenye viwanja vya JK Park Kidongo Chekundu, Gerezani jijini Dar es Salaam.
Post a Comment