Header Ads

Maalim SEIF SHARIF HAMAD ajinadi kwa Wananchi Katika Jimbo la MKWAJUNI

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia wafuasi wa chama hicho katika viwanja vya jimbo la Mkwajuni.
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikabidhi kadi kwa mmoja kati ya vijana 39 wa jimbo la Mkwajuni waliojiunga na CUF.
Wafuasi na wapenzi wa CUF wakifuatilia mkutano huo.   
Na: Hassan Hamad (OMKR)

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema anakusudia kuuzindua rasmi mpango wake wa kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki mwishoni mwa wiki hii.
 
Amesema anapozungumzia mpango huo huwa hafanyi utani bali anazungumza akiwa na mikakati maalum ya kuweza kuibadilisha Zanzibar kufikia lengo hilo.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ametoa kauli hiyo wakati akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa Chama hicho katika viwanja vya Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
 
Amesema tayari chama hicho kimeshapanga mikakati imara ya kuweza kuikomboa Zanzibar kiuchumi katika kipindi kifupi kijacho iwapo atachaguliwa kuiongoza Zanzibar.
 
Akizungumzia mafanikio ya safari yake ya kichama nchini Afrika ya Kusini, amesema alikutana na viongozi wa makampuni mbali mbali ya nchi hiyo ambao walikubali kushirikiana nae kuikomboa Zanzibar kiuchumi iwapo atachaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi mkuu ujao.
 
Kuhusu matarajio ya ushindi kwa chama hicho Maalim Seif amesema kina matarajio makubwa ya kupata ushindi na kuapa kuwa hakuna atakayeweza kuzuia mabadiliko hayo.
 
Amesema wananchi wa Zanzibar wameshajiika kuleta mabadiliko na kuwahimiza kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuweza kufikia malengo hayo.
Ameishauri Tume ya uchaguzi ya Zanzibar kujiandaa kutoa matokeo ya uchaguzi mapema, ili kuzuia vurugu zinazoweza kuepukika.
 
“Inawezekana kabisa kutoa matokeo siku hiyo hiyo kwa majimbo 54 ya Zanzibar. Naamini kuwa ikifika saa sita za usiku matokeo yote ya Zanzibar yatakuwa yamekamilika, hivyo Tume wajitahidi wayatangaze ili wananchi wapate kutulia” alieleza.
 
Maalim Seif amesisitiza haja ya kuwepo kwa uchaguzi wa amani, na kuwata vijana wa chama hicho wasikubali kuchokozeka na kupelekea kuvunjika kwa amani ambayo ni hazina kubwa kwa taifa.
 
Kuhusu Masheikh wa Jumuiya ya Uamsho wanaoshikiliwa Tanzania Bara, Maalim Seif amesema siku zao za kukaa ndani sasa zinahesabika kwani iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar atawarejesha masheikh hao Zanzibar ndani ya kipindi cha wiki moja baada ya kuapisha.
 
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amesema iwapo Maalim Seif atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, atayarejesha yale yote yaliyoahidiwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za elimu na afya bila ya malipo.
 
Mjumbe wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Janeth Fussi akizungumza katika mkutano huo amesema Maalim Seif anatosha na anavyo vigezo vyote vya kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar.

No comments

Powered by Blogger.