Waziri Mkuu MIZENGO PINDA, ataka SADC iwabane Wanachama Wake
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) haina mpango wa
kuweka mkakati utakaohakikisha kuwa nchi wanachama zinakuwa na mpango
mahsusi wa kuendeleza viwanda kama ambavyo imekubaliwa kwenye kikao chao
kilichomalizika leo.
Ametoa kauli hiyo leo mchana
(Jumanne, Agosti 18, 2015), wakati akizungumza na waandishi wa Habari
mara baada ya kumaliza mkutano wa 35 wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya
Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika jijini Gaborone,
Botswana.
“Jumuiya ya SADC kupitia
sekretarieti yake itabidi iweke mkakati maamlu wa kufuatilia kama nchi
wananchama imeandaa mapango wa kuendeleza viwanda kulingana na
makubaliano yaliyofikiwa kwenye kikao cha leo,” alisema Waziri Mkuu
ambaye ameshiriki kikao hicho kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete.
Alisema yeye binafsi
amefurahishwa na kupitishwa kwa azimio la uendelezaji wa viwanda katika
nchi za SADC kwani unaendana na juhudi za Serikali ya Tanzania za kukuza
uchumi kupitia uendelezaji wa viwanda vya usindikaji.
“Nimefurahi kwa sababu azimio
hili linaendana na mpango wetu wa kuendeleza viwanda wa mwaka 2015/2016
hadi 2020/2021. Sisi tumelenga viwanda vya kusindika mazao ya wakulima,
wavuvi na wafugaji… kwa hiyo naamnini tutaenda vizuri na mpango mzima wa
Jumuiya hii,” alisema.
Kuhusu madeni ya michango kutoka
kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo, Waziri Mkuu alisema Tanzania iko
kwenye hatua nzuri ya ulipaji michango hiyo. “Jana nilipofika niliulizia
suala hilo, nikaambiwa kwamba Tanzania imekwishalipa kwa kiwango cha
kuridhisha. Nilitoa wito wakamilishe kulipa hiyo michango iliyobakia
kwenye maeneo husika,” aliongeza.
Mapema, Waziri Mkuu Pinda alisoma
salamu maalumu mbele ya wakuu wa nchi na washiriki wa mkutano huo zaidi
ya 500, zikiwa ni salamu maalum za kuwaaga zilizotolewa na Rais Jakaya
Kikwete. Rais Kikwete anamaliza muda wake mwishoni mwa mwaka huu na
hatapata nafasi nyingine ya kushiriki kikao cha wakuu wa nchi.
Kikao kijacho kimepangwa
kufanyika Agosti, 2016 nchini Lesotho ambapo Mfalme Letsie Mswati wa III
alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wakuu wa nchi wanachama kwenye
mkutano huo.
Katika hatua nyingine, wakuu wa
nchi za Jumuiya ya SADC wamechangua Rais Ian Khama Seretse Khama kuwa
mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo.
Katika kikao hicho waliazimia
kuendeleza mapambano dhidi ya magonjwa ya Kifua Kikuu, Malaria na
kuazimia kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwenye nchi
wanachama.
Mbali na kusisitiza utunzaji na
uhifadhi wa mazingira, waliazimia pia kila nchi itekeleze mpango wake wa
kilimo ili kuwa na akiba ya kutosha hasa ikizingatiwa hali ya ukame
ambayo imezikumba nchi za kusini mwa jangwa la Sahara na kuashiria uhaba
mkubwa wa chakula.
Post a Comment