Ofisi ya Taifa ya Takwimu yatangaza Mfumuko wa Bei wa Mwezi Oktoba 2015
Na Veronica Kazimoto
MFUMUKO wa bei wa Taifa kwa mwezi Oktoba, 2015 umeongezeka hadi kufikia asilimia
6.3 kutoka asilimia 6.1 mwezi Septemba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi wa Sensa
ya Watu na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo amesema kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei kumesababishwa na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma zingine za kijamii ikiwemo
chakula na nishati.
“Kupanda kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Oktoba, 2015 kumechangiwa na ongezeko
la bei za vyakula kama vile Mchele ambao umeongezeka bei kwa asilimia 0.8, unga
wa muhogo umeongezeka hadi asilimia 0.7, nyama kwa asilimia 0.8, samaki kwa
asilimia 5.5, ndizi za kupika asilimia 0.7 na choroko kwa asilimia 0.9”,
amesema Kwesigabo.
Bidhaa zisizokuwa za vyakula kama vile vitambaa kwa ajili ya nguo za kike zimepanda
kwa asilimia 1.6, viatu vya kiume asilimia 1.1, mkaa asilimia 1.4 na gharama za
kupata ushauri kwa daktari pia zimepanda hadi kufikia asilimia 1.4.
Kwa upande Mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 0.1
ambao ni ongezeko sawa na mwezi Septemba, 2015. Fahirisi za bei pia
zimeongezeka kutoka 159.04 hadi kufikia 159.17 kwa mwezi Oktoba, 2015.
“Fahirisi za bei za vyakula vya nyumbani na migahawani iliongezeka kidogo
hadi kufikia asilimia 10.0 kutoka asilimia 9.4 kwa mwezi Septemba, 2015 ambapo bidhaa
zisizokuwa za vyakula zimepungua kidogo kutoka asilimia 1.9 hadi asilimia 1.7
kwa mwezi Oktoba, 2015,” amefafanua Kwesigabo.
Kwesigabo amesema kuwa Mfumuko wa Bei ambao haujumuishi vyakula na nishati
kwa mwezi Oktoba, 2015 umepungua kidogo hadi kufikia asilimia 2.1 kutoka
asilimia 2.2 kwa mwezi Septemba, 2015.
Post a Comment