Waziri Profesa MAKAKE MBARAWA aiagiza TAA kuongeza Mapato yake
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ameiagiza Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Tanzania (TAA) kuongeza kiwango cha ukusanyaji mapato kutoka Bilioni 74
hadi kufikia bilioni 105 katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Ametoa agizo hilo
jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka hiyo mara
baada ya kukagua majengo matatu na ofisi mbalimbali zilizopo Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere (JNIA).
Amesisistiza wafanyakazi
wa Uwanja huo kuhakikisha kiasi cha ukusanyaji wa mapato hayo kinaongezeka siku
hadi siku ili kukuza uchumi wa taifa na kuchochea fursa za kimaendeleo.
“Ni lazima muongeze
kasi ya kufanya kazi ili mapato yaongezeke kwa kuwa uwezo mnao na nimeona kwenye
viwanja vyenu kuna sehemu nyingi za biashara, hivyo mna kila sababu ya
kukusanya kiasi hicho cha fedha”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, katika ziara
hiyo Waziri Prof. Mbarawa alibaini ucheleweshwaji wa vibali kwa abiria
wanaoingia katika Uwanja wa Ndege wa JNIA
ambapo abiria huchukua zaidi ya saa moja kupata vibali.
“Nimesikitishwa na
kitendo cha ucheleweshwaji wa vibali kutoka Idara ya Uhamiaji na huduma za
kibenki zinazotolewa… hali hii haileti picha nzuri kwa wageni wetu. Abiria
kuwekwa zaidi ya saa moja akisubiri kupata huduma, sitaki kuona hali hiyo ikiendelea”,
amesisitiza Prof. Mbarawa.
Muonekano wa Jengo la Tatu (Terminal III) la abiria ambapo ujenzi wake unaendelea. |
Sambamba na hilo amezitaka
taasisi zote zinazofanya kazi katika viwanja vya ndege kushirikiana kwa ukaribu
ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kuongeza mapato kwa taifa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa TAA, Eng. George Sambali amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa
mapungufu yaliyobainishwa yatafanyiwa kazi ili kuongeza ufanisi na huduma bora
kwa abiria.
“Kwa kushirikiana na
taasisi zote ambazo zinafanya kazi katika Kiwanja hiki tutahakikisha tunatoa
huduma nzuri na kuongeza ufanisi katika utendaji ili kufikia malengo”, amesema
Eng. Sambali.
Waziri Prof. Mbarawa
amefanya ziara ya siku moja katika Kiwanja cha JNIA ili kuona utendaji kazi na
maendeleo ya Ujenzi wa Jengo la Tatu la abiria ambapo jengo hilo linatarajiwa
kukamilika mwezi Desemba 2017 na litakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya abiria
milioni sita kwa mwaka.
Post a Comment