Header Ads

Serikali imewataka TANROADS kuondoa Matuta ya Barabarani ambayo ni Kero

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akifunga mkutano wa 14 wa siku mbili wa Wahandisi uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Serikali imewataka Mameneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kutojenga na kuondoa matuta ambayo yamekuwa kero kwa watumiaji wa usafiri wa vyombo vya moto katika barabara zote kuu nchini.

Akifunga maadhimisho ya 14 ya wahandisi nchini, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amesema hakuna sababu ya kuweka matuta endapo madereva watatii sheria za usalama barabarani.

“Natambua kuwa mkutano huu umeshirikisha wahandisi kutoka sehemu mbalimbali pamoja na wanataaluma wengine hivyo zingatieni maelekezo ya kutojenga na kuondoa matuta katika barabara kuu ili kurahisisha matumizi sahihi na ya kisasa ya barabara”, amesema Eng. Ngonyani.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB) Profesa Ninatubu Lema akizungumza na wahandisi katika mkutano wa 14 wa siku mbili uliowakutanisha wahandisi wa ndani na nje ya nchi, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wahandisi wakila kiapo mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani katika mkutano wa 14 wa Siku ya Wahandisi uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Aidha Eng. Ngonyani amewataka Mameneja wa TANROADS kutumia njia mbadala ya kuweka alama za vivuko vya waenda kwa miguu (Zebra), na alama za kupunguza mwendo katika barabara kuu ili kuzuia ajali zinazoepukika.

Naibu Waziri huyo amewataka Wahandisi wa Halmashauri kuwa mabalozi wa kutoruhusu kuanzishwa vituo vya biashara katika maeneo ya barabarani na ambayo hayajapangwa na Halmashauri husika, suala ambalo linahatarisha usalama wa wananchi na uharibifu wa miundombinu.

“Hakikisheni wananchi hawafanyi biashara karibu na miundombinu ya barabara kwani kufanya hivyo licha ya kusababisha ajali pia huongeza msongamano”, amesisitiza Eng. Ngonyani.
Baadhi ya wahandisi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (hayupo pichani), katika mkutano wa 14 wa Siku ya Wahandisi uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia Siku ya Wahandisi Eng. Ngonyani amewataka wahandisi hao kutumia fursa kuonesha uwezo wao wa kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuanzisha viwanda na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

“Mkumbuke kutekeleza aliyoagiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kwa kujihusisha katika utekelezaji wa miradi mikubwa nchini ikiwemo miradi ya gesi, bomba la mafuta na ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege”, amefafanua Eng. Ngonyani.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB), Eng. Prof. Ninatubu Lema amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa watatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuja na mpango mkakati wa utekelezaji wake.

Zaidi ya Wahandisi 2500 wameshiriki katika maadhimisho ya 14 ya Siku ya wahandisi na kujadiliana kwa kina namna bora ya utekelezaji wa kauli mbiu ya mwaka huu isemayo ‘Tanzania kuelekea kuwa nchi ya uchumi wa kati na kuwa nchi ya viwanda: Nini jukumu la wahandisi’. 

No comments

Powered by Blogger.