Header Ads

Mtendaji Mkuu TEMESA aagiza Kutumika Kwa Wataalamu Kutoka Vyuo vya Veta

Na Theresia Mwami

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu amemuagiza Meneja wa TEMESA Katavi Mhandisi Sunday Kyungai kuwatumia wataalamu waliohitimu katika chuo cha VETA kilichoko Mpanda ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mafundi katika kituo hicho.

Dk Mgwatu ametoa agizo hilo alipotembelea Kituo cha TEMESA Mkoani Katavi na kujione utendaji kazi wa kituo hicho.
“Nakuagiza Meneja katika kuajiri wataalamu mzingatie wataalam hasa wale waliohitimu kutoka Vyuo vya VETA nchini” alisisitiza Dk Mgwatu.

 Dkt Mgwatu ameongeza kuwa vituo vya wakala huyo vinatakiwa  kuwa wabunifu katika kutatua matatizo mbalimbali badala ya kutegemea kila kitu kutoka Makao Makuu ya TEMESA.

Aidha  Dkt. Mgwatu amemuagiza Mhandisi Kyungai kuwasilisha kwake mpango wa kujenga karakana mpya kwenye eneo jipya la  TEMESA lililopo Katavi katika mji wa Mpanda.

Kwa upande wake Meneja wa TEMESA Katavi Mhandisi Sunday Kyungai amemuhakikishia  Mtendaji Mkuu kuwa  watazingatia  kuajiri watumishi wa TEMESA katika kituo cha Katavi kwa kuzingatia agizo alilolitoa la kupata wataalamu kutoka vyuo vya VETA nchini.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu yuko katika ziara ya kikazi katika vituo vya TEMESA Nyanda za Juu Kusini kutembelea na kukagua vituo hivyo ili kujionea changamoto mbalimbali pamoja na utendaji kazi wake.

No comments

Powered by Blogger.