Header Ads

Wanaotaka Urais ni Wakombozi wa Taifa gani?

 HUU ni mwaka wa uchaguzi, mwaka ambao rais wa awamu ya nne wa Tanzania anakabidhi kijiti kwa rais mwingine atakayejulikana kabla ya Novemba mwishoni mwa mwaka.
 
Nashukuru kuwa miongoni mwa Watanzania walio hai ambao wameshuhudia uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi vya siasa mwaka 1995, lakini pia niliyeshuhudia uchaguzi wa mwisho wa chama kimoja mwaka 1990, ingawa nilikuwa shule ya msingi sikuwa nikijua kinachoendelea.
 
Kimsingi ninachataka kujadili hapa ni namna nafasi ya urais ilivyopoteza maana, ile nguvu iliyotumiwa na rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere haiakisi chochote katika hali tuliyonayo sasa.
 
Nazungumzia Tanzania kwa ujumla nikimaanisha bara na visiwani, mbio za kusaka urais hazionyeshi uzalendo wala kutaka kuwa watumishi wa wananchi wanaoendelea kuhangaika kutokana na maadui watatu aliowatangaza Mwalimu Nyerere: Ujinga, Maradhi na Umasikini.
 
Cha kushangaza, vurugu kubwa ilianzia katika chama tawala (Chama Dola), Chama Cha Mapinduzi (CCM). Tofauti na ambavyo mgeni yeyote kutoka nje ya mipaka yetu angedhani kuwa vurugu zinaletwa na wapinzani, hapa kwetu chama kilicho madarakani ndicho kilichotaka kuvuruga kutokana na ulafi wa wachache, waroho wa madaraka wanaotumia kila mbinu kuingia Ikulu; Ikulu ambayo Mwalimu Nyerere aliita mzigo.
 
Miezi kadhaa niliwahi kuhudhuria kongamano la wiki ya ukombozi wa Afrika iliyoanza Mei 25-29, nilivutiwa na mdahalo wa ‘Wazee’ wawili Profesa Issa Shivji na Balozi Ibrahim Kaduma.
 
Viumbe hawa historia zao zinajiandika zenyewe, Balozi Kaduma alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika serikali ya awamu ya kwanza pia alikuwa balozi akiiwakilisha nchi yetu mataifa ya nje na mwanasiasa mkongwe anayezijua siasa za nchi hii.
 
Profesa Shivji yeye ni msomi wa sayansi ya siasa, sheria na ni  Nyagoda wa kwanza katika Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambacho kwa sasa kinashikiliwa na Profesa Penina Mlama, kama hiyo haitoshi Profesa Shivji ameingia katika jopo la wasomi wanaochimba historia na kazi za Mwalimu Nyerere katika Kavazi la Mwalimu Nyerere. Hayo ni machache tu katika sifa zinazowagubika ‘Wazee’ hawa.
 
Balozi Kaduma, alizungumzia ahadi ya viongozi wa Afrika juu ya kupatikana uhuru wa fikra ambayo anaamini mpaka sasa haujapatikana.
 
“Mei 25, 1963 Mfalme Haile Selassie wa Ethiopia, alifanya mkutano wa nchi huru za Afrika jijini Addis Ababa, ili kutafuta namna ya kuzikomboa nchi nyingine hasa za Kusini mwa Afrika zilizokuwa zikiendelea kukaliwa kimabavu na wakoloni, walihudhuria viongozi wan chi 12 zilizokuwa huru.
 
“Walikubaliana kuwa ili tuwe huru vinahitajika vitu vitatu, kwanza upatikane uhuru wa bendera ili tuwe na uwezo wa kujiamulia mambo yetu, pili upatikane uhuru wa fikra na hatimaye uhuru wa uchumi ili kumiliki uchumi wetu, lakini mpaka anaondoka nchi za Afrika zimefanikiwa kupata uhuru wa bendera tu basi,” alisema Balozi Kaduma.
 
Katika maelezo yake alibainisha kuwa Tanganyika ilipopewa uhuru Desemba 9, 1961 Mwalimu Nyerere alidumu katika nafasi ya Uwaziri Mkuu kwa siku 42 tu akaachia nafasi hiyo kwa Rashid Kawawa, yeye alikwenda kuimarisha chama ili kuwaandaa wananchi na uhuru wa kifikra.
 
Kwa sababu tulitawaliwa na wazungu kwa zaidi ya karne moja hivyo aliamini kuna haja ya kubadili fikra za wananchi waamini wanaweza kujitawala wenyewe, wafanye kazi kwa bidii bila kutegemea msaada wa wakoloni.
 
Juni 28, 1962 Tanganyika ilitangazwa kuwa Jamhuri ndipo Mwalimu alipochukua nafasi ya urais mpaka alipoamua kung’atuka mwaka 1984. Yote hiyo inaonyesha namna viongozi wetu wa mwanzo walivyotumia madaraka kwa faida ya wengine tofauti na sasa.
 
Nikiangalia historia ya Zanzibar na Abeid Amani Karume wakiwemo kina Abdulrahman Babu, naona kile kile kilichofanywa na Mwalimu Nyerere kukataa kuwa chini ya Malkia.
 
Kwa sababu kama angebweteka kuwa Waziri Mkuu na Malkia wa Uingereza kuwa mtawala kama inavyotamka Katiba ya Tanganyika ya mwaka 1954, maana yake mpaka leo tungekuwa tunapangiwa cha kufanya na koloni la Uingereza.
 
Zanzibar ilikuwa chini ya utawala wa Waarabu tangu mwaka 1856 mpaka Sultani alipopinduliwa mwaka 1964. Ikiwa ni mwezi mmoja baada ya kutangazwa uhuru wa visiwa hivyo mwaka 1963.
 
Kwa sababu kutokana na vuguvugu la mabadiliko barani Afrika, Uingereza ilifanya mashauriano na utawala wa Oman kuwa watumie sanduku la kura kuwapa uongozi Wazanzibari ili wawatawale kwa mlango wa nyuma.
 
Vyama vya ASP(Afro Shirazi Party), ZNP (Zanzibar Nationalist Party) na ZPPP (Zanzibar and Pemba People’s Party) vilichuana katika uchaguzi tangu mwishoni mwa miaka ya 1950 bila mafanikio, kila uchaguzi ulipoitishwa kulitokea vurugu watu wakauana, mpaka ZNP na ZPPP walipounganisha viti vyao katika uchaguzi wa mwaka 1963 na kuunda serikali ya mseto Desemba 12, 1963 chini ya Waziri Mkuu Mohammed Shamte akiongozwa na Sultani Jamshid Bin Abdullah.
 
Yaani Wazanzibari walikuwa na madaraka, lakini Waarabu nao walikuwa na madaraka lakini madaraka ya wageni yalikuwa makubwa kwa maana ya kuongoza maamuzi yote kama ilivyo Uingereza, Waziri Mkuu David Cameron anaongoza serikali lakini Malikia Elizabeth ndiye mkuu wa dola.
 
Siku ya uhuru wa Zanzibar, waliitwa viongozi wote wakiwemo kina Abeid Karume na kiongozi wa Chama cha Umma, Abdulrahman Babu. Katika hotuba yake Babu alitoa kauli tata kwa kusema, wanashukuru kwa uhuru lakini watafanya kitu cha kushangaza ndani ya mwezi mmoja.
 
Naami, ndani ya siku 32 Zanzibar kulifanyika mapinduzi ambayo yalirudisha hadhi ya Mwafrika na kukoma utawala wa Kiarabu uliodumu kwa karne moja (1856-1964).
Uhuru ulitangazwa Desemba 12, 1963 na mapinduzi yalifanyika Januari 12, 1964. Hadhi ya wakwezi na wavuvi ilirudi Zanzibar na Sultani Jamshid mpaka sasa anaishi uhamishoni Uingereza.
 
Profesa Shivji anasema wakoloni hawakufurahishwa na kujitawala kwetu, walitaka kuona bado wanaongoza uchumi wa Afrika na kutugeuza watumwa katika ardhi iliyotukuza.
 
Hivyo anashangazwa kuona katika mataifa ya Afrika kuna vyama vya siasa vinavyotumia nguvu nyingi kuingia madarakani utadhani Afrika haijakombolewa.
Zinatumika nguvu za pesa kuingia Ikulu, lakini hakuna kinachofanyika kuhakikisha tunaondokana na matatizo yanayotukabili. Ulafi na tamaa ya madaraka inawafanya Waafrika wasahau matatizo ya wananchi na kujali matumbo yao.
 
Kumbuka Abeid Karume, alianza harakati za kuikomboa Zanzibar tangu mwanzoni mwa miaka ya 1950 chini ya Chama cha African Association (AA), hata kufikia kuunganisha vyama vilivyokuwa na mrengo mmoja yaani Shirazi Association (SA) mwaka 1957 na kuundwa Afro-Shirazi Party (ASP).
 
Yalipofanyika mapinduzi mwaka 1964 likaja wazo la kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar, Karume hakufanya ajizi akakubali haraka nchi zaikaunganishwa na kuundwa Tanzania, Aprili 26, 1964 ikiwa ni miezi miwili na wiki kadhaa tangu kutangazwa kuwa Rais wa Zanzibar, alikubali kuachia madaraka yake na kuwa chini ya Julius Nyerere, ni moyo wa kizalendo unaoonyesha hakuwa mroho wa madaraka.
 
Nimeeleza hayo kwa kuakisi visa na vurugu zinazofanyika sasa katika nchi inayosifika kwa ukarimu, watu wanapigana vikumbo kuingia Ikulu kwa namna yoyote ile, kuna watu wanapoteza utu wao kwa sababu ya kuwaingiza madarakani viongozi hawa, haifai hata kidogo.

No comments

Powered by Blogger.