Header Ads

UN na EU waendeleza Kampeni ya Uelewa wa Malengo ya Maendeleo Endelevu


UMOJA wa Ulaya (EU) na Umoja wa Mataifa (UN) wamejiunga pamoja kuendesha kampeni ya uelewa wa malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) nchini Tanzania, Aidha kwa pamoja wamezuru miradi iliyofadhiliwa na EU.

 Wakiwa Mkoani Iringa wamepata nafasi ya kuzungumza na wanachuo 1,000 kutoka vyuo vikuu vya Iringa na Mkwawa kwenye semina iliyoelezea malengo hayo ya dunia ambayo ni sehemu ya ajenda 2030 ya maendeleo endelevu duniani. 

Kampeni hiyo imelenga kuwafanya vijana waelewe malengo 17 ya dunia ambayo kwa sasa yana mwaka mmoja tangu yapitishwe na kuwatanabaisha wajibu wao katika kufanikisha utekelezaji wake ndani ya mazingira ya Tanzania.



Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini ambaye pia ni Afisa Miradi, Anna Muro (kushoto) akisalimiana na mmoja wa wahadhiri wa chuo hicho alipowasili katika ofisi za Mkuu wa Chuo Kikuu cha Iringa (UOI), Prof Joshua Madumulla akiwa ameambatana na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez.

Semina katika vyuo hivyo ni sehemu ya mpango madhubuti wa Umoja wa mataifa uliozinduliwa Arusha Mei mwaka huu na Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Bw. Alvaro Rodriguez wenye lengo la kuwaelimisha vijana zaidi ya 30,000 ifikapo mwaka ujao kuhusu malengo hayo ya dunia.

 Ujumbe huo wa EU na UN pia ulipata nafasi ya kutembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na EU ukiwamo wa Boma la Kijerumani ambalo lilikarabatiwa kwa ruzuku ya EU kupitia 'fahari yetu – Southern Highlands Culture Solutions'. Boma hilo ni moja ya majengo ya zamani katika mji wa Iringa na lilijengwa na Wajerumani mwaka 1900 kama hospitali ya kijeshi. 

Baada ya vita ya Kwanza ya Dunia, jengo hilo lilibadilishwa matumizi na watawala wapya, Uingereza, na kulifanya kuwa jengo la utawala. EU imesema inaona fahari kuwa mmoja wa wawekezaji wakubwa katika sekta ya sanaa na urithi wa kitamaduni nchini Tanzania, ikifadhili miradi 10 iliyo chini ya programu ya 10 ya EDF ya kusaidia masuala ya kitamaduni. 


Mkuu wa Chuo Kikuu cha Iringa (UOI), Prof Joshua Madumulla akiwa kwenye mazungumzo na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez aliyeambatana na Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini ambaye pia ni Afisa Miradi, Anna Muro (upande wa kushoto katikati) pamoja na Mtaalam wa Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Hoyce Temu (kushoto) alipotembelewa ofisini kwake na ugeni huo, Kulia ni Meneja wa Mradi wa Fahari Yetu, Jan Kuever pamoja na Katibu Tawala Msaidizi -Miundombinu wa Mkoa wa Iringa, Henry Mditi.

Masuala yanayohusu urithi wa kitamaduni ni muhimu katika kuchagiza ukuaji wa uchumi, ajira na huku ikifuma mahusiano ya kijamii, na kutoa fursa ya kuboresha utalii endelevu mkoani Iringa huku ikileta faida kwa wakazi wa eneo hilo. Bw. Rodriguez, akizungumza katika kampeni hiyo alisema kwamba ajenda 2030 ambayo ni ajenda ya maendeleo endelevu inahitaji ushiriki wa kila mmoja.

Aliwapongeza wanachuo hao na wanazuoni kwa kujikita kutambua malengo hayo ya dunia. Aidha aligusia umuhimu wa vijana kushiriki katika masuala ya maendeleo kutokana na ukweli kuwa, kwa taifa kama la Tanzania vijana ni asilimia 60 ya wananchi wote waliopo.Alisema kwamba vijana wanajukumu kubwa la kushiriki katika maendeleo hayo kwa lengo la kuipeleka nchi katika hatua nyingine ya maendeleo. 


Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez akiwa ameongozana na Katibu Tawala Msaidizi -Miundombinu wa Mkoa wa Iringa, Henry Mditi kuelekea kwenye ukumbi wa mikutano Chuo Kikuu cha Iringa.

Hata hivyo alisema kwamba ni wajibu wa kila mtu hasa vijana, kuhakikisha kwamba malengo hayo ya dunia yanafanikiwa . 

Alisema Umoja wa Mataifa kwa kusaidiwa na wadau wake muhimu kama Umoja wa Ulaya, utaendelea kusaidia Watanzania kuwajibika katika shughuli mbalimbali za maendeleo katika kuunga mkono malengo hayo ya dunia. 

Mmoja wa washiriki alipongeza Umoja na wa Mataifa kwa kuwafikia vijana wa vyuoni na kuwapa semina hiyo. “Ninajisikia mtu mwenye bahati kupata nafasi ya kujifunza maendeleo endelevu kutoka kwa Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini. 

Nikiwa kama kijana, naona faraja kuona kwamba viongozi wetu wanafuata maelekezo yaliyofafanuliwa kwenye malengo 17 ya maendeleo endelevu; naamini kama tukijitahidi kuyafikia ifikapo 2030, basi Tanzania na duniani kwa ujumla itakuwa eneo jema la kuishi. Na kwa kuwa sasa natambua kuhusu malengo hayo ya dunia, ninaweza kutoa mchango wangu kusaidia kuyafikia -najisikia kuwezeshwa sana.” amesema Mary, mmoja wa washiriki. 


Mkuu wa Chuo Kikuu cha Iringa (UOI), Prof Joshua Madumulla akisoma taarifa fupi ya Chuo Kikuu cha Iringa mbele ya ujumbe kutoka Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya wakati semina kuhusu malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambayo ni sehemu ya ajenda 2030 ya maendeleo endelevu duniani kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa.


Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela akizungumza kwenye semina ya malengo ya dunia kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa ambapo aliwaasa wakawe mabalozi wazuri wa malengo hayo kwenye jamii zao na wanafunzi wenzao wa vyuo vingine.

No comments

Powered by Blogger.