( MAKALA ) Mfumo wa TEHAMA wazidi Kuongeza Wigo wa Utoaji Huduma Kwa Wananchi
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
Dar es Salaam.
SERA ya
Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ya mwaka 2003, pamoja na
mambo mengine inasisitiza umuhimu wa Serikali kutumia fursa za TEHAMA katika
utendaji kazi wa kila siku na utoaji huduma kwa wananchi.
Katika
kutekeleza sera hiyo, mwaka 2004 Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma
(OR-MUU) ilianza kuchukua hatua mbalimbali kuongeza matumizi ya TEHAMA katika kuimarisha
mifumo ya utoaji habari na huduma kwa wananchi.
Moja ya
maeneo ya TEHAMA ambayo Serikali imewekeza na kupata mafanikio makubwa ni
pamoja na eneo la tovuti ambapo hadi kufikia mwaka 2010 takribani Taasisi zote
za Serikali zilikuwa na tovuti.
Katika kipindi cha mwaka mmoja wa
Serikali ya Awamu ya Tano, kumekuwepo na mapinduzi makubwa katika mfumo wa upashanaji wa habari na
utoaji wa huduma kwa umma kupitia tovuti.
Mtendaji
Mkuu wa Serikali Mtandao, Dkt. Jabiri Bakari anasema taasisi za umma zinapaswa
kuwa na tovuti zitakazosaidia wananchi kupata kwa urahisi taarifa zinazohusu
shughuli na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hizo.
“Tovuti
za Serikali zinatakiwa kuwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza na
mwananchi anapofungua tovuti hizo lugha itakayoonekana kwanza iwe ni
Kiswahili na muda wowote mwananchi huyo anaweza kubadili kwenda kwenye
lugha ya Kiingereza”.
Dkt.
Bakari amesema kuwa Wakala imetoa miongozo ya kusimamia na kuendesha
tovuti hizo na unapatikana kwenye tovuti ya Wakala www.ega.go.tz sehemu ya
Miongozo na Viwango.
Akizungumzia
mafanikio ya Wakala hiyo, Dkt. Jabiri anasema Wakala imetengeneza mifumo
mbalimbali na kuweka miundombinu ya kuwezesha taasisi za umma kutumia Tehama
katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Tovuti
Kuu ya Serikali ni zao la kwanza la Wakala na ilibuniwa na kusanifiwa na
wataalam wa ndani. Katika tovuti hiyo ambayo pia ni mfumo, ina taarifa za
baadhi ya taasisi za umma, sekta mbalimbali na huduma zake pamoja na balozi
zilizoko nchini na zile za kwetu zilizoko nje ya nchi”, anasema Dkt.
Bakari.
Anaongeza
kuwa mfumo mwingine uliotengenezwa na Wakala hiyo ni Tovuti Kuu ya Ajira ambayo
humwezesha mwananchi kuona ajira mbalimbali zinazotangazwa na Serikali ambapo
muombaji wa ajira anaweza kutuma wasifu wake kwa njia ya mtandao na
nafasi zinapotangazwa zenye kuhitaji mtu mwenye sifa hizo.
Kwa mujibu wa Dkt
Jabiri anasema jitihada mbalimbali zinatekelezwa na Wakala ili
kuwezesha taasisi za umma kutoa huduma zao kwa njia ya mtandao kwa kuongeza
uwezo wa wataalam wa Tehama kwa kuwapa maarifa na ustadi wa kubuni.
Dkt. Jabiri anasema
Wakala imetoa mafunzo kuhusu usimamizi na Ujenzi wa Mtandao wa Mawasiliano
Serikalini kwa taasisi za umma 149 wakiwemo Maofisa TEHAMA 226, Mafunzo ya
uendeshaji wa Vituo vya data kwa Taasisi za umma 91 wakiwemo Maofisa TEHAMA
162.
Aidha Mafunzo ya
Usimamizi wa Mfumo wa Barua Pepe Serikalini yametolewa kwa taasisi 157 pamoja
na Mafunzo ya usimamizi wa taarifa tovuti za serikali yametolewa kwa taasisi
71.
“Mafunzo ya uwekaji
taarifa katika tovuti kuu yametolewa kwa taasisi 86 na Mafunzo hayo yanaendelea
kutolewa kwa kila taasisi ambayo inatengenezewa Tovuti na Wakala” anasema Dkt.
Jabiri.
Kwa upande wake Meneja
Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala wa Serikali Mtandao, Suzan Mshakangoto
anasema mbali na kuanzisha mtandao huo Serikali imeziagiza taasisi zote za umma
kuhuisha taarifa katika tovuti zake na Tovuti Kuu ya Serikali
(www.tanzania.go.tz).
Anaongeza kuwa tangu
kuanzishwa kwa tovuti hizo kumesaidia kuongeza kasi ya utendaji, uwazi,
ufanisi, uwajibikaji na tija katika utoaji wa taarifa na huduma kwa wananchi,
pamoja na changamoto kadhaa zilizojitokeza katika usimamizi wa tovuti hizo.
Akifafanua zaidi
anasema miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na tovuti za taasisi za umma
kutokuwa na taarifa mpya na za mara kwa mara, na kutofuatwa kwa mwongozo uliowekwa unaosisitiza usanifu wa tovuti
hizo.
Naye Mkurugenzi wa
Habari, Hassan Abbas anasema ofisi yake kwa kushirikiana na e-GA tayari
imezisaidia Halmashauri 93 kuhuisha taarifa zilizopo katika tovuti zao ili
kuwawezesha wananchi kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali katika
maeneo yao.
Abbas
anasema tovuti ni mojawapo ya nyenzo na njia rahisi na ya haraka ya kutoa taarifa
na kufikisha huduma kwa umma kwani miaka
ya nyuma taarifa na huduma za Serikali zilitolewa kwa njia ya kutembelea ofisi
husika au kwa kupitia vyombo vya habari.
Anasema Serikali imetoa
mafunzo kwa Maafisa Habari katika Wizara, Idara, Wakala na Taasisi mbalimbali
jinsi ya kuboresha taarifa katika tovuti zao, na kuanzia sasa ofisi yake itaanza kufanya tathimini
ili kufahamu Wizara ambazo hazijaanza kuhuisha taarifa zake.
Kwa mujibu wa Abbas
anasema Serikali imekusudia kupanua wigo wa mawasiliano katika Wizara, Idara,
na Taasisi zake kwa kuwahimiza Maafisa Habari kutumia zaidi mitandao ya kijamii
kwa ajili ya kujibu na kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zinazoelekezwa kwa
Serikali.
Katika kuboresha
mfumo wa mawasiliano Serikalini, ofisi yake imeanzisha akaunti ya twitter ya;
msemaji wa Serikali@TZ_Msemaji Mkuu ambayo mwananchi anaweza kuifuata akaunti
hiyo kwa kutafuta Msemaji Mkuu wa Serikali on Twitter.
Anasema wananchi
wengi kwa sasa wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuendesha mijadala
mbalimbali ambayo baadhi yao imekuwa ikipotosha ukweli kuhusu utelekezaji wa
sera mbalimbali za Serikali.
Abbas anasema
jukumu la kuboresha mawasiliano kati ya
Serikali na Wananchi ni suala mtambuka, na hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari wa
Wizara, Idara, Taasisi, Wakala za Serikali kutoogopa kutoa taarifa muhimu kwa
waandishi wa habari.
“Waandishi wa habari wasitoe taarifa zisizofanyiwa utafiti wa
kutosha kwa wananchi, ni vyema sote tushirikiane katika kutoa taarifa sahihi
kwa wananchi kuhusu sera na mikakati ya serikali ili kuleta maisha bora kwa
watanzania wote” anasema Abbas.
Kwa kutambua umuhimu
wa tovuti kama nyenzo kuu ya mawasiliano, Serikali kupitia Mradi wa Uimarishaji
wa Mifumo ya Umma (PS3) unaofadhiliwa na shirika la misaada la Marekani iliunda
kikosi kazi kwa ajili ya uhuishaji wa tovuti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa
(TAMISEMI)
Kikosi kazi hicho
kinahusisha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ofisi ya Rais-
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), na Wakala wa Serikali
Mtandao (E-GA).
Msimamizi
wa Mifumo ya Taarifa wa PS3, Bunto Mbozi anasema tovuti nyingi za TAMISEMI zimetengenezwa,
zinasimamiwa na kuendeshwa bila kuwepo na utaratibu unaofanana, hali hiyo inasababisha uwepo wa tovuti
zisizokidhi viwango na ubora kufuatana na mahitaji ya watumiaji.
Anaongeza kupitia
mradi, PSE3 imekusudia kuhuisha taarifa zote za tovuti za Serikali, ambapo kwa
sasa wataanza na Halmashauri 93 nchini na baadae katika Wizara, Idara, Taasisi
nyingine za Umma.
Bunto anasema mradi
huo ulizinduliwa mapema mwaka huu mkoani Iringa ambapo hadi kufikia mwezi
Agosti mwaka huu, jumla ya mikoa 13 ilifikiwa na taasisi hiyo na kuendesha
mahojiano na Watendaji Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Idara na vitengo mbalimbali.
Anaitaja mikoa hiyo
kuwa ni Iringa, Shinyanga, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Kagera, Mara, Rukwa, Kigoma,
Lindi, Mtwara na Morogoro.
Akifafanua zaidi
anasema katika utafiti uliofanyika ulibaini kuwa mikoa mingi ilianza
kutengezeza tovuti zao lakini hazikikuwa na taarifa muhimu zinazohitajika na wananchi wa kawaida.
“Tovuti ya Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) inatembelewa na watu zaidi ya 500,000 kwa siku, hii
inatokana na mahitaji ya huduma inazotoa TRA kwa wananchi, hivyo mradi huu pia
umekusudia kuzifanya tovuti za Mikoa na Halmashauri kutembelewa na wananchi
wengi zaidi” anasema Bunto.
Kwa mujibu wa Bunto
anasema, mradi huo uliichagua TAMISEMI kutokana na Ofisi hiyo kutoa huduma muhimu zinazomgusa wananchi wa kawaida
ikiwemo afya, maji, elimu, mazingira, uvuvi, ufugaji na kadhalika, ambapo
wananchi wengi wanapenda kufuatilia taarifa na huduma hizo katika ofisi za umma.
Anaongeza uhuishaji
wa taarifa za tovuti utasaidia kutangaza fursa na rasilimali za kiuchumi
zilizopo katika mikoa, hatua itayoziwezesha halmashauri nyingi kuibua vivutio
vya uwekezaji sambamba na kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.



Post a Comment