Vita Dhidi ya Uagizaji, Usambazaji na Matumizi ya Madawa ya Kulevya ni Kubwa Nchini
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kwamba vita inayopiganwa sasa dhidi ya uagizaji, uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa ya kulevya ni kubwa na kila Mtanzania anapaswa kuunga mkono jitihada hizo.
Kassim Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Bungeni, Mjini Dodoma katika hotuba yake ya kuahirisha mkutano wa sita wa Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Moja ya eneo lililojadiliwa na kuibua hisia kali ni kuhusu vita inayoendelea nchini dhidi ya dawa za kulevya. Watanzania wote ni mashahidi kwamba vijana wetu wengi wameendelea kudhoofisha afya zao kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya. Dawa za kulevya ni hatari kwa usalama na ustawi wa Taifa,” alifafanua Waziri Mkuu.
Aliendelea kwa kusema kuwa kitaalamu madhara ya kiafya yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya ni pamoja na kuathirika kwa mfumo wa fahamu kwa mtumiaji ikiwemo kuchanganyikiwa, kuwa na ulevi usioponyeka kirahisi na kusababisha vifo ikiwa mtumiaji atazidisha matumizi ya dawa hizo.
Aidha Waziri Mkuu amesema kuwa madhara ya kiuchumi yanayosababishwa na magonjwa hayo ni pamoja na kuwatibu waathirika wa dawa za kulevya, gharama kubwa za uchunguzi wa kimaabara kwenye maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na watumiaji wa dawa za kulevya kushindwa kujisimamia na kuendesha maisha yao.
Amesema kuwa madawa hayo huingia nchini kwa kutumia bandari bubu kupitia Bahari ya Hindi na kwa njia ya magari binafsi kupitia mipaka ya nchi ya Kenya, Uganda na mpaka wa Tunduma.
Kassim Majaliwa amesema kuwa lengo la Serikali ni kuwasaidia walioathirika na dawa hizo na kuwachukulia hatua kali wale waliowaathiri kwa maana ya wauzaji na wasambazaji.
Amewashukuru wabunge kwa kutoa mchango mkubwa na ushauri wa namna nzuri zaidi ya kupambana na janga hilo ikiwa dhamira ya Serikali ni kupambana na janga hilo kwa dhati bila kumuonea mtu yeyote na kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki.
Kassim Majaliwa ametoa takwimu ya Watanzania ambao wamefungwa katika magereza mbalimbali nje ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na Watanzania 200 ambao wamefungwa China, Watanzania 12 nchini brazil, Watanzania 63 nchini Iran, Watanzania 7 nchini Ethiopia na Watanzania 296 ambao wamefungwa Afrika ya Kusini.
Post a Comment