Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya
habari wakifuatilia ufafanuzi wa Gavana wa Benki Kuu kuhusu masuala mbalimbali
ya uchumi nchini - Picha/ Aron Msigwa –MAELEZO.
Na
Lilian Lundo na Abushehe Nondo- MAELEZO.
Gavana wa Benki Kuu
ya Tanzania (BOT), Prof. Benno Ndulu amesema kuwa hakuna mdororo wa uchumi
nchini bali uchumi wa Tanzania umeendelea
kukua kwa kiwango cha asilimia 5.5 kwa kipindi cha robo ya kwanza ya
mwaka 2016.
Aidha, amesema kuwa
Tanzania ni kati ya nchi kumi bora za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi
ya haraka.
Prof. Ndulu ameyasema
hayo leo jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
juu ya hali ya uchumi nchini.
“Kwa mujibu wa Takwimu
ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa, hali ya ukuaji wa wa Tanzania imeendelea kuwa ya kuridhisha,
ambapo katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ukuaji wa pato la Taifa unakadiriwa
kuongezeka kwa asilimia 5.5” Prof. Ndulu.
Prof. Ndulu amezitaja
shughuli zinazochangia kasi ya ukuaji wa uchumi kuwa ni pamoja na sekta ya,
kilimo asilimia 11.7, biashara asilimia 10.6, uchukuzi asilimia 10.1, fedha
asilimia 10.1 na mawasiliano asilimia 10.0.
Kwa mujibu wa Prof.
Ndulu amesema shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi ya juu zaidi katika robo
ya kwanza ya mwaka 2016 ni sekta ya fedha asilimia 13.5, mawasiliano asilimia
13.4 na utawala wa umma asilimia 10.2.
Kuhusu mchango wa
Sekta mbalimbali katika kuchangia kuleta fedha za kigeni nchini amesema kuwa
Kilimo cha mazao yote kinachangia asilimia 25 ambazo ni dola za Kimarekani
milioni 850, Utalii ukiongoza kwa dola bilioni 2.5, Viwanda dola bilioni 1.5 na
dhahabu dola bilioni 2.5, usafirishaji kwenda nje bilioni 1.1.
Akizungumzia deni la Taifa, Prof. Ndulu amesema kuwa kiwango cha deni hilo kwa sasa ni asilimia 20
ya pato la Taifa ambayo si mbaya ikilinganisha na ukomo wa asilimia 50 ya Pato
la Taifa.
Prof. Ndulu
amebainisha kuwa kulingana na tafsiri ya uchumi kuhusu deni hilo, Tanzania bado
ina nafasi kubwa ya kuendelea kukopa bila kuhatarisha ustahimilivu wa deni
hilo.
Katika hatua
nyingine, Prof. Ndulu ametoa ufafanuzi kuhusu mapato katika bandari ya Dar es Salaam kuwa
yameongezeka licha ya kupungua kwa uingizwaji wa mizigo kupitia bandari hiyo.
Kuhusu mfumuko wa
bei, Prof. Ndulu amesema bei za bidhaa mbalimbali zimeendelea kushuka na kufikia
asilimia 4.9 kwa mwezi Agosti, ambapo
kushuka kwa kiwango hicho kulichangiwa na bei zisizojumuisha vyakula na
nishati.
Prof. Ndulu pia amesema
Serikali inaendelea na umaliziaji na uendelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu
ikiwa ni pamoja na mradi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard
gauge), ujenzi wa bomba la mafuta la Uganda na upanuzi wa bandari ya Tanga.
Aliitaja miradi
mingine kuwa ni pamoja na ujenzi wa kanda
maalum ya uwekezaji, mradi wa kuzalisha megawati 240 za umeme wa
Kinyerezi II ambapo miradi hiyo itachangia katika kuimarisha uchumi wa nchi.
|
Post a Comment