Header Ads

Matumizi ya Nishati Mbadala ya Gesi na Makaa ya Mawe Suluhisho la Uharibifu wa Misitu

 Sehemu ya makaa ya mawe yaliyotengenezwa na Shirika Lisilo la Kiserikali la Mbalawala Women Organization (MWO) la Mkoani Ruvuma kwa ajili ya matumizi ya majumbani.
 Moja ya mashine inayotumiwa na Shirika Lisilo la Kiserikali la Mbalawala Women Organization (MWO) kuchakata makaa ya mawe kwa ajili ya matumizi ya majumbani. 
Jengo ambalo ndani yake kuna tanuri la kuchakata makaa ya mawe ambalo limejengwa kwa msaada wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ikiwa moja ya mkakati wake wa kushirikiana na wadau mbalimbali katika  kuanzisha na kutumia nishati mbadala kunusuru Misitu nchini. Jengo hilo linatumiwa na Shirika Lisilo la Kiserikali la Mbalawala Women Organization (MWO).


Misitu ni muhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe hai kwakua huifadhi vyanzo vya maji, kuboresha hali ya hewa, kuzuia mmomonyoko wa ardhi, upatikanaji wa kuni, mbao, madawa, malisho ya mifugo, kuboresha shughuli za kilimo na kuboresha mandhari ya nchi yetu mijini na vijijini. 

Aidha, misitu pia ni chanzo muhimu cha mapato kwa wananchi wengi wa vijijini na mijini.

Ni kutokana na umuhimu huo wa Misitu ndio maana Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) akapewa jukumu la kusimamia misitu na rasilimali zake kwa niaba ya Serikali Kuu ili iweze kuwanufaisha watanzania wa leo na wa vizazi vijavyo kupitia matumizi endelevu.

Iko wazi kuwa kuna utegemezi mkubwa wa misitu kama chanzo rahisi na kikuu cha nishati nchini, ambapo zaidi ya asilimia 90 ya nishati inayotumika Nchini inatokana na miti. Uvunaji mkubwa wa mkaa umeathiri sana ubora wa misitu. Kuni zinatumika zaidi vijijini na mkaa unatumika zaidi mijini.

Matumizi ya nishati mbadala yanatajwa kama moja ya suluhisho la tatizo hilo, Katika kukabiliana na tatizo la uharibifu wa Misitu Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) inafanya ushirikiano na wadau wa sekta mbalimbali hasa  Wizara ya Nishati na madini na jamii kwa ujumla ili kupunguza utegemezi wa misitu kama chanzo kikuu cha nishati.

Miongoni mwa asasi za kiraia ambazo Wizara inashirikiana nazo katika kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ni Shirika Lisilo la Kiserikali (NGO) la Mbalawala Women Organization (MWO) ambalo lipo katika wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, Makao yake makuu yakiwa katika kijiji cha Ruanda eneo maarufu kwa jina la Center D.

Shirika hilo limejikita katika uwezeshwaji wa vikundi vya wanawake kiujisiliamali ili waweze kujikwamua kiuchumi hasa wanawake ambao wanazunguka mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka uliopo Kata ya Ruanda wilayani Mbinga, wengi wao wameshindwa kuajiriwa na mgodi huo kutokana na ugumu wa shughuli husika ambazo hufanywa na wanaume.

Likiwa limejikita na shughuli za miradi ya utengenezaji wa vitofali vya kupikia vya makaa ya mawe pia lina lengo la kutunza mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti kwa kutengeneza na kuhamasisha jamii juu ya matumizi ya nishati hiyo mbadala.

Akizungumza na Mwandishi wa Makala hii, Meneja wa Uzalishaji wa shirika hilo, Harid Kapinga aliitaja miradi mingine ambayo inafanywa na shirika hilo kuwa ni huduma ya chakula na usafi katika kambi ya mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka, programu ya shule, bustani ya mboga na matunda, shamba la mpunga na ufinyanzi wa vyungu.

Akizungumzia uongezaji wa thamani wa makaa ya mawe ili yaweze kutumika kwa matumizi ya majumbani, Meneja huyo wa Uzalishaji alisema, awali wananchi walikuwa wanaokota makaa ya mawe pembezoni na mgodi na kwenda kupikia bila kujua madhara yake kwa maisha ya binadamu na uharibifu wa vyombo ambavyo walikuwa wanavitumia katika kupikia vyakula vyao.

“Kutokana na umuhimu wa jambo hilo Kampuni ya Tancoal Energy kwa kushirikiana na Mbalawala waliamua kuchukua hatua ya kuongeza thamani ya makaa ya mawe kupitia wataalam na maabara ya mgodi ili yaweze kufaa kwa kupikia majumbani” alisema Kapinga.

Alisema kuwa huwa wanatumia vumbi ambalo linatokana na kukatwa kwa mkaa wa mawe na kupelekwa maabara ili kuweza kubaini kiasi cha athari ya joto lililopo kabla ya kuongezewa thamani kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya majumbani.

Alieleza kuwa joto la Makaa wa mawe ya Ngaka  lipo juu sana kati ya Calorific Value (CV) 5800 hadi 6200 wakati joto linalotakiwa kwa ajili ya kupikia ni kati ya CV - 4200 mpaka 4500 hivyo wataalamu wa maabara huuingiza kwenye mitambo maalum na kuuongezea thamani kwa ya kurekebisha joto linalotakiwa kabla ya matumizi ya majumbani.

Alieleza kuwa wanatengeneza aina mbili za mkaa, wenye umbo dogo kwa ajili ya matumizi ya majumbani na wenye umbo kubwa kwa ajili ya matumizi ya taasisi kubwa kama Shule, Hoteli, Vyuo na Magereza.

Akielezea faida za mkaa huo Kapinga alisema “Miongoni mwa faida za makaa haya ya mawe ni pamoja na unafuu wa bei katika manunuzi, kwa mfano tani moja ya mkaa wa miti ni shilingi 2,225,000 lakini mkaa huu unaotokana na makaa ya mawe tani moja ni shilingi 200,000 ukiyanunua kiwandani kwetu”

Alifafanua kuwa makaa ya mawe yenye umbo dogo kwa bei ya rejareja huuzwa shilingi 200 kwa kilo na kwa ule wenye umbo kubwa ambao unafaa kwa matumizi makubwa huuzwa kwa shilingi 350, na kwa kipande kimoja cha mkaa unaweza ukapikia vitu vingi kwakuwa toka kuwaka kwake mpaka kuwa jivu huchukua zaidi ya masaa manane.

Alitaja faida nyingine kuwa ni uhifadhi na utunzaji wa misitu kwakuwa matumizi ya makaa ya mawe yataepusha utegemezi wa rasilmali za misitu kama nishati pekee ya kupikia, aliongeza kuwa utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa uchimbaji wa makaa ya mawe unaweza kuchukua zaidi ya miaka 100, hivyo ukitumika ipasavyo unaweza kuokoa uharibifu wa misitu.

Akizungumzia hali ya soko alisema kuwa ulifanyika utafiti wa mwaka mmoja na baada ya hapo wakaanza uzalishaji kisha elimu kwa wananchi ikatolewa katika vitongoji 8 ambavyo vina zunguka mgodi huo kuhusu matumizi bora ya makaa ya mawe, pia elimu hiyo ilitolewa kwenye vikundi mbalimbali ambavyo vinauza mkaa wa kuni, kwenye maonesho mbalimbali kama Saba Saba na makongamano.

“Watumiaji wengi wamehamasika sana kutumia mkaa huu na mawakala pia wamepatikana kwa ajili ya kusambaza mkaa huu nchi nzima na sasa tunajipanga kwa uzalishaji mkubwa zaidi kwani majaribio ya utengenezaji yameshafanyika na kukamilika” alisema Kapinga.

Alisema kuwa matokeo ya majaribio hayo yameonyesha mafanikio makubwa kutokana na mwitikio wa wananchi kwani vitofali vina ubora vimetengenezwa kwa kutumia mavumbi ya makaa ya mawe na malighafi zingine na wananchi wanaendelea kuvitumia katika shughuli zao za kila siku kuzunguka mgodi.

Akizungumzia ushirikiano baina yao na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) alisema, ushirikiano wao ni mzuri sana kwa kuwa wamepatiwa fedha za kujengea jengo na tanuri la kuchakatia makaa ya mawe, ingawa bado kuna changamoto ya mitambo ya kuzalishia pamoja na umeme wa uhakika.

“Mradi huu ni muhimu sana hivyo tunaziomba Taasisi na Serikali ziweze kutusaidia kukabiliana na changamoto zinazotukabili katika uzalishaji ili tuweze kufanikiwa kusambaza mkaa huu nchi nzima na kufanikisha kampeni ya utunzaji wa misitu kwa kutumia nishati mbadala kwani bila nishati mbadala kamwe vita ya utunzaji wa misitu haiwezi kushinda” alisema Kapinga.

Awali Meneja huyo wa Uzalishaji alisema kuwa Mbalawala Women Organization ni matokeo ya juhudi za Tancoal Energy Limited katika kuisaidia jamii inayozunguka mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka na kwamba Shirika la Mbalawala Women Organization limeundwa na vijiji vya Ruanda na Ntunduwaro, Tancoal Energy Limited na kikundi cha Umoja wa Wanawake Mbalawala (Mbalawala Women Association).

Alisema kuwa Ruanda na Ntunduwaro ni vijiji jirani vinavyozunguka mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka ambapo Umoja wa Wanawake Mbalawala ni kikundi cha wanawake walioungana kutoka vijiji vya Ruanda na Ntunduwaro.

Tancoal ni mwekezaji wa mgodi wa makaa ya mawe ya Ngaka na maana ya neno Mbalawala limetokana na jina la mto uliopo karibu na eneo la mgodi mmojawapo wa machimbo ya Ngaka wilayani Mbinga.

Wakati huo huo baadhi ya wananchi wa Dar es Salaam wametoa maoni yao tofauti juu ya dhana ya rasilimali za misitu kuwa ndiyo nishati rahisi zaidi nchini na kueleza kuwa matumizi ya nishati mbadala hususani gesi asilia katika matumizi ya kupikia ni rahisi zaidi na ina faida nyingi kuliko matumizi ya mkaa wa miti.

Anthony Ntiina ni Mkazi wa Kata Mwinjuma Wilaya ya Kinondoni, amesema yeye na familia yake ya watu watano hutumia nishati ya gesi kupikia na wamegundua faida nyingi za kiuchumi kwakuwa hutumia kiasi kidogo cha fedha katika nishati hiyo kuliko walivyokuwa wakitumia nishati ya mkaa hapo awali.

“Nilikuwa natumia karibu 4,000 kila siku kununua mkaa wa reja reja, kwa wiki mbili ilinigharimu shilingi 60,000. Kwa sasa natumia nishati ya gesi kupikia ambapo kwa wiki mbili hutumia mtungi wa gesi wa kilo sita ambao kuujaza hunigharimu shilingi 18,000 tu, hiyo ni faida kubwa” alisema Ntiina.

Alisema kwa sasa ameacha kabisa matumizi ya mkaa kwa kuwa hayana faida kiuchumi na athari zake kimazingira ni kubwa ukilinganisha na gesi ambayo matumizi yake ni rahisi na hupika kwa haraka zaidi.

Kwa upande wake mfanyabiashara, Hassan Rashid Ally ambaye ni wakala wa mitungi ya Oryx maeneo ya Mkwajuni Wilaya ya Kinondoni, amesema tatizo lililopo kwa baadhi ya wananchi ni uoga wa kuingia kwenye matumizi ya gesi wakiamini kuwa nishati hiyo ni ghali zaidi kuliko matumizi ya mkaa ambayo wameyazoea jambo ambalo sio la kweli.

Hassan alisema kuwa kwa sasa bei ya kununua mtungi na gesi ya kilo 15 ni shiingi 85,000 na bei ya kujaza mtungi mtupu ni shilingi 45,000. Kwa upande wa mtungi wa kilo 6 alisema unauzwa shilingi 70,000 pamoja na jiko lake na hujazwa kwa shilingi 18,000.

Alisema ukipiga mahesabu ya matumizi ya kawaida, mtungi wa kilo 15 huweza kutosha familia ya watu watano kwa zaidi ya mwezi mmoja. Akifananisha matumizi hayo na yale ya mkaa alisema kiwango cha mkaa kwa mwezi kwa ukubwa wa familia kama hiyo hata kama wanatumia kiwango cha chini kabisa cha 2,000 kwa siku, kwa mwezi itakua shilingi 60,000 matumizi ambayo ni ghali zaidi ukilinganisha na bei ya kujaza mtungi wa kilo 15 ambao ni shilingi 45,000 na bado matumizi yake huweza kuzidi mwezi mmoja.


Aliongeza kuwa kinachotakiwa ni wananchi kuacha uoga na kuwa na mtaji kidogo wa kuweza kumiliki mtungi wa gesi na jiko lake kwa wale watakaotumia mitungi mikubwa kuanzia kilo 15 kwenda juu na kuanza mara moja matumizi ya nishati ya gesi ambapo wataona faida zake kiuchumi na kimazingira. 

NA HAMZA TEMBA - WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

No comments

Powered by Blogger.