Taifa Stars Kuondoka Nchini JUMAMOSI
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inatarajiwa kuondoka
nchini siku ya jumamosi usiku kuelekea Muscat Oman, kucheza mchezo wa
kirafiki kabla ya kuunganisha kuelekea Istambul Uturuki kwa kambi ya
wiki moja.
Taifa Stars imepata mwaliko wa kucheza mchezo wa kirafiki na
timu ya Taifa ya Oman tarehe 24 Agosti, 2015 usiku, ambapo baada ya
mchezo huo timu itasafiri kuelekea nchini Uturuki katika jiji la
Istambul.
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Oman (OFA) liliomba
kucheza mchezo wa kirafiki na Taifa Star kabla ya kuwavaa Turkemebistan
katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia Septemba 03, 2015 kwa
bara la Asia, ambapo kocha wake mkuu Mfaransa Paul Leguen aliomba
kucheza na vijana wa Charles Mkwasa kujiandaa na mechi hiyo.
Mara baada ya mchezo huo Taifa Stars itaelekea Istambul
katika mji wa Kocael hoteli ya Kartepe kwa kambi ya wiki moja, ikiwa
nchini Uturuki Stars inatarajiwa kucheza michezo miwili ya kirafiki
kabla ya kurejea nchini kucheza na Nigeria Septemba 05, 2015 mchezo wa
kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika.
Kocha mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa anatarajiwa kutoa
orodha ya kikosi chake cha wachezaji 22 mwishono mwa wiki watakaosafiri
kuelekea nchini Uturuki kwa kambi ya hiyo ya kujiandaa na mchezo dhidi
ya Nigeria.
Mshambuliaji Adi Yussuf anayechezea klabu ya Mansfield Towny
ya Uingereza alitarajiwa kujiunga na timu nchini Uturuki, lakini
kutokana na majeruhi aliyoyapata hivi karibuni katika michezo ya ligi,
uongozi wa Mansfield umeomba mchezaji huyo kutojiunga na timu ya Taifa
kwa ajili ya kupata mataibabu zaidi.
Adi aliumia wiki iliyopita katika mchezo dhidi ya Nottingham
Forest ambapo kwa sasa anaendelea na matibabu chini ya uangalizi wa
klabu hiyo, na pindi atapokuwa fit atapata nafasi ya kujumuika na
kuitumika timu ya Taifa ya Tanzania.
Post a Comment