Serikali Kujenga Shule za Michezo kwa Kila Mkoa
Na Raymond Mushumbusi
Serikali imeazimia kujenga na kuendeleza shule za michezo zilizopo katika mikoa yote nchini kwa kipindi hiki cha Serikali awamu ya tano.
Azimio hilo limetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia James Wambura wakati akizungumza na timu ya mpira ya miguu ya wasichana ya Fc Vito Malaika katika hafla ya kukabidhi Bendera ya Taifa kwa timu hiyo kwenda kushiriki mashindano ya mpira wa miguu ya Helsinki Cup yatakayofanyika nchini Finland Julai 8 mwaka huu.
“Azima ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuendeleza michezo nchini kwa kuibua vipaji vya michezo na kuviendeleza kuanzia wakiwa shule” Alisema Mhe. Annastazia.
Mhe Annastazia Wambura ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania inashirikia na Serikali ya Finland katika kuendeleza michezo shuleni na zaidi ya shule 462 nchini zitafaidika na miradi ya michezo ya vijana inayofadhiliwa na Serikali ya Finland.
Kwa upande wake Balozi wa Finland nchini Tanzania Pekka Hukka amesema kuwa wamedhamiria kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza michezo nchini hasa kwa vijana ili kujenga timu nzuri za baadae, na kwa sasa wanapeleka timu za vijana kwenda kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa ikwemo Helsinki Cup linalofanyika nchini finland Julai 8 mwaka huu.
Naye Meneja wa Timu ya wasichana ya mpira wa miguu ya Fc Vito Malaika Bakari selemani ameipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuendeleza michezo hasa kwa vijana kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali na ili kuendeleza michezo na kukuza vipaji kwa vijana Serikali na wadau wa michezo wametakiwa kuwekeza kwa vijana ili kujenga timu zenye kuleta ushindani katika mashindano ya kitaifa na kimataifa.
Post a Comment