Header Ads

Zahanati ya MCHOMORO kukamilika Mwezi Machi Mwakani

Mbunge wa Namtumbo Eng. Edwin Ngonyani akitoa maelekezo kwa mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa zahanati ya Mchomoro mara baada ya kukagua ujenzi wa zahanati hiyo. 

...................................


Mbunge wa Jimbo la Namtumbo ambae pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amewahakikishia wananchi wa Kata ya Mchomoro Wilayani humo kuwa jengo la Zahanati ya kijiji hicho litakamilika na kuanza kutoa huduma mwezi Machi mwakani kama ilivyopangwa.

Jengo hilo ambalo ujenzi wake unatokana na kuharibika kwa jengo la zamani kulikosababishwa na ujenzi wa barabara ya Songea- Tunduru linatarajiwa kuendelezwa ili kuwa kituo cha afya na hivyo kuhudumia idadi kubwa ya wananchi wa Kata hiyo.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo hilo Eng. Ngonyani amewakabidhi wasimamizi wa ujenzi huo fedha kwa ajili ya kukamilisha hatua upauaji wa jengo hilo na kusisitiza umuhimu wa  matumizi sahihi ya fedha hizo ili ziwiane na ubora wa kazi.

“Hakikisheni mnazingatia makubaliano ili zoezi la kuezeka jengo hili la Zahanati likamilike kabla ya Januari na hivyo kuwezesha zahanati hii kuanza kazi mapema mwezi Machi”. Amesema Eng.Ngonyani.

Zahanati hiyo ambayo ujenzi wake unagharamiwa na Mbunge wa Namtumbo akishirikiana na kampuni ya Mantra Tanzania LTD na nguvu za wananchi wa kata hiyo inatarajiwa kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya cha kata hiyo mara zoezi la ujenzi wa majengo mengine utakapokamilika.

Naye msimamizi wa ujenzi wa zahanati hiyo Bw, Yasini Languka amemhakikishia Mbunge huyo wa Nmatumbo kwamba fedha zinazopelekwa kwaajili ya ujenzi huo zinatumika kama ilivyokusudiwa ili kufikia lengo la kuifungua upya zahanati hiyo ifikapo mwezi Machi mwakani na hivyo kuwaondolea usumbufu wananchi wa Kata hiyo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo amekagua barabara ya  Mangaka –Tunduru- Matemanga –Namtumbo hadi Songea na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) pale wanapoona vitendo vya hujuma katika barabara hiyo ikiwemo utengenezaji na uegeshaji wa magari mabovu katika barabara hiyo.

Naibu Waziri Ngonyani yupo katika ziara ya kukagua Miundombinu ya barabara, Bandari na Mawasiliano katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa zahanati ya Mchomoro wakijadiliana jambo mara baada ya kupokea fedha kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Eng. Edwin Ngonyani kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.


Muonekano wa jengo la zahanati ya Mchomoro wilayani Namtumbo ambayo ipo katika hatua za za mwisho za ujenzi wake, Zahanati hiyo inatarajiwa kuendelezwa ili kuwa kituo cha afya ya kata hiyo.

No comments

Powered by Blogger.