Taasisi za Serikali Ziwe Tayari Kutumia Mtandao Mmoja wa Mawasiliano
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi
Ombeni Sefue akifungua mkutano wa Serikali Mtandao unaowahusisha
Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala,Wakurugenzi, Watendaji Wakuu wa Taasisi
na Wakala za Serikali unaofanyika katika Ukumbi wa AICC leo jijini
Arusha.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo Sihaba Nkinga akifuatilia mada
mbalimbali wakati wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Serikali Mtandao ngazi ya
Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala, Wakurugenzi na Watendaji wakuu wa
Taasisi za Serikali unaoendelea jijini Arusha.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Mwaka wa Serikali Mtandao wakifuatilia mkutano huo leo jijini Arusha.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue (katikati) akiwa
katika picha ya pamoja na Makatibu wakuu, Makatibu Tawala wa
mikoa,Wakurugenzi wa Halmashauri na Watendaji wa Taasisisi mbalimbali za
Serikali mara baada ya kufungua Mkutano wa Serikali Mtandao leo jijini
Arusha.
...................................................
Na Aron Msigwa -Arusha
Serikali
imezitaka Wizara,Idara,Wakala na Taasisi mbalimbali kuanza kujiandaa
na mageuzi makubwa ya matumizi ya Mfumo mmoja wa Mawasiliano kupitia
Serikali Mtandao ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuondoa urudufu
wa mifumo ya TEHAMA inayofanya kazi za aina moja serikalini.
Hatua
hiyo ya Serikali imekuja kufuatia kuwepo kwa mifumo ya TEHAMA ya
kutolea huduma kwa umma katika Taasisi mbalimbali za Serikali isiyoweza
kuwasiliana na kubadilishana taarifa jambo linalosababisha usumbufu kwa
wanannchi wanapotakiwa kuwasilisha taarifa za aina moja kwenye taasisi
tofauti za serikali.
Akifungua Mkutano wa
Serikali Mtandao wa Makatibu Wakuu,Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi
na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Wakala za Serikali leo jijini Arusha
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema kuwa mabadiliko hayo ni
Sehemu ya mpango wa Serikali wa kuhakikisha kuwa inawafikishia
wananchi huduma bora kwa haraka, gharama nafuu na mahali walipo.
Ameeleza
kuwa hatua ya Tanzania kuweka msukumo kwenye Serikali Mtandao
haiepukiki kwa kuwa imelenga kuboresha utendaji wa kazi ndani ya
Serikali, kuongeza tija, ufanisi na kasi ya ubadilishanaji wa taarifa
ndani ya Serikali.
"Jambo hili la Serikali
mtandao tumeshalizungumza sana Serikalini kutokana na umuhimu wake
tumekutana watoa maamuzi kwa mara ya kwanza ili kufikia malengo ya
Serikali mtandao tuliyojiwekea kila mmoja achukue hatua kuhakikisha kuwa
fursa zilizopo zinatumika ipasavyo,tumeshaanza hakuna kurudi nyuma
katika jambo hili"
Amesema Serikali imefanya
mageuzi makubwa katika uwekezaji wa miundombinu ya TEHAMA ikiwemo
uanzishaji wa Mkongo wa Taifa, Kituo cha Taarifa Serikalini (National
Data Centres) ili kuhakikisha kuwa huduma za Serikali zinapatikana kwa
urahisi, haraka,uwazi,gharama nafuu,wakati wowote na mahali popote
nchini.
"Serikali tumefanya uwekezaji mkubwa
kwenye miundombinu ya TEHAMA ikiwemo Mkongo wa Taifa (NICTBB), Mtandao
wa Serikali (GovNet),Vituo vya kitaifa vya Data na kutenga Masafa ya
Intaneti ya Serikali, hii yote ni kuwahakikishia wananchi huduma bora za
Serikali mtandao" Amesisitiza Balozi Sefue.
Amefafanua
kuwa Serikali imeendelea kuboresha Sera na sheria, kutokana kutungwa
kwa Sera ya TEHAMA ya mwaka 2003 na Mpango Mkakati wa Kitaifa wa
Serikali Mtandao 2013 pamoja na sheria ya Elekroniki na Mawasiliano ya
Posta (Elektonic and Postal Communicatins),Sheria ya Miamala ya
Kielektroniki 2015 na Sheria ya Makaosa ya Mitandao ya mwaka 2015.
Ameongeza
kuwa Serikali inaendelea kujenga uwezo wake wa ndani ili kuondoa
utegemezi wa wakandarasi wa nje katika ujengaji wa mifumo ya TEHAMA hapa
nchini ambao huigharimu serikali fedha nyingi.
"Tunalo
jukumu kubwa la kuhakikisha tunaimarisha na kujenga uwezo wetu wa ndani
ili kuondoa utegemezi kutoka nje, wataalamu sasa tunao na tutaendelea
kujenga uwezo wetu wa miundombinu ya ndani ili kuwahudumia wananchi"
Ametoa
wito kwa wataalam wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
Tume ya Mipango na Wakala ya Serikali Mtandao kushirikiana katika
kuhakikisha Serikali Mtando inaingizwa katika mpango wa taifa wa miaka
mitano.
Aidha, amezitaka Taasisi ambazo zina
kiwango kidogo cha utekelezaji wa Serikali mtandao kushirikiana na
Wakala ya Serikali Mtandao kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha kuwa
matumizi ya TEHAMA yanaleta ufanisi katika kujenga Serikali Mtandao
madhubuti.
"Taasisi za Serikali ambazo bado
zina kiwango kidogo cha utekelezaji wa Serikali Mtandao zinatakiwa
kuchagua jambo moja, kukubali kubadilika au kubadilishwa" amesisitiza
na kuongeza kuwa Serikali inaendelea kuzijengea uwezo taasisi hizo
ziweze kuendana na mabadiliko yaliyopo.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw.Felix Kijiko Ntibenda
akiwakaribisha washiriki wa mkutano huo jijini Arusha amesema kuwa
kufanyika kwa mkutano huo ni mwanzo mzuri wa kuelekea Serikali Mtandao
Imara.
Amesema matumizi ya TEHAMA katika
shughuli za Serikali yameisaidia Serikali kuongeza ufanisi katika
shughuli mbalimbali ikiwemo utambuzi, tiba, ukusanyaji wa mapato ya
Serikali na huduma za matibabu.
Amesema kupitia
mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa njia ya mtandao mkoa wa Arusha
anaouongoza umenufaika kwa kiasi kikubwa kwa kuongeza mapato ya ndani na
kufanikiwa kupunguza vitendo vya wizi na ubadhirifu.
Awali
akizungumza kuhusu mkutano huo Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali
Mtandao (e Government Agency) Bw. Jabir Bakari amesema kuwa mkutano huo
umelenga kuongeza ufanisi katika matumizi ya Rasilimali za TEHAMA
nchini.
Amesema Serikali inaendelea kufanya
vizuri katika kufanikisha lengo kubwa la kufikisha huduma kwa wananchi
pia kufanikisha mpango wa kuwa na mfumo mmoja utakaowezesha taarifa zote
za wananchi kuwa katika sehemu moja.
Kuhusu
mkutano huo Dkt.Jabiri amesema kuwa washiriki watapata fursa ya
kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano katika kutekeleza jitihada
za Serikali Mtandao nchini pamoja na Kutafuta ufumbuzi wa changamoto za
serikali mtandao zilizopo nchini ili kuleta maendeleo ya kiuchumi na
kijamii.
Aidha,amesema washiriki watapata fursa
ya kujifunza kutoka kwa wataalam wengine wanaohusika na Serikali
Mtandao kutoka nchi zinazofanya vizuri katika eneo la Serikali mtandao
zikiwemo India na Singapore.
Pia amesema mada
mbalimbali zitajadiliwa zikiwemo za usimamizi wa Serikali Mtandao nchini
Tanzania, Hali ya miundombinu ya Serikali mtandao na Utekelezaji wa
Mpango wa Uendeshaji wa Serikali kwa uwazi.
Mada
nyingine zitahusu uimarishaji wa uwazi na Mfumo wa Takwimu huria nchini
Tanzania na uimarishaji wa huduma za Serikali kupitia simu za mkononi
na mifumo inayotumika kutoa huduma kwa wananchi.
Post a Comment