Watumishi wa Umma Watakiwa Kuwa Chachu ya Mabadiliko katika Kukuza Uchumi
Na.Aron Msigwa - DODOMA
Watumishi wa Umma wametakiwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na maarifa na kuwa tayari kukubali mabadiliko yanayotokea ndani ya Utumishi wa Umma ili kuliwezesha Taifa kufikia malengo yaliyokusudiwa katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa mjini Dodoma na Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu wa mkoa wa Dodoma Bw. Deogratius Nyinza wakati akifunga kikao kazi cha Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vilivyo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mjini Dodoma.
Akizungumza na Wakuu hao amesema kuwa wakati umefika kwa watumishi wote wa umma kutimiza kikamilifu wajibu na majukumu yao ya kila siku katika maeneo yao ya kazi kwa weledi mkubwa ili utendaji wao uweze kupimwa kwa kuwa na matokeo makubwa kwa wananchi
Bw. Nyinza amesema kuwa wao kama viongozi wa Taasisi muhimu za Elimu hapa nchini wanapaswa kuwa chachu ya kuleta mabadiliko nchini kwa kuwa mfano katika kusimamia rasilimali fedha katika mapato na matumizi ili wananchi waweze kupata huduma endelevu zilizokusudiwa.
" Najua mna sehemu kubwa sana katika kusimamia rasilimali hakikisheni mnasimamia vizuri fedha zinazopatikana ili zilete matokeo yaliyokusudiwa ili kuepuka mtego wa kuingia kwenye matumizi mabaya ya fedha za umma,kagueni matumizi yote ili kujiridhisha na mambo yanayotendeka katika maeneo yenu " Amesisitiza Bw.Nyinza.
Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu wa mkoa wa Dodoma Bw. Deogratius Nyinza (kulia) akifunga kikao kazi cha Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vilivyo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mjini Dodoma.Katikati ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw.Erasimus Rugarabamu na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Bw.Enterberth Nyoni (kushoto).
Amewataka wawe tayari kuzuia aina yoyote ya ufujaji wa fedha katika vyuo wanavyovisimamia kwa kuzingatia kanuni na taratibu zinazosimamia matumizi ya fedha huku akisisitiza kuwa Serikali ya awamu ya tano inasimamia matumizi bora ya rasilimali za umma na kupiga vita matumizi mabaya ya fedha.
Ametoa wito kwa wakuu hao kuwa tayari kukubali mabadiliko ya mfumo wa elimu yanayotokea nchini kwa kuweka mikakati itakayowafanya waendane na mabadiliko yanayotokea ikiwemo uboreshaji wa Taasisi za elimu wanazozisimamia, kujiendeleza kielimu na kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa lengo la kuongeza mapato ya taasisi zao.
Bw.Nyinza amewataka Wakuu hao wa vyuo kutekeleza maazimio yaliyotokana na kikao kazi chao ili Taifa liendelee kunufaika na mchango wao maendeleo ya Vyuo vya Maendeleo ya jamii.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli anayeshughulikia Taaluma Bi. Columba Maboko akizungumza kwa niaba ya Washiriki wenzake waliohudhuria kikao kazi cha Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii wakati kufunga kikao hicho mjini Dodoma.
Wakuu wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu wa mkoa wa Dodoma Bw. Deogratius Nyinza (katikati mstari kwanza) na baadhi ya viongozi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Awali akizungumza kabla ya kufungwa kikao kazi hicho, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw.Erasimus Rugarabamu amewashukuru wakuu wa vyuo kwa ushiriki mzuri waliouonyesha wenye lengo la kujenga taasisi imara za utoaji wa elimu Bora ya Maendeleo ya jamii nchini.
Amesema ushiriki wao katika kikao kazi hicho utawawezesha kutekeleza majukumu yao katika viwango vinavyostahili na kuwawezesha kuziongoza taasisi zao kwa weledi kwa kuzingatia Sheria, Sera, Kanuni na taratibu zinazosimamia uendeshaji wa vyuo.
" Kikao kazi chenu kimekuwa kizuri sana, mmekua na ushiriki hai wenye lengo la kuwajengea uwezo na ufanisi wa kazi katika maeneo yenu, ninaomba mtakaporudi katika maeneo yenu ya kazi myazingatie yote" mliyojifunza kuleta maokeo chanya" Amesisitiza.
Amewataka kuzingatia maadili katika utumishi wao kwa kuzingatia kuwa wao ni watumishi wa umma pia kuwa tayari kukabiliana na changamoto ya ukiukwaji wa maadili unaofanywa na baadhi ya watumishi walio chini yao ili kujenga nidhamu kazini.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli anayeshughulikia Taaluma Bi. Columba Maboko akizungumza kwa niaba ya Washiriki wenzake waliohudhuria kikao kazi hicho amesema kuwa wao kama viongozi wa Vyuo hivyo wako tayari kuhakikisha Ubora wa Elimu katika Vyuo vya Maendeleleo ya Jamii nchini unaimarishwa.
"Sisi kama wasimamizi na viongozi tuliopewa dhamana ya kuongoza vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini, Tuko tayari kuyafanyia kazi mafunzo yote tuliyopewa ili vyuo vyetu viendelee kuzalisha wataalam bora wa Maendeleo ya Jamii" Amesema Bi. Columba.
Amefafanua kuwa katika kutekeleza Majukumu yao watahakikisha wanasimamia vyema mapato na matumizi ya fedha za Serikali zinazoelekezwa katika vyuo hivyo ili kuviwezesha vyuo hivyo kutoa huduma kwa jamii.
Post a Comment